Jamii yahimizwa kulinda, kuheshimu haki za watoto

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wakati dunia ikisherehekea Siku ya Kimataifa ya Watoto, wito umetolewa kwa jamii kuheshimu haki za watoto na kuhakikisha wanalindwa wakati wote.

Siku ya Kimataifa ya Watoto huadhimishwa Juni Mosi kila mwaka kwa lengo la kutambua umuhimu wa watoto katika jamii na kuangazia haki na ustawi wao.

Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya CCCC Tawi la Tanzania, Yue Guozhu, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto, Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa maadhimisho yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Bajeviro Dar es Salaam, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Tausi Makemba, amesema kumekuwa na matukio mengi ya uvunjifu wa haki za watoto na kusababisha wengine kuzikimbia familia zao.

Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Kampuni ya Ujenzi inayomilikiwa na Serikali ya China (CCCC) Tawi la Tanzania ambayo pia ilikabidhi misaada mbalimbali ya kujifunzia kwa wanafunzi wa shule hiyo.

“Tunapoadhimisha siku hii ni muhimu kutambua kwamba mtoto anazo haki zake kwa sababu kuna unyanyasaji mwingi unaofanyika kupitia kukiukwa au kuvunjwa kwa sheria na haki za watoto. Kipindi cha sasa tulichonacho tunatakiwa tusiwafiche kitu watoto, tunatakiwa tuongee nao na kuwaelekeza kwa upendo.

“Kupitia shuleni tunawaelekeza watoto namna ya kuishi na kupitia masomo ya uraia na maadili watoto wanaelewa hatua inayowasaidia kuepuka vishawishi vya mtaani kama vile matumizi ya dawa za kulevya na makundi rika ambayo hayastahili,” amesema Mwalimu Makemba.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Baech A, Steven Kinyota, amesema ni muhimu jamii kutambua na kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi.

Naibu Mkurugenzi wa Kampnuni ya CCCC Tawi la Tanzania, Yue Guozhu, amesema wanatambua umuhimu wa kundi hilo muhimu ndiyo maana walichagua shule hiyo kusherehekea na watoto.

Kampuni hiyo imekabidhi misaada mbalimbali ya vifaa vya kujifunzia yakiwemo madaftari, kalamu na mabegi ya madaftari ili kuwawezesha wanafunzi wa shule hiyo kusoma katika mazingira mazuri.

Related Posts