Kompany, mazalia ya Pep yasikushangaze sana

MDOMO wazi? Kwamba? Vincent Kompany ni kocha mpya wa Bayern Munich? Kashangae vitu vingine. Hili halishangazi sana. Dunia inazunguka katika mhimili wake na wanadamu wapo kazini wakiendelea kumuamini mtu anayeitwa Pep Guardiola pamoja na mazalia yake.

Wengi wameshangaa hili. Mtu ambaye ameishusha Burnley daraja, lakini sasa ameteuliwa kuwa kocha wa Bayern Munich, moja kati ya timu bora duniani, lakini timu kubwa zaidi katika ile ya Ujerumani. Nchi ya walevi. Imekwendaje hii? Bayern wameingia katika mkumbo wa kuyaamini mazalia ya Guardiola.

Inachosha kurudia kwamba kuna mpira mpya umeingia duniani muasisi wake akiwa Guardiola. Makocha wengi vijana wamemuiga katika staili hii ya mpira. Wengine wamepita katika mikono yake. Wengine hawajapita katika mikono yake lakini wametoboa. Waliopita katika mikono yake ni kama hawa kina Mikel Arteta na Kompany.

Ambao hawajapita lakini wanatoboa ni kama Xabi Alonso. Huyu Mhispaniola amewasumbua Bayern Munich katika namna ya kushangaza kule Ujerumani. Timu yake, Bayer Leverkusen ilikuwa moto kuanzia mwanzo wa msimu mpaka mwisho wa msimu. Kwa mara ya kwanza katika historia ikatwaa taji la Bundesliga. Na walifanya hivi kwa kucheza bila ya kupoteza pambano lolote la soka.

Bayern wametafuta jibu la mpira huu na wameangukia kwa Kompany. Kinachoshangaza cha kwanza ni kwamba wameangukia kwa mtu ambaye alishinda mechi sita tu katika Ligi Kuu England msimu uliopita na kuishusha daraja timu ambayo yeye mwenyewe ndiye ambaye aliipandisha kwa kishindo kikubwa msimu mmoja kabla.

Lakini kinachoshangaza ni kwamba Bayern Munich wamekwenda kwa kocha mweusi. Sikumbuki kama wamewahi kufundishwa na kocha mweusi. Ni kama ilivyo kwa klabu nyingine kubwa barani Ulaya. Kufundishwa na kocha mweusi wamesema hapana. Hawa kina Kompany na Patrick Vieira anga zao zilionekana ni kuwa katika timu za mitaa ya kati kama Crystal Palace na Burnley.

Lakini sasa Bayern wamejitwika Kompany, staa wa zamani wa Manchester City. Mwanafunzi wa Guardiola. Kwanini wamechukua uamuzi huo? Ni rahisi kufikiria. Nadhani wanaamini kwamba Kompany alikosa pesa kuiwezesha Burnley kutamba Ligi Kuu. Sawa, mpira upo, falsafa zipo, lakini unahitaji pesa kununua wachezaji wenye ubora kama unataka kufika nchi ya ahadi kwa kutumia mpira huu. Pep mwenyewe ametumia pesa kupata wachezaji bora wa kuutumikia mfumo wake. Arteta ametumia pesa nyingi kupata wachezaji bora wa kuutumikia mfumo wake. Kompany aliipandisha Burnley kwa kishindo sana.

Soka safi. Kwa ngazi ya daraja la kwanza ilikuwa kitu sahihi kwake. Alipokwenda Ligi Kuu alihitaji pesa kuweza kurudia alichofanya Championship.

Alihitaji pesa nyingi kupata wachezaji bora wa hadhi ya Ligi Kuu afanye ambacho alifanya Championship. Bahati mbaya Burnley ni maskini. Ndio maana haikushangaza kuona kwamba licha ya timu kuwa na mwelekeo mbaya katika Ligi Kuu bado hakufukuzwa. Ndio maana haikushangaza kwamba hata wakati timu imeshuka daraja msimu huu bado haikumfukuza.

Nadhani walijua kwamba wao ndio walikuwa tatizo na sio kocha. Na mpaka Bayern Munich kumpata Kompany wamelazimika kulipa fidia kuweza kupata saini ya staa huyu wa zamani wa Ubelgiji ambaye kabla ya kutua City alikuwa palepale Ujerumani akicheza katika Klabu ya Hamburg. Kumbe Kompany hakuwa tatizo.

Na sasa Bayern wana pesa. Wana wachezaji wenye hadhi. Watampa Kompany kila kitu ili iwe wazi kwamba tatizo ni yeye au umaskini wa Burnley. Nadhani waliutazama zaidi mpira wa Burnley wakiwa Championship. Na kwa sababu wana pesa, basi wanautaka mpira ule Ujerumani kwa ajili ya kumdhibiti Alonso ambaye kuna kila dalili akawasumbua tena msimu ujao kama kikosi hakitasambaratika. Mpira upo kwa Kompany sasa hivi.

Kama mshambuliaji wako ni Harry Kane kisingizio kitatoka wapi? Kama wachezaji wako ndio hawa kina Serge Gnabry, Leroy Sane, Joshua Kimmich, Tom Muller, Manuel Nauer visingizio vitatoka wapi? Na bado kuna pesa ya kutosha kuleta vipaji vikubwa kutoka katika klabu yoyote ya ndani na nje ya Ulaya, visingizio vitatoka wapi?

Bahati nzuri kwa Kompany ni kwamba jina lake linaweza kuandikika kwa urahisi katika historia ya Bayern Munich kama akiwarudishia taji la Bundesliga tu achilia mbali suala la ubingwa wa Ulaya. Imekuwa rahisi kwa miaka mingi sasa kocha kwenda kufundisha Bayern na kutwaa taji la Bundesliga. Ni kwa sababu Bayern wana pesa na timu nyingine ni dhaifu.

Kutwaa ubingwa Bundesliga halikuwa jambo gumu na makocha walikuwa wanapata wasifu rahisi kutwaa taji hilo. Ukiwa kocha wa Bayern Munich au mchezaji wa timu hiyo moja kwa moja unatwaa taji hilo. Lakini sasa Kompany anatua huku Bayern wakiwa hawana taji hilo mkononi. Zaidi ni kwamba anatua huku Alonso na vijana wake wa Bayer Leverkusen wakiwa wasumbufu waliopitiliza.

En-dapo Kompany atarudisha taji hilo kwa Bavarians, basi atakuwa tofauti kidogo na makocha ambao wamekuwa wakidandia meli na kula chakula kwa urahisi. Swali ni kama itawezekana katika msimu wake wa kwanza. Atayaweza makali ya Alonso? Na kama akishindwa katika msimu wake wa kwanza je wataweza kumvumilia?

Hii miradi inahitaji uvumilivu kidogo. Guardiola katika msimu wake wa kwanza England aliishia kuwania Top Four tu. Akaanza kuwafungasha virago kina Yaya Toure, Pablo Zabaleta, Edin Dzeko na wengineo mpaka alipokipata kitu ambacho alikuwa anakihitaji. Leo kwa msimu wa nne mfululizo anatwaa taji la Ligi Kuu England.

Mikel Arteta katika misimu yake ya kwanza pale Arsenal alionekana kuwa kichekesho. Mpaka alipoondoa mbao mbovu za kina Mesut Ozil, Pierre Emerick Aubameyang na wengineo ndio akatuonyesha uwezo wake alionao.

Hatukumbuki ni lini ilikuwa mara ya mwisho Arsenal kuwania taji la Ligi Kuu England mpaka mwisho. Na ameshindwa kutwaa taji hilo basi tu kwa sababu sikio halizidi kichwa. Arteta anabaki kuwa mwanafunzi wa Guardiola. Kompany atapewa muda Bayern Munich? Tusubiri na kuona.

Hata hivyo ni wazi kwamba amepewa nafasi aliyopo kwa sababu inaonekana anaweza kuupeleka mpira wa Guardiola katika viunga vyao. Kama akifanikiwa, basi kuna wakubwa wa England watauma meno na kujiuliza kwanini hawakumnyakua Kompany pale tu alipoipandisha Burnley kwa kishindo.

Watu wengine waliofanya hivyo ni Chelsea. Wao wamemnyakua mwanafunzi wa Guardiola, Enzo Maresco mapema zaidi. Huyu alikuwa mwanafunzi wa Guardiola akaenda zake Leicester City Championship. Ameipandisha kwa kishindo na papo hapo wamemchukua. Hawakutaka masihara. Naye anakabiliwa na swali hili hili la Kompany kwa sababu yeye pesa anayo.

Chelsea ina pesa na ina wachezaji wa maana. Kwanini msimu unachelewa kuanza? Twende katika usajili. Twende tukatazame Euro. Waache waende ‘pre season’. Baadaye tutakutana msimu ujao. Utakuwa msimu mwingine wa kusisimua katika soka. Tuone kama mazalia ya Guardiola yatafanikiwa katika majukumu mapya ya watu wenye pesa zao. Tusubiri tuone.

Related Posts