Jaji Tiganga ataka ushiriki wa sekta binafsi udhibiti taka ngumu

Arusha. Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Joachimu Tiganga ameitaka Serikali kuishirikisha sekta binafsi na kuweka mazingira wezeshi ya kusaidia katika udhibiti wa taka ngumu zinazozagaa mitaani.

Jaji Tiganga amesema kuwa zaidi ya tani milioni saba za taka ngumu zinazozalishwa nchini, ni asilimia 35 pekee ndizo zinazokusanywa na kuteketezwa, huku zingine zikibaki mitaani zikizagaa na kuleta madhara kama magonjwa na athari za kimazinira.

Jaji Tiganga ameyasema hayo leo Juni 1, 2024 katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani mwaka 2024 uliofanyika jijini Arusha.

Amesema, kushirikisha sekta binafsi kudhibiti taka ngumu zinazozalishwa, kutasaidia kupunguza taka ngumu zinazobaki mitaani na kuleta madhara kwa wananchi.

“Ifike mahali mamlaka za serikali za mitaa zishirikishe sekta binafsi kwa vitendo na ziwawekee mazingira wezeshi,  maana wao watasaidia kukusanya kwa kiwango kikubwa zaidi kwa matumizi mbalimbali ikiwemo hata kuzirejelesha kuwa bidhaa tena ya kutumika na kuzalisha fursa nyingine za ajira,” amesema Jaji Tiganga.

Mbali na hilo amezitaka mamlaka za udhibiti wa taka na usafi wa mazingira kuhakikisha zinasimamia utekelezaji wa mkakati wa nishati safi na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa,  ili kusaidia nchi kuondokana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi kutokana na ukataji miti.

“Tunaona siku hizi majanga makubwa yanatokea kama mafuriko ya maji na matope, lakini pia ukame uliopitiliza na kuua mifugo na kuhatarisha hata ustawi wetu wenyewe. Tusipochukua hatua za makusudi mapema hata sisi tuko hatarini,” amesema Jaji Tiganga.

Mbali na hilo amezitaka halmashauri nchini kujiwekea mpango endelevu wa uhifadhi, utunzaji na usafi wa mazingira,  ikiwemo kufanya usafi kila mara na kuhakikisha wanajiwekea malego ya kupanda angalau miti milioni 1.5 kila mwaka.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathimini kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Sigsbert Kavishe amesema kuwa kwa sasa wanatekeleza mpango wa kuhakikisha taka zinazofaa kurejeleshwa zifanywe hivyo ili kuzalisha fursa lakini pia kupunguza wimbi la taka zinazobaki mitaani kama chupa za plastiki na vifaa vya kielektroniki.

“Tumeanza kushirikisha sekta binafsi katika kukabiliana na taka ngumu na mwaka huu tumeandaa maonyesho ya ubunifu wa uhifadhi na usimamizi wa mazingira ambayo kila taasisi itaonyesha ubunifu wa kiteknlojia katika kurejelesha hizi taka kuwa bidhaa,” amesema.

Kwa upande wake,  Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Felician Mtahengerwa amesema kuwa usafi wa mazingira unakwenda sambamba na upangaji wa mji, huku akikemea baadhi ya wafanyabiashara kupanga bidhaa za chakula chini.

“Kila kitu kikikaa eneo ambalo sio lake ni uchafu, hivyo nitumie fursa hii kuwaambia wafanyabiashara wa Jiji la Arusha kuzingatia kwanza usafi wa maeneo yao ya biashara lakini pia wasipange bidhaa chini hasa za vyakula kwani inafifisha mvuto wa mji huu wa kitalii,” amesema.

Naye mfanyabiashara wa soko kuu, Lucy Lukumai ameiomba Serikali kuhakikisha inaweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa taka ndani ya masoko ili kuwanusuru na magonjwa ya milipuko hasa msimu wa mvua.

Related Posts