Dar es Salaam. Ikiwa ni siku ya tatu kwa taifa la Afrika Kusini kuendelea kuhesabu matokeo ya uchaguzi, chama tawala cha African National Congress (ANC) kimeendelea kutokwa na jasho katika uchaguzi huo kitu ambacho hakijawahi kutokea tangu 1994.
Hili linatajwa kuwa ni anguko kubwa kwa ANC licha ya kuongoza kwa zaidi ya asilimia 40 ya kura za kitaifa ambapo asilimia 97 ya kura zote zimehesabiwa.
Chama cha ANC kinaongozwa na Rais Cyril Ramaphosa kimejinyakulia zaidi ya asilimia 50 za kura katika majimbo saba kati ya tisa.
ANC kinapata wakati upinzani mkali zaidi kutoka Chama kikuu cha cha Democratic Alliance (DA) ambacho kwa sasa kiko katika nafasi ya pili kikiwa na asilimia 21.7 kikifuatiwa na chama cha MK kwa asilimia 14.8 na EFF chenye asilimia 9.37.
ANC katika majimbo saba kati ya tisa ya Afrika Kusini kimevuka zaidi ya asilimia 50 katika hesabu za kura katika majimbo matano kati ya hayo: Limpopo (asilimia 74), Rasi ya Mashariki (asilimia 64), Kaskazini Magharibi (asilimia 59), Free State (asilimia 53) na Mpumalanga (asilimia 52).
Chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) ambacho kinaongozwa na John Steenhuisen kiko mbioni kuendelea kuitawala Cape Magharibi (asilimia 53), ambacho kimefanya hivyo tangu 2009.
Kwa upande wa KwaZulu-Natal (KZN), chama cha MK cha Rais wa zamani, Jacob Zuma kina idadi kubwa zaidi ya kura kwa asilimia 46 mbele ya ANC chenye takribani asilimia 18 pekee.