UNGUJA. Yanga inafanya mambo kama ipo Ulaya vile. Leo hii imewaacha watu wengi midomo wazi baada ya kutambulisha kifaa kipya cha mazoezi kwa makipa wao wakiongozwa na kipa namba moja, Djigui Diarra.
Awali, Yanga ilitambulisha vifaa tofauti mazoezini ikiwemo ‘ball launcher’ ambacho kinatumika kama mbadala wa wachezaji kuwapigia makipa mashuti langoni.
Kikosi hicho kinajiandaa na mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Azam utakaopigwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan, Abdul Suleiman ‘Sopu’ anayemtesa sana Diarra wanapokutana sambamba na Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyemtungua mechi ya mwisho katika Ligi Kuu Bara.
Yanga katika kujiandaa na mchezo huo wa kesho Kocha Mkuu, Miguel Gamondi aliyekuwa akiwapigisha tizi mastaa wa timu hiyo kwenye Uwanja wa Amaan Kwa Wazee, alikitambulisha kifaa hicho katika siku ya pili ya mazoezi.
Kifaa hicho cha kisasa ni kama miwani ambacho kitaalamu kinaitwa Strobe Eyewear au Strobe Glasses, ambapo Kocha wa Makipa wa Yanga, Alaa El Meskini, alikuwa akiwanoa Diarra, Aboutwalib Mshery na Kassim, huku wakiwa wamevaa kifaa hicho machoni ilhali wakipigiwa mipira na kudaka kwa ufasaha.
Kifaa hiki kimetengenezwa maalumu kwa ajili ya kumfanya mtumiaji kufanya uamuzi wa haraka na sahihi kwani macho yanapoona basi taarifa hufika kwa haraka zaidi kwenye ubongo.
Unapovaa kifaa hicho, uchakataji wako wa taarifa unakuwa wa haraka zaidi jambo linalofanya utendaji wako wa kazi kuwa wa kasi na fasaha.
Kipa akivaa kifaa hicho humfanya kudaka michomo mingi kwa usahihi na nadra sana kuruhusu kufungwa kwani macho yake yanapouona mpira, taarifa inafika kwa haraka kwenye ubongo na kurudisha majibu kwa kasi ambayo humfanya kuwa tayari kufanya uamuzi sahihi.
Thamani ya kifaa hicho inasimama katika Dola za Marekani 299 ambazo ni takriban Sh774,506.
FAIDA ZA KIFAA HICHO
Zipo faida kadhaa za kuvaa kifaa hicho ikiwamo kuongeza umakini. Hii inaanya macho kuwa kwenye tukio jambo linalomfanya kipa aende sawasawa na hali ya mchezo.
Akitumia kifaa hicho, pia huyawezesha macho yake kuona vizuri zaidi ya ilivyo kawaida na pia humfanya kuwa mwepesi katika kufanya uamuzi ulio sahihi.
Faida nyingine ni kuufanya mwili wako kuwa kwenye sehemu sahihi ya kufanya uamuzi kwani kinakupa uwezo wa kuona pembeni na mbele yako kuna hatari gani.
MAANA KWA YANGA
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wanafahamu kwamba Jumapili wana kibarua kigumu mbele ya Azam katika mchezo wa fainali, hivyo wanajiandaa kwa namna yoyote wasipoteze.
Inafahamika wazi kwamba, mchezo wa fainali kama ikitokea matokeo yakawa sare, basi mikwaju ya penalti itaamua mshindi na Yanga imekuwa haipo vizuri sana ikifika hatua hiyo kwani inakumbuka katika Ngao ya Jamii msimu huu dhidi ya Simba, ilipoteza.
Lakini, Yanga wanakumbuka msimu huu walipokutana na Azam mara mbili kwenye ligi kuu, waliruhusu mabao manne na wao wakifunga manne, lakini mabao waliyoruhusu yalionekana kama kipa wao alishindwa kufanya uamuzi wa haraka kutokana na mashambulizi waliyofanyiwa.
Hivyo uamuzi wa kutumia kifaa hiki unaendana na jambo hilo, kwanza ifahamike kwamba mabao ya penalti na faulo yanaitesa sana Yanga hasa inapocheza na timu kubwa kwani macho huwa na kawaida ya kuona jambo lakini mwili unashindwa kuchukua uamuzi wa haraka kutenda, kulingana na kasi ya mpira matokeo yake kipa anashtuka nyavu zinatikisika.
Ukiangalia mechi ambayo Azam ilishinda 2-1 dhidi ya Yanga, bao la kwanza lililofungwa na Gibril Sillah, Diarra alishindwa kuokoa hatari na kuwafanya walinzi wake kujigonga kabla ya kumfikia mfungaji.
Bao la pili, ilipigwa krosi ambayo Diarra akiwa amebana kwenye nguzo, Feisal Salum akafunga palepale.
Kutokana na hilo, utumiaji wa kifaa hiki huongeza ufanisi wa macho katika utendaji wake wa kazi, hivyo humsaidia kipa kuokoa hizo hatari hasa zile za kushtukiza. Kumbuka kwamba kifaa hiki hakitumiki kwenye mechi, kinaishia mazoezini tu, lakini matumizi yake yana faida kwani ukitumia kisha ukakiacha na kwenda kudaka kawaida, bado uwezo wako wa kuona na kufanya uamuzi wa haraka huwa mkubwa.