Yanga, Azam acha kipigwe fainali Shirikisho

MWISHO wa ubishi. Ndivyo unavyoweza kusema wakati Azam FC na Yanga zitakapovaana katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho.

Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja Zanzibar, ikiwa ni mara ya kwanza kwa pambano la michuano hiyo kupigwa huko.

Timu hizo zinakutana katika fainali hiyo ya tisa tangu michuano hiyo iliporejeshwa upya nchini msimu wa 2015-2016 baada ya awali kusimama kwa karibu miaka 10 enzi ikifahamika kama michuano ya Kombe la FA ambalo lilizimika mwaka 2002 wakati JKT ilipoifunga Baker Rangers ya Magomeni.

Kuanzia mwaka 2003 hadi 2014 michuano ilikuwa haichezwi, ndipo mwaka 2015 Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likairejesha michuano hiyo baada ya kupatikana kwa udhamini kutoka Azam Media na kupewa jina la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na mechi ya fainali ya kwanza ilipigwa Kwa Mkapa.

Katika mechi hiyo, Yanga iliendeleza rekodi ya kulibeba taji la michuano hiyo ikiwa ni ya kwanza kama ilivyofanya ilipoasisiwa mwaka 1967 kwa jina la Kombe la FAT ilipoifunga Liverpool ya Ilala kwa mabao 2-0.

Yanga ilitwaa taji la kiwanza la ASFC kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Azam FC, kabla ya kuja kupokewa na Simba msimu uliofuata ilipoitungua Mbao FC kwa mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kuchezwa kwa dakika 120.

Rekodi zinaonyesha kuwa, tangu kurejea kwa michuano hiyo mwaka 2015 imechezwa kwenye mikoa saba tofauti, huku jiji la Arusha likiongoza kwa kuzibeba fainali hizo mara mbili zilizopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Arusha ilianza msimu wa 2017-2018 pale Singida United ilipovaana na Mtibwa Sugar na Wakata Miwa wa Manungu wakaibuka wababe kwa ushindi wa mabao 3-2 kisha zikafanyika tena ‘Chugga’ misimu miwili iliyopita.

Fainali hiyo ya pili kwa jiji hilo kuandaa ilizikutanisha Yanga na Coastal Union na mechi kupigwa kwa dakika 120 na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 kabla ya mikwaju ya penalti 4-2 kuipa Yanga taji la pili la michuano hiyo tangu iliporejea.

Jiji la Dar ndilo lililokuwa la kwanza kuandaa fainali za ASFC na kushuhudiwa Yanga ikiikanda Azam kwa mabao 3-1, kisha fainali zilizofuiata zikahamishwa jijini Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri na Simba kulitwaa taji mbele ya Mbao FC iliyokuwa imepanda Ligi Kuu Bara kwa msimu huo.

Baada ya fainali hizo ndipo jiji la Arusha likapewa nafasi ikiwa ni fainali ya tatu, kisha ngoma kupelekwa mkoani Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu, ambako Azam ilimalizana na Lipuli ya Iringa na kuibuka ushindi kwa bao 1-0 lililofungwa na Obrey Chirwa. Hiyo ikiwa ni fainali ya nne.

Mkoa wa Rukwa katika mji wa Sumbawanga nao ukapata heshima ya kuandaa fainali ya tano ya ASFC iliyozikutanisha Simba na Namungo iliyokuwa imepanda Ligi Kuu msimu huo na Simba ilishinda mabao 2-1, meehi ikipigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.

Fainali ya sita ilipigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma kwa kuzikutanisha Simba na Yanga, ikiwa ni Kariakoo Derby ya kwanza kupigwa mkoani humo na Mnyama alimtafuna Mwananchi kwa bao 1-0.

Ndipo msimu wa 2021-2022 fainali zikarudishwa tena jijini Arusha kwa kuwakutanisha Wagosi wa Kaya, Coastal Union dhidi ya Yanga zikiwa ni fainali za saba tangu michuano hiyo kurejeshwa na la nne kwa Yanga, ilipelekwa Mkwakwani, jijini Tanga ambako Yanga ilikutana na Azam FC.

Hiyo ilikuwa ni fainali ya tatu mfululizo kwa Yanga na turufu ikawa upande wao kwa kupata ushindi wa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Mzambia Kennedy Musonda na kutwaa taji la tatu tangu kurejeshwa kwa michuano hiyo.

Safari hii ikiwa ni fainali ya tisa, inapelekwa visiwani Zanzibar, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mechi ya Kombe hilo kupelekewa huko.

Jambo hilo limeletea sintofahamu kwa baadhi ya mashabiki kutokana na ukweli Zanzibar licha ya kuwa ni sehemu ya Muungano wa Tanzania, lakini yenyewe ina michuano kama hiyo ambayo kwa sasa ipo hatua ya fainali na itazikutanisha Uhamiaji dhidi ya JKU zilizozing’oa Mlandege na Zimamoto.

Sintofahamu hiyo imetokana na ukweli hivi karibuni Simba ilikuwa ikitoa taarifa ya kutaka kupeleka mechi zao za Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Amaan, lakini ilizuiwa kwa kanuni zinazoelekeza mechi za Ligi Kuu Bara zitachezwa katika ardhi ya Tanzania Bara na sio vinginevyo.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba michuano ya Kombe la Shirikisho kwa Bara licha ya kuwa na kanuni, lakini imetoa nafasi kwa TFF kuwa ndio wenye mamlaka ya kuchagua mechi za nusu fainali au fainali kupigwa wapi.

Ndio maana mara zote nane katika fainali zilizopita zilikuwa zikitangazwa na TFF mapema na hata safari hii awali zilikuwa zipigwe kwenye Uwanja wa Tanzanite, uliopo Manyara lakini ghafla ulibadilishwa baada ya matukio yaliyojitokeza katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa jijini Arusha kati ya Yanga na Ihefu.

Katika fainali hizo, mashabiki walijazana pononi uwanjani na wengine waliokuwa na tiketi zao walibaki nje na kuanzisha timbwili ambalo lilitishia usalama, ndipo saa chache baadaye TFF ikaamua kuipeleka fainali hiyo ya tisa kwenye Uwanja wa New Amaan, Unguja na kesho kazi inamalizwa kuanzia saa 2:15 usiku.

Mashabiki wa soka visiwani Zanzibar walitoa maoni yao mapema kwamba wanafurahia kupelekewa fainali hiyo ya kibabe, kwani ni muda hawajaziona Yanga na Azam zikimalizana visiwani humo.

Wanasema licha ya Yanga kucheza michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, lakini hawakwenda na mashine zao zote za kikosi cha kwanza zilizokuwa kwenye majukumu ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika Ivory Coast.

Pia hata katika michuano mipya ya Kombe la Muungano, Yanga haikwenda na badala yake Azam FC na Simba zilienda na kucheza fainali na Mnyama kubeba ubingwa.

Hivyo wanaamini kesho usiku watamuona Stephane Aziz KI wanayemsikia tu na kumuona kwenye runinga.

Watauona mziki wa Pacome Zouzoua. Watamuona Diarra Djigui wanayemsikia tu makali yake na wakali wengine akiwamo Yao Kouassi waliyemuona tu mazoezini visiwani humo, lakini hakucheza mechi yoyote.

Lakini hata kwa upande wa Azam, licha ya kwamba ilicheza michuano ya Mapinduzi na Muungano, lakini wangetaka kushuhudia bato ya Wana Zanzibar, Feisal Salum ‘Fei Toto’ dhidi ya Ibrahim Bacca anayetokea visiwani humo.

Wangependa kuona pia kazi ya Mudathir Yahya na Shekhan Ibrahim wote wa Yanga mbele ya nyota wa Azam FC akiwamo mbaya wa timu ya Wananchi, Abdul Suleiman ‘Sopu’ ambaye katika fainali ya msimu wa 2021-22 kule Arusha aliifunga Yanga mabao matatu (hat-trick) wakati huo akiitumikia Coastal Union.

Azam wataingia na uwanjani kesho na kumbukumbu ya kuipiga Yanga 2-1 katika mechi yao ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na kuifanya mechi hii kuwa ngumu sana.

Kiufupi Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kesho utadamshi na pira litapigwa na mwishowe bingwa wa Kombe la Shirikisho la Bara atapatikana kwenye ardhi ya Zanzibar.

2015-2016- Benjamin Mkapa Dar

2016-2017- Jamhuri, Dodoma

2017-2018- Sheikh Amri Abeid, Arusha

2019-2020- Nelson Mandel, Rukwa

2020-2021- Lake Tanganyika, Kigoma

2021-2022- Sheikh Amri Abei, Arusha

2022-2023- Mkwakwani, Tanga

2023-2024- New Amaan, Zanzibar

MABINGWA SHIRIKISHO TANGU ENZI ZA KOMBE LA FAT

Related Posts