Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu ameanza ziara ya wiki tatu Mkoa wa Singida ambako atafanya mikutano ya hadhara katika kata zote kwenye kila wilaya.
Lissu ambaye ameongozana na viongozi kadhaa wa chama hicho, akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema (Bazecha), Hashim Juma wameanza na Jimbo la Iramba Magharibi linaloongozwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Shelui leo Jumamosi Juni Mosi, 2024 Lissu amewataka wananchi kujipanga kwa ajili ya uchaguzi vijiji, vitongoji na mitaa utakaofanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani 2025.
Amesema baada ya kumaliza uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu, kazi inayofuata ni kujipanga na uchaguzi wa madiwani, wabunge na rais.
Amewasisitiza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili waweze kutengeneza mikakati.
“Tunaenda kwenye uchaguzi hakikisheni mnasimamisha wagombea wote wanaostahili, tunaanza kuchochea kuni huku chini ili moto uwake, kisha tujipange kwa kazi kubwa iliyopo mbele,” amesema Lissu.
Amewataka wananchi watakapokwenda kwenye uchaguzi wasichague kwa kuwa walipewa fedha kwani wataenda kuangamia.
“Utakavyochagua ndivyo utakavyopata, ukichagua vibaya utapata mabaya, vizuri utapata vizuri tunapaswa kujipanga na kuwa makini kwenye kazi,” amesema.
Lissu ambaye amewahi kuwa mbunge wa Singida Mashariki, amesema alipokuwa katika nafasi hiyo kwenye jimbo lake lake mwaka 2014 kati ya vijiji 50 Chadema kilishinda vijiji 47.
“Tunaanza na vijiji na vitongoji, pia tunapokuja kuchagua diwani na mbunge unakuwa umemaliza mambo yote, hakutakuwa na ushuru wala tozo za ajabu ajabu kwa kuwa wakuwasemea wapo,” amesema.
Akizungumzia hali ya umasikini mkoani Singida, amesema watu masikini ndio wanaotumiwa kwa gharama kubwa kuwaweka madarakni wale wanaowatia umasikini.
Amesema mikoa ya Dodoma na Singida ni kati ya mikoa inayokandamizwa kwenye ushuru hasa wa mazao na mifugo, akisema kumekuwa na tozo na ushuru wa kila aina.
“Kwenye mpunga na alizeti kumekuwa na tozo na ushuru lakini mkiulizwa ni lini mmesomewa mapato na matumizi hamjui…hakuna anayefahamu,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Bazecha, Juma amewataka wananchi kuungana na kuwa kitu kimoja ili waweze kushinda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na uchaguzi mkuu mwakani.
“Kama ninyi ni wanyonge na mko wengi mkishikamana pamoja Mungu ataleta baraka zake, tunaenda kusimamisha wagombea tutafanya kampeni na yule mgombea wetu atakayeshinda tutahakikisha anatangazwa,” amesema.