Singida. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Serikali inatarajia kuongeza kodi kwenye mafuta ya kula yanayotoka nje ya nchi katika bajeti ya mwaka 2024/25, ili kuwalinda wakulima wa alizeti.
Pia, inakwenda kujenga soko kubwa na la kisasa la vitunguu mkoani Singida, na ujenzi wa mradi mkubwa wa umwagiliaji mkoani humo wenye thamani ya zaidi ya Sh10 bilioni.
Bashe amesema hayo katika mkutano wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi jana, aliposimama kuwasalimia wananchi wa Itaja, mkoani hapa.
Dk Nchimbi amesimama akiwa ziarani kutoka Singida kwenda Manyara kuendelea na ufuatilia wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi, kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Awali, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Ramadhan Ighondo amesema licha ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, wananchi hao kwa sehemu kubwa ni wakulima, hivyo wanaomba kujengewa soko la mazao.
Ighondo ameomba kusaidiwa wakulima wa ndani, wakiwemo wa alizeti ili kuwa na soko la uhakika.
Baada ya ombi hilo, Dk Nchimbi alimpigia simu Waziri Bashe kujibu changamoto hizo.
Bashe amesema suala la soko ameagiza liandaliwe eneo na liwe na hati yenye jina la Singida Vijijini na halmashauri ili lisije kubadilishwa siku za usoni.
Dk Nchimbi amemweleza Bashe anataka soko hilo ujenzi wake ukamilike kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa 2025 na Waziri Bashe alijibu: “Nimepokea.”
Kuhusu kuwalinda wakulima wa ndani, Waziri Bashe amesema: “Nimekwishazungumza na Waziri wa Fedha, tunakwenda kuongeza kodi katika mafuta yanayotoka nje ili kuwalinda wazalishaji wa alizeti.
“Hili litafanyika katika Bajeti ya Serikali itakayosomwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba Juni 13, 2024.”
Baada ya kumaliza hilo, Dk Nchimbi amesema: “Mazao yanayotokana na alizeti yanapatikana kwa wingi nchini, ni vizuri wakulima wakaneemeka na mazao yao.”
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, kwa mwaka 2023/24, zaidi ya nusu ya mafuta yaliyozalishwa nchini, sawa na asilimia 52 yalikuwa ya alizeti, yakifuatiwa na asilimia 27 ya mafuta yaliyotokana na karanga.
Hata hivyo, uzalishaji huo wa bidhaa za mafuta unakidhi nusu ya mahitaji, hivyo kufanya nusu nyingine kuagizwa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa wizara, uzalishaji wa alizeti uliongezeka zaidi ya mara mbili kutoka tani 425,653.1 msimu wa 2021/2022 hadi tani 1,132,298.34 msimu wa 2022/2023.
Pia uzalishaji wa alizeti kwa hekta umeongezeka kutoka tani 0.8 hadi tani moja kwa hekta, sawa na ongezeko la asilimia 30, huku lengo likiwa kuzalisha tani nne kwa hekta.
Wizara imeeleza tani 725 kati ya tani 1,974.4 za mbegu bora za alizeti zimesambazwa kwa wakulima kupitia mpango wa ruzuku mikoa ya Singida, Dodoma, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Geita hadi Aprili 2024.
Akigusia kilimo cha umwagiliaji, Waziri Bashe amesema kuna zaidi ya Sh10 bilioni zimetengwa kwenye bajeti ijayo ili kujenga Bwawa la Msangi ambalo litakuwa mkombozi kwa wananchi na kuendeleza kilimo pasi na kutegemea mvua.
“Tayari mkandarasi amepatikana na yupo eneo la mradi. Nikuhakikishie katibu mkuu na wananchi wa Singida kwa ndugu yangu Ighondo mradi utakamilika kwa wakati,” amesema Bashe.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha afya eneo hilo ambalo limeibuliwa na Mbunge Ighondo, Dk Nchimbi amemwelekeza Waziri wa Tamisemi, kuhakikisha ujenzi unaanza Agosti 2024 na atafika mwezi huo kukagua kama Serikali inatekeleza maagizo ya chama.