Wataka wajumbe kuondolewa uchaguzi wa madiwani, wabunge CCM

Babati. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimechukua na kinakwenda kufanyia kazi mapendekezo ya wanachama wake mkoani Manyara wanaotaka wagombea udiwani na ubunge kuchaguliwa na wanachama na si wajumbe.

Ushauri huo wameutoa leo Jumamosi, Juni 1, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya zamani ya Babati Mjini, uliohutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi.

Dk Nchimbi yuko ziarani kufuatilka utekelezaji wa Ilani, maandalizi ya chaguzi zijazo na kusikiliza kero za wananchi.

Wanachama hao wamesema hatua hiyo itasaidia kupata wagombea wasiotumia fedha na watakaokuwa na sifa za kuchagulika.

CCM imekuwa na utaratibu tofauti wa kuwapata wagombea ndani ya chama hicho wa udiwani na ubunge na katika uchaguzi wa 2020 walitumia wajumbe. Utaratibu huo ulilalamikiwa na baadhi ya wagombea kuwa uligubikwa na vitendo vya rushwa.

Baada ya Dk Nchimbi kupanda jukwaani na kuomba wananchi wenye kero kujitokeza, Andrew Omary amesema zamani kura za maoni za wabunge na madiwani zilikuwa zinapigwa na wanachama, baadaye zikawa zinapigwa na wajumbe.

Omary ameshauri utaratibu wa wanachama kuwapigia kura madiwani urejeshwe na kwa ubunge unaweza kuendelea na wajumbe.

“Kura za wanachama zikirudi kwanza zitasaidia hata wanachama kulipa ada za uanachama na wanachama wanakuwa na nguvu tofauti na utaratibu wa sasa wanapigiwa kura na wajumbe, ambao wengine wananunuliwa,” amesema.

Katika majibu, Dk Nchimbi amesema: “Tumeupokea ushauri wake, tumeuchukua na tutaufikisha katika vikao vya chama.”

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya zamani ya Babati Mjini leo Juni Mosi, 2024.

Baada ya maelezo hayo, wananchi waliokuwapo  mkutanoni walishangilia, kisha Dk Nchimb  akasema: “Wananchi wa Babati mmetulia na kushauri namna bora ya kupata viongozi.” Wakajibu ‘ndiyoo.’

Kwa majibu ya wananchi, Dk Nchimbi amesema: “Hata mimi sipendi wagombea ambao hawachaguliki, wanaopatikana kwa rushwa.”

Diwani wa Namelock (CCM), Masiyo Kibiki akizungumza na Mwananchi Digital amesema: “Ushauri huo na mimi naafiki, kutumia wajumbe kuna watu wana sifa za kugombea lakini hawana fedha. Ukitumia mfumo wa wajumbe ni rahisi wajumbe kuhongeka, na hatuwezi kupata kiongozi bora bali bora kiongozi.”

Kibiki amesema: “Lakini wakitumika wanachama wote, hawezi kuwahonga wanachama wote na pale ndipo tutapata viongozi bora. Hili utaona hata mwaka 2020 hali ilivyokuwa, wagombea waliwalalamikia wajumbe, kwa hiyo mimi naunga mkono na chama ikifanyie kazi.”

Awali, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema kwa waliyoyaona mkoani humo,  wamejiridhisha katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wataibuka washindi.

Makalla amesema kinachowafanya watembee kifua mbele ni utekelezaji wa miradi mbalimbali.

“Na kazi yetu ni kuwaletea wagombea wazuri wanaokubalika ili tushinde kwa kishindo na mwakani tuibuke washinde tena,” amesema.

Amesema wanatambua kuna changamoto ndogondogo zilizopo na wamezichukua ikiwemo zilizotolewa katika kikao cha ndani.

“Katibu mkuu amezichukua na anazipeleka serikalini kuzitafutia ufumbuzi,” amesema.

Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah amewaomba wananchi wa mkoa huo kutokatishwa tamaa na maneno ya uchochezi yanayotolewa na baadhi ya watu wasiowatakia mema.

“Kama mambo makubwa mama yetu ameyafanya, madogomadogo hawezi kuacha kuyafanya. Wapo waliokuwa hawaamini kama angeweza kuwa kiongozi mkuu wa nchi na ameweza kwa viwango vikubwa,” amesema Rabia.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara (RC), Queen Sendiga,  amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul amesema utekelezaji wa Ilani ya chama hicho katika jimbo hilo ni zaidi ya asilimia 98. Miongoni mwa miradi ni shule kubwa ya kidato cha tano na sita ya masomo ya sayansi ambayo imekamilika na itaanza kupokea wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Gekul aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria amesema, sekta ya afya kila eneo kazi zinafanyika, miradi ya maji, barabara na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) wanajenga kituo cha kufundisha michezo.

Related Posts