Johannesburg. Ni wazi kwamba Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kimeporomoka kimvuto na ushawishi kwa wapigaa kura.
Kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ilipopata uhuru miaka 30 iliyopita ANC imepata asilimia 40 ya kura, hivyo kitalazimika kuungana na chama kingine kuunda serikali.
Kutokana na anguko hilo, sasa viongozi wa ANC wanajipanga kuwa na mazungumzo kutafakari chama cha kuungana nacho.
Hadi wakati asilimia 99 ya matokeo ikiwa imeshatangazwa, ANC ilikuwa imepata asilimia 40 ya kura, kikifuatiwa na Democratic Alliance (DA) chenye asilimia 22, huku chama kipya cha Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma uMkhonto we Sizwe (MK) kikiwa na asilimia 15 na Economic Freedom Fighter (EFF) kikiwa na asilimia tisa.
Kwa matokeo hayo, ANC haiwezi kuunda Serikali kwa kuwa haijafikisha asilimia 50 ya kura kwa mujibu wa Katiba ya Afrika Kusini.
MK imepata ushindi kwenye jimbo muhimu la KwaZulu Natal anakotoka Zuma na ambako ANC haijawahi kulipoteza tangu uchaguzi wa kwanza baada ya ubaguzi wa rangi mwaka 1994.
Mbali na KwaZulu-Natal, MK pia imeungwa mkono katika maeneo ya vijijini na mijini, pamoja na maeneo katika majimbo ya Gauteng na Mpumalanga.
Mbali na KwaZulu Natal na Western Cape, ambako DA inaonekana kurejea madarakani kwa wingi wa kura, ANC pia imepata pigo katika jimbo la Gauteng, ambako imepitwa kwa mbali.
Zuma, mwanaharakati mkongwe wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi aliyeondolewa madarakani mwaka 2018 kutokana na madai ya ufisadi, ni mtu maarufu kati ya Waafrika Kusini wengi na ametegemea sera za ujamaa kuvutia kura.
Wakati wa kampeni za uchaguzi, alihusisha matatizo ya Afrika Kusini kama mtaji wa ukiritimba wa Wazungu.
Kutokana na anguko hilo, ANC sasa itahitaji kwa mara ya kwanza katika miaka 30, kuomba msaada kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani ili kuunga mkono Serikali ya Muungano ya Kitaifa ikiwa inataka kubaki madarakani chini ya Rais Cyril Ramaphosa.
Pia itahitaji kufanya hivyo ili kubaki madarakani katika majimbo kama Gauteng.
Akiizungumzia hali hiyo, mchambuzi Sizwe Mpofu-Walsh aliyezungumza na Aljazeera, alisema ni ‘kifo cha utawala wa ANC.’
“Nadhani ni vizuri. Kuna matumaini kama vile inavyopaswa kuwa na hofu. Watu wana wasiwasi na kutokuwa na uhakika wa nini kitatokea, itafungua njia mpya za mabadiliko na njia mpya za uwajibikaji,” amesema.
Mpofu-Walsh amesema kupoteza uchaguzi kwa ANC, ni mchanganyiko wa kiburi na kukataa kushindwa kwao.
Mchambuzi huru wa siasa Sandile Swana amesema ANC imejiunga na harakati nyingine za ukombozi ambazo zilipata adhabu kwa kushindwa kutimiza ahadi zao za ukombozi.
“Swapo nchini Namibia, Zanu PF nchini Zimbabwe na ANC nchini Afrika Kusini wako kwenye boti moja,” amesema, akimaanisha vyama vilivyoongoza harakati za uhuru nchini Namibia na Zimbabwe.
Imraan Buccus, msomi na mtafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Kijamii na Kiuchumi ya Auwal, amesema matokeo ya uchaguzi yanaashiria kuporomoka kwa ANC.
“Ni sawa na kile kilichotokea kwa harakati za ukombozi kote barani Afrika. Kuna mifano nchini Zambia na Kenya,” amesema.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB), asilimia 55 ya wakazi wa Afrika Kusini wanaishi katika umasikini.
Miaka 30 ya ANC madarakani imekuwa na sifa ya kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na kwa sasa ni asilimia 33.
Ufisadi wa kimfumo na uzembe wa serikali, unaosababisha hali mbaya zaidi ya maisha, ni miongoni mwa masuala yanayowakabili Waafrika Kusini.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni Mosi, 2024, wakili Dk Onesmo Kyauke amesema sababu kubwa ya anguko la ANC ni kugombana na Zuma.
“ANC waliingia mgogoro na Zuma anayetoka Kwazulu Natal ambako awali ilikuwa ngome ya chama cha Inkhata Freedom Party. Alipokuwa Rais, Zuma aliihamishia nguvu hiyo ANC na sasa ameihamishia MK,” amesema.
Mbali na ANC, Dk Kyauke anasema MK pia imechota kura za EFF katika jimbo hilo.
Dk Kyauke pia ametaja kero za wananchi akisema zimechangia kupoteza ushindi wa ANC.
“Matatizo ya rushwa na ufisadi, kuharibika kwa miundombinu hasa ya reli, kuna mgawo wa umeme na maji, yote hayo yamewachosha wananchi wa Afrika Kusini,” amesema.
“Awali wananchi wa mijini walikuwa hawapigi kura, lakini sasa wameamka wamepiga kura,” amesema.
Kwa mujibu wa Katiba ya Afrika Kusini, Rais lazima achaguliwe ndani ya siku 14 baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa na Tume ya Uchaguzi.
Hata hivyo, swali linabaki, chama kipi kitaunda Serikali?
Dk Kyauke amesema ANC iko njia panda kwani bado hakijajua kiungane na chama gani kuunda Serikali.
“Katika majimbo tisa yaliyopo, ANC imeshinda majimbo matano kwa wingi, majimbo mengine italazimika kuungwa mkono,” amesema.
“Kitaifa ANC inaweza kuomba kuungana na MK, lakini masharti ya Zuma ni magumu na si rahisi kufanya kazi na Rais Ramaphosa,” amesema.
Njia nyingine ambayo pia ni ngumu ni ANC kuomba kuungana na DA yenye Wazungu wengi au kuomba kuungwa mkono na vyama vidogo kama vitaongeza kura.
“Vyama vya DA, MK na EFF vikiungana na vyama vidogo pia vinaweza kuunda Serikali na kuifanya ANC kuwa chama cha upinzani,” anasema.
Hata hivyo, amesema sera za vyama hivyo hazishabihiani na huenda vikashindwana kabla havijaungana.
Akizungumza na vyombo vya habari jana, Mwenyekiti wa ANC, Gwede Mantashe, amesema chama hicho hakikupanga matokeo hayo, akisema, “Muungano ni matokeo, hupangi matokeo.”
Mantashe amehusisha uungwaji mkono wa Zuma na utaifa wa kikabila, akisema Zuma alihimiza uungwaji mkono kutoka kwa watu wa kabila la Wazulu katika jimbo hilo, ambalo yeye pia ni sehemu ya kabila hilo.
Katika matokeo hayo, chama cha DA kimeonekana kuimarika kidogo.
Chama hicho kilipata asilimia 21 ya kura na viti katika uchaguzi wa 2019.
Kiongozi wake, John Steenhuisen, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kwamba alikuwa na furaha na ukuaji wa chama chake.
“Ukuaji ni ukuaji,” amesema alipoulizwa kuhusu ongezeko dogo la uungwaji mkono wa chama chake.
Imeandikwa na Elias Msuya na mashirika ya habari.