Luhemeja akumbusha fursa biashara hewa ukaa

Geita. Watanzania wametakiwa kuacha kuendelea kuona mabadiliko ya tabia nchi kama changamoto badala yake waitumie kama fursa ya kiuchumi kwa kupanda miti na kuitunza ili kufanya  biashara ya hewa ukaa inayohimizwa na jumuiya ya kimataifa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais anaeshughulikia Muungano na Mazingira, Cyprian Luhemeja ameyasema hayo wakati wa shughuli ya upandaji miti na usafi wa mazingira iliyofanyika katika Hospitali ya Kanda Chato ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya mazingira iliyoadhimishwa kikanda katika eneo hilo.

Luhemeja amesema jamii imekuwa ikipanda miti kwa muda mrefu lakini haitafsiri miti hiyo kama fursa ya kiuchumi na kusema kwa sasa miti ni biashara iliyogeuka inayoweza kuwaingizia mapato na kuwakwamua kiuchumi.

“Tumekuwa tukipanda miti muda mrefu kupambana na mazingira lakini hatuitafsiri kama fursa ya kupata fedha.Kwa sasa miti ni biashara iliyogeuka tunahamasisha biashara ya Carbon (hewa ukaaa)mti mmoja unaoupanda unazalisha Oksijeni lakini unakula Carbon mchakato huo ndio unaitwa biashara ya Carbon (hewa ukaa)”amesema Luhemeja

Amesema kupitia biashara hiyo Halmashauri ya Tanganyika imeanza kuvuna faida ambapo Juni 5,2024 ambayo ni kilele cha siku ya mazingira duniani itakabidhiwa Sh14 bilioni zinazotokana na biashara ya hewa ukaa.

Akizungumzia usafi wa mazingira Luhemeja  amesema Ofisi ya Makamu wa Rais iko mbioni kuanzisha  mchakato wa kutoa zawadi kwa halmashauri na mkoa utakao kuwa umefanya vizuri kwenye kutunza na kuhifadhi mazingira .

“Mkoa wa Geita na Mwanza umeanza kuliwa na jangwa na endapo haitachukua hatua za makusudi za kukabiliaana na hali hiyo hali itakuwa mbaya zaidi kwa miaka ijayo,” amesema Luhemeja.

Akiongoza  usafi na upandaji miti kwa niaba ya Waziri Mkuu aliyetegemewa kuwa mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ametaka shughuli za upandaji miti na usafi wa mazingira kuwa endelevu .

Shigella amesema ni vema wananchi wakachangamkia fursa ya biashara ya hewa ukaa badala ya kufanya biashara ya kuchoma mkaa na kuchana mbao, huku akizitaka halmashauri kutekeleza agizo la Serikali la kupanda miti 1.5milioni kila mwaka.

“Tupange ratiba vizuri tuhakikishe miti inapandwa kuanzia kwenye makazi ya watu, msikitini kwenye masoko, shuleni ili kuhakikisha agizo la kupanda miti 1.5 milioni linafikiwa.

Shigella amesema mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa yenye uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na shughuli za uchimbaji madini ambazo mbali na kuathiri miti inaathiri pia udongo na kuwataka wachimbaji wanapohitimisha shughuli zao, kukumbuka kurejesha uoto wa asili.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo wamesema ili kuacha shughuli za ukataji miti Serikali haina budi kuja na mbinu mbadala ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kutotumia ‘matimba’ kwa kuwa wanachangia uharibifu wa mazingira kwenye mkoa huo.

Mashauri Mashamba Mkazi wa Chato amesema hali ngumu ya maisha ndio inachangia watu kukata miti na kuharibu mazingira na kuiomba Serikali kupunguza bei za gesi ili wananchi wa kipato cha chini waweze kumudu na kuachana na mkaa.

Related Posts