Huenda Afrika Kusini ikaunda serikali ya mseto – DW – 01.06.2024

Afrika Kusini huenda ikaunda serikali ya mseto kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo kufuatia uchaguzi wa bunge uliofanyika nchini humo.

Huku asilimia 80 ya kura zikiwa zimekwisha kuhesabiwa, chama tawala cha African National Congress (ANC)kimefikia 41.37% ya kura zote kufikia jana jioni. Hii ni kulingana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEC).

ANC yaonesha kupoteza wabunge wengi

Matokeo ya awali yanaonyesha hali ya kupoteza wingi wa viti vya bunge kwa chama hicho tawala cha Rais Cyril Ramaphosa, ambacho kilipata 57.5% ya kura katika uchaguzi wa bunge uliofanyika 2019.

Soma pia:Afrika Kusini yasubiri matokeo ya uchaguzi mkuu na majimbo

Ikiwa chama hicho cha ANC kitasalia chini ya alama ya asilimia 50 ya kura kama inavyoonekana kuwa hali kwasasa, kitabidi kuunda muungano.

ANC imeongoza Afrika Kusini kwa takriban miaka 30

Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, tangu kuanza kwa demokrasia nchini humo mnamo mwaka 1994, ANC imekuwa ikishinda chaguzi kwa wingi wa kura na kuongoza taifa hilo lililoimarika zaidi kiuchumi barani Afrika bila miungano.

Soma pia:Raia wa Afrika Kusini washiriki uchaguzi Mkuu

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kinachoongozwa na John Steenhuisen, mpaka sasa kimefikia 22.16% ya kura huku chama kilichoanzishwa miezi sita tu iliyopita na rais wa zamani Jacob Zuma, uMkhonto we Sizwe (MK), kikijipatia asilimia 13.06 ya kurakufikia sasa na kile cha wapigania ukombozi wa kiuchumi, EFF, cha Julius Malema kikifikia asilimia 9.41 ya kura.

Maafisa wa uchaguzi wa kujitolea wahesabu kura katika shule ya msingi ya Craighall Park iliyoko Johannesburg, Afrika Kusini, Jumatano Mei 29, 2024
Zoezi la kuhesabu kura laendelea Afrika KusiniPicha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Kulingana na matokeo ya awali, ANC pia itapoteza wingi wa kura katika jimbo lililoimarika kiuchumi la Gauteng, ambapo unapatikana mji mkuu Pretoria na kitovu cha biashara cha Johannesburg.

Soma pia:Raia nchini Afrika Kusini waanza kupiga kura ya mapema

ANC pia inatarajiwa kupata kura ya chini ya 50% katika eneo la KwaZulu-Natal, nyumbani kwa kina Zuma.

Jimbo la Cape Magharibi, ambalo ni la pili kwa nguvu kiuchumi uliko mji wa Cape Town limetawaliwa kwa miaka mingi na chama cha DA. Matokeo ya awali yanaashiria kuwa chama hicho kitahifadhi wingi wake wa kura katika eneo hilo.

Mei 29, wanachama wa vyama 52 walishirika katika uchaguzi huo wa bunge kugombea viti 400 katika bunge la taifa.

Bunge litakalochaguliwa litahitajika kuunda serikali

Bunge jipya litakalochaguliwa lazima liunde serikali na kumchagua rais ndani ya siku 14 baada ya tangazo la mwisho la matokeo.

Hasara za kihistoria zaANC katika uchaguzi, zinaweza kuhusishwa na rekodi yake dhaifu serikalini.

Changamoto zinazowakabili wananchi Afrika Kusini

Taifa hilo lenye idadi ya watu milioni 61, linakabiliwa na uchumi mbaya pamoja na kiwango kikubwa cha ukosefu ajira .

Mara kwa mara umeme unakatwa pamoja na viwango vya juu vya uhalifu na rushwa.

 

Related Posts