Njombe. “Baada ya kuona amekufa, mimi nilichukua panga na kuanza kumkata kuanzia kiunoni nikamtenganisha mara mbili,” hayo ni maelezo ya Katekista Daniel Mwalango wa kigango cha Makambako cha Kanisa Katoliki, akisimulia alivyomuua Nickson Myamba.
Ni simulizi ambayo itakuacha mdomo wazi hasa ikizingatiwa kuwa Katekista huyo ni kiongozi wa kiroho anayehubiri waumini kutotenda dhambi na kuwa na hofu ya Mungu, ikiwamo kuziheshimu amri 10 za Mungu, ikiwamo amri ya sita inayoharamisha kuua.
Ukisoma maelezo ya ungamo ya Mwalango namna alivyotafuta vifaa vya kutekeleza mauaji na kuvihifadhi katika duka la vitabu lililopo ndani ya uzio wa kanisa, kisha kutekeleza mauaji na kudeki chumba ili kupoteza ushahidi, yatakutoa machozi.
Mauaji hayo ya kikatili, yalifanyika katika duka la kuuza vitabu lililopo ndani ya Parokia ya Makambako ya Kanisa Katoliki mkoani Njombe usiku wa Februari 7, 2021. Mauaji hayo yalitikisa mji wa Njombe na Tanzania kwa ujumla hasa waumini wa dini ya Kikristo.
Katika makala ya simulizi ya mauaji haya, tutawaletea mwanzo mwisho namna Mwalango alivyopanga kwa ustadi mauaji hayo, silaha aliyoitumia, sababu ya kufanya hivyo na namna alivyoweka mabaki ya mwili huo kwenye mifuko ya sandarusi.
Makala haya yataegemea hukumu iliyotolewa Desemba 12, 2023 na Jaji Said Kalunde wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa, baada ya kusikiliza ushahidi wa pande mbili.
Jaji Kalunde anasema ukweli wa kesi hiyo kama ulivyofichuliwa na upande wa mashitaka, ulishtua dhamiri ya mahakama na anaonyesha mfano halisi wa jinsi uchoyo na hasira vinavyoweza kuharibu maisha hata katika taasisi inayoaminika na jamii ya mwanadamu.
“Katekista ambaye alipaswa kuwa mwalimu wa mafundisho matakatifu aligeuka kuwa jini. Ukweli wa tukio hili unawakilisha kisa kisicho na maana cha kusaliti tumaini la baba na la kiMungu la kutaniko lililomtumaini kufundisha watoto,” alieleza Jaji Kalunde.
Nini kilimuudhi hadi kuua
Mwaka 2017, Parokia ya Makambako, kigango cha Makambako ilianzisha mradi wa duka la kuuza vitabu kwa lengo la kuuza vitabu vya dini ambapo Daniel Mwalango maarufu kwa jina la ‘Dani’ akawa ni mmoja wa waanzilishi na mtunza stoo wa kwanza.
Mradi huo ulisimamiwa na uongozi wa Kanisa kigango cha Makambako ambao ni Mwenyekiti Michael Kihaga na Nickson Myamba aliyekuwa Katibu huku Padri Paschal Makoha akiwa mlezi wa mradi na Dani aliuendesha hadi mwanzoni mwa 2022.
Januari mwaka 2022, kigango kiliitisha mkutano kujadili uendeshaji wa duka hilo na kuazimia kuwa Dani akabidhi uendeshaji wa mradi huo kwa Nickson Myamba, kwa sababu Dani alikuwa hafungui duka wakati wote na hivyo kusababisha mapato kushuka.
Dani au Mwilango akaamriwa kuandaa hesabu ili kurahisisha makabidhiano na uamuzi huo wa kanisa haukumfurahisha, lakini hiyo haikumzuia Nickson Myamba kuendelea kumshinikiza Dani kukamilisha uandaaji wa hesabu na kukabidhi duka kwake.
Katekista alivyotekeleza mauaji
Katika kuandaa mipango ya mauaji, Dani akatafuta kipande cha bomba la chuma na kulihifadhi ndani ya duka na akaenda nyumbani kuchukua panga na kulinoa ili liwe na makali, nalo akalihifadhi ndani ya duka hilo lililopo ndani ya uzio wa kanisa.
Ili kuhakikisha mpango huo wa mauaji unakwenda vizuri, alitafuta mifuko mitatu ya sandarusi na kuihifadhi ndani ya duka, akatafuta mifuko ya nailoni lakini kulingana na ushahidi wa upande wa mashitaka, haikujulikana maandalizi haya yalichukua muda gani.
Tarehe ya makabidhiano ilipangwa kuwa Januari 7, 2022 siku ya Jumatatu na ilipofika saa 10:00 alasiri, Myamba akampigia simu Dani kupitia simu yake ya mkononi na kumjulisha kuwa wakutane katika duka la vitabu ili kukamilisha makabidhiano.
Makabidhiano yalianza saa 10:15 alasiri kwa kupitia akaunti za duka na wakati Myamba alipokuwa bize kupitia taarifa za mauzo akiwa amegeukia upande tofauti, Dani akatumia nafasi hiyo kutekeleza mpango wake wa mauaji.
Alichukua bomba lile la chuma na kumpiga nalo mara mbili Myamba kichwani kwa nyuma akaanguka sakafuni na akafariki dunia.
Ndipo Dani alichukua mifuko ile miwili ya nailoni na kuitandika sakafuni.
Baadaye akachukua mwili wa Myamba na kuuweka juu ya ile mifuko ya nailoni ili kuepuka damu kusambaa.
Baadaye aliukata mwili vipande viwili kuanzia kiunoni na vipande hivyo akavitumbukiza kwenye mifuko miwili.
Kwa uangalifu mkubwa, akachukua mifuko ile ya nailoni nayo akaitumbukiza kwenye mifuko ya sandarusi na hii aliifanya ili iwe rahisi kubeba vifurushi hivyo wakati akipita getini ambako walinzi waliokuwa zamu, hawakuhisi chochote.
Baada ya kumaliza kutekeleza mauaji, Dani alideki chumba ili kupoteza ushahidi wa nini kilichotendeka akitumia majoho ya kanisa yaliyokuwa yameandikwa “Parokia ya Makambako Tanzania.”
Dani baada ya kumaliza kufanya usafi, aliendelea kupoteza ushahidi wa silaha aliyoitumia kwenye mauaji kwa kutumbukiza kile kipande cha bomba la chuma kwenye bomba linalokusanya maji ya mvua kutoka kwenye bati kuleta chini.
Alienda kutupa lile panga alilolitumia kutenganisha mwili kwenye shimo la choo la Shule ya Msingi Makambako wakati nguo alizozitumia kudeki na kufuta damu, aliziweka kwenye mfuko wa sandarusi na kuutumbukiza chooni.
Baada ya kumaliza, alichukua simu za marehemu, akafunga duka na kuondoka lakini muda wote akifanya shughuli ya mauaji, simu ya marehemu ilikuwa ikiita kwa sababu viongozi wa kanisa walitaka kujua nini kilichojitokeza katika makabidhiano.
Simu hizo zilikuwa zikipigwa na Katibu Mtendaji wa Parokia ya Makambako, Moses Lubangula na Luciana Mduge ambaye ni mke wa marehemu kwa sababu tayari alikuwa amepata mashaka kwa sababu mumewe hana utamaduni wa kuchelewa kurudi nyumbani.
Ujumbe mfupi (SMS) kutoka simu ya marehemu
Mke wa marehemu, Luciana Mduge aliyekuwa shahidi wa kwanza wa Jamhuri, alieleza kuwa mumewe alikuwa na simu mbili, moja ilikuwa na laini ya Airtel na nyingine ya Vodacom na laini ya vodacom ndio ilikuwa ikitumika mara kwa mara.
Alieleza kuwa kwenye saa 4:00 usiku, alijaribu kumpigia mumewe lakini namba zote mbili zilikuwa hazipatikani, akaona amtafute mtawa mmoja ambaye alikuwepo eneo la kanisa na kumuuliza, ili afahamu ni kipi kimemtokea mumewe.
Mtawa huyo akamweleza kuwa mumewe alikuwa kwenye kikao na muda si mrefu angerejea nyumbani lakini usiku uleule akapokea meseji (SMS) iliyomtia mashaka kutoka kwa mumewe ikisema Nickson amepata ajali na yuko hospitali amepoteza fahamu.
Ujumbe huo ulisomeka; “Nipo hospitali” na ujumbe mwingine ukasema “nimepata ajali sijitambui.”
Alisema baada ya kupokea ujumbe huo alimpigia simu tena mtawa, lakini safari hii alikuwa hajui nini kimempata mumewe hasa.
Lakini mke huyo alimjulisha pia shahidi wa pili, Michael Kihaga ambaye ni Mwenyekiti wa Kigango.
Hata hivyo, alimjibu kuwa mumewe ametumia SMS kupitia laini ya Vodacom saa 1:30 usiku.
Alisema SMS hiyo ilikuwa ikimjulisha kuwa makabidhiano yalikuwa yamekwenda vizuri na ujumbe huo ulisomeka; “Tayari imewezekana” na baada ya kupokea ujumbe huo mwenyekiti huyo alisema akaenda kulala akiamini shughuli nzima ya makabidhiano ilikuwa imeenda vizuri.
Lakini alisema alishangaa, saa 5:00 usiku huohuo alipokea tena ujumbe mwingine kutoka kwa simu ya Myamba ikimjulisha kuwa amepata ajali na anaelekea hospitali na ulisomeka; “Nilipokuwa narudi nyumbani nilipata ajali hivi sasa nakwenda hospitali.”
Baada ya kupokea ujumbe huo, Kihaga akaamua kupeleka taarifa hiyo kwa Mwenyekiti wa Parokia, Justin Sanga na kwa mke wa marehemu, akiwajulisha kuwa amepokea SMS zinazofanana kimaudhui na zile alizokuwa amepokea mke wa marehemu.
Hapo uamuzi ulifikiwa kuwa waende kituo cha Polisi Makambako kutoa taarifa na pia kujiridhisha kama kuna taarifa zozote za ajali, lakini uongozi wa Kanisa ukimjumuisha Justin Sanga ulienda kwanza nyumbani kwa Nickson Myamba na kumchukua mkewe.
Walikwenda pamoja kituo cha Polisi Makambako ambako polisi waliwaeleza kuwa kulikuwa hakuna taarifa yoyote ya uwepo wa ajali na wakawashauri waende kuulizia hospitali ambako kote huko waliambiwa hawajapokea majeruhi yeyote wa ajali.
Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii kupata mwendelezo wa simulizi hii ya hukumu ya Katekista aliyeua.