Matatizo ya mzazi yanavyoweza kumuathiri mtoto

“Licha ya kwamba familia yetu haina uwezo, nilikuwa na amani kuishi na mama yangu, sikujali magumu tuliyopitia, lakini siku alipoamua kutoweka ghafla baada ya kuzidiwa na madeni maisha yangu yalianza kuharibika.”

Hayo ni maneno ya Amina Salum, mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Mashujaa, akiwa miongoni mwa wanafunzi walioondolewa kwenye hatari ya kupata matatizo ya afya ya akili.
Binti huyu alipatwa msongo mkali wa mawazo kutokana na kutoweka ghafla kwa mama yake katika kipindi alichomhitaji zaidi kama nguzo na tegemeo lake.

Amina anasimulia katika kipindi chote alichokuwa anaishi na mzazi wake alikuwa akishuhudia magumu anayopitia kuhakikisha yeye na mdogo wake wanapata mahitaji muhimu.

“Kuwa pamoja kama familia ilikuwa inatupa faraja, mimi na mdogo wangu hatukujali magumu tuliyokuwa tunapitia, ingawa tulikuwa tunamuona mama alivyokuwa akihangaika huku na kule kuhakikisha maisha yanaenda.

Mama alikuwa akifanya biashara ya mbogamboga sokoni, ili kufanya mambo yaende alikuwa pia anakopa hii mikopo ya ‘kausha damu’ na ndiyo ilimfanya atoweke kwa sababu ilifika kipindi alizidiwa na madeni,” anasema Amina.

Anasema alikuwa akishuhudiwa mara kwa mara mama yake akija kudaiwa na kuchukuliwa vitu, lakini hakuwa na la kufanya zaidi ya kumuomba Mungu amsaidie katika safari yake ya elimu ili siku moja aikomboe familia yake kutoka kwenye lindi la umasikini.

Wakati anaendelea kufikiria hivyo, simanzi ikaongezeka maradufu baada ya mama yake kutoweka ikiwa ni siku chache kabla ya kujiunga na kidato cha tano, akapigwa na bumbuazi asijue wapi ataanzia.

“Mama aliondoka nikiwa nasubiri kuanza form five, aliniacha nikiwa sijui nitapata vipi mahitaji ya shule, kitendo hicho kiliniumiza kupita kiasi, nikajikuta nina msongo wa mawazo kiasi kwamba nikaanza kupoteza matumaini ya kuishi.

“Hali hiyo iliendelea hata baada ya kufanikiwa kupata mahitaji na kujiunga na shule, niliendelea kuwa na mawazo, nikawa najitenga na hata kitaaluma nikaanza kuyumba, nikapoteza shauku ya kusoma,” anasema.

Akiwa katika hali hiyo, klabu ya afya ya akili ikaanzishwa shuleni hapo, akashawishika kujiunga, ndipo ukawa mwanzo mpya wa maisha yake, kwani aliweza kutambua kuwa ana changamoto ya afya ya akili na akasaidiwa kupata ufumbuzi.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 700,000 hupoteza maisha kwa mwaka kutokana na kujiua, hiyo ikiwa sababu ya nne ya vifo vinavyotokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 29.

Afya ya akili inatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa hali hii ya kuwasukuma watoto na vijana kukatisha uhai wao au hata kuangukia kwenye matumizi ya dawa za kulevya, ngono zembe na vitendo vya uhalifu.

Kutokana na alichopitia binti huyu, huenda na watoto wengine, ipo haja ya kuwepo mkakati utakaowezesha elimu ya afya ya akili kujumuishwa kwenye mitalaa ya elimu sambamba na huduma za unasihi kutolewa shuleni.

Hatua hii itawezesha kuwasaidia watoto na vijana rika balehe kujua njia sahihi za kukabiliana na changamoto zao, hasa zinazowaathiri kisaikolojia.

Msaikolojia tiba, Isack Lema anasema mlipuko wa magonjwa ya akili unaanzia miaka 14, hivyo ni muhimu kwa hatua madhubuti kuchukuliwa kwa rika hilo ili kuwaepusha kuangukia kwenye wimbi la changamoto ya afya ya akili.

Anasema ni rahisi kwa mtoto kupata matatizo ya kisaikolojia kutokana na changamoto anazoziona kwa mzazi au wazazi wake.

“Wewe mzazi unaweza kufikiri kwamba unayopitia hayamhusu mtoto, ukweli ni kwamba kisaikolojia anaathirika kwa kiasi kikubwa na inawezekana akaangukia kwenye changamoto ya afya ya akili kama hatapata matibabu mapema,” anasema.

Nini kinasababisha hali hii

Lema anasemea yapo mazingira tofauti yanaweza kumsababishia mtoto kuwa na tatizo la afya ya akili na yanaweza kuchangiwa pia na mzazi, akitoa mfano ukali kupitiliza unaweza kumsababishia mtoto kupata ugonjwa wa wasiwasi uliopitiliza.

Mtaalamu huyo anaeleza wasiwasi ni ugonjwa unaowapata watoto wengi, hali hii inatengenezwa na watu wa karibu wa mtoto husika, mfano mzazi anapokuwa mkali na kumfokea mara kwa mara inamfanya mtoto kuwa na hofu na wasiwasi wa kufokewa au kuadhibiwa.

Mbali na wasiwasi, yapo magonjwa mengine ya akili ambayo yanawasonga zaidi watoto na inahitaji uangalizi wa karibu kubaini na kutamfutia tiba mapema, akitoa mfano utundu kupitiliza ni miongoni mwa magonjwa hayo.

Anasema programu ya afya ya akili ikiwepo shuleni itasaidia kuwapatia wanafunzi njia za kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo kwenye mazingira yanayowazunguka na kufanya maamuzi sahihi yatakayowaweka mbali na tabia hatarishi.

“Watoto siku hizi wanakutana na changamoto za maisha mapema zaidi na tunavyosikia kuna watoto wamejiua ni matokeo ya hayo wanayopitia. Siku hizi siyo ajabu mtoto kushuhudia mwizi anauawa mbele yake, kisaikolojia hii ni hatari kwa afya ya akili.”

Msaikolojia huyo anasema watoto na vijana wa rika balehe wanakabiliwa na changamoto lukuki ambazo zinaweza kuwafanya waangukie kwenye changamoto ya afya ya akili.

“Programu hii imesaidia kuwabaini wanafunzi wenye changamoto na wakapewa afua ambazo zimeweza kuwaepusha dhidi ya matatizo ya afya ya akili. Walimu wamefundishwa kutofautisha tabia za kawaida za watoto na changamoto.

“Hapo awali ilikuwa vigumu kumbaini mwanafunzi mwenye changamoto, ilikuwa inawekwa kundi moja kwamba ni utukutu au ujeuri, hivyo waliishia kupigwa na kupewa adhabu zilizoongeza tatizo, lakini sasa wamebadilika,” anasema Lema.

Hilo limethibitishwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Mashujaa, Joyce Kivelege anayeeleza kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya kitabia kwa wanafunzi, hali inayochangia kupanda kwa kiwango cha taaluma.

“Tumeona mabadiliko makubwa katika kipindi hiki cha mwaka mmoja tangu mradi huu uanze kutekelezwa hapa shuleni, watoto wamekuwa huru kuzungumza wanayopitia na tunashirikiana kutatua changamoto zao wanaendelea vyema na masomo.

“Awali ilikuwa ni vigumu kuelewa mtoto ana tatizo na huenda limeanzia nyumbani, kwa haraka ukiona mtoto haeleweki inatafsiriwa kama mjeuri na adhabu zinamfuata, kumbe badala ya kumsaidia unamuongezea tatizo,” anasema Joyce.

Mkurugenzi wa asasi ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY), Rustika Tembele ambao ndio watekelezaji wa programu hiyo anasema imelenga kusaidia walimu na wanafunzi kufundishwa mbinu za kukabiliana na changamoto za afya ya akili.

Anasema shule ni sehemu muhimu kwa elimu ya afya ya akili kupelekwa ili kuwanusuru watoto na vijana wa rika balehe wasitumbukie kwenye janga hilo ambalo limeshagharimu maisha ya wengi.

“Hali ni mbaya, tunashuhudia kila siku matukio ya watoto na vijana wadogo kukatisha uhai wao, ndiyo maana tumeona tuanze na shule, elimu ya afya ya akili itolewe huku chini kabisa, tumeanza na Mashujaa sekondari, katika kipindi cha mwaka mmoja tumeona matokeo chanya, kuna mabadiliko makubwa kwa watoto hawa” anasema.

Related Posts