Johannesburg, Afrika Kusini. chama cha African National Congress (ANC), kimesema kuwa kitavishawishi vyama vingine kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Cyril Ramaphosa bungeni ili kumruhusu kuunda uongozi.
Chama hicho kimetoa kauli hiyo leo Juni 2,2024 kufuatia kuhesabiwa asilimia 99 za uchaguzi uliofanyika Mei 29,2024 ambapo chama hicho kiliongoza kwa asilimia 40.2 katika uchaguzi huo, chama cha Democratic Alliance (DA) kikifuatia kwa asilimia 21.78, uMkhonto weSizwe (MK) asilimia 14.59. ANC inahitaji kushirikiana katika muungano wa vyama kuunda serikali, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.
Chama hicho kikongwe kilichodumu madarakani kwa miongo mitatu iliyopita leo Jumapili Juni 2, 2024 kimesema kitaingia kwenye mazungumzo na vyama vingine ili kuunda Serikali mpya.
“ANC imejitolea kuunda Serikali inayoakisi matakwa ya watu, ambayo ni imara na yenye uwezo wa kutawala kwa ufanisi,” Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula amewaambia waandishi wa habari hii leo.
Mbalula amesema Chama lazima kijadiliane na Serikali ya mseto au kuwashawishi wengine kuunga mkono kuchaguliwa tena kwa Ramaphosa bungeni ili kumruhusu kuunda uongozi.
“Tunataka kuwahakikishia watu wa Afrika Kusini kwamba tumewasikia. Tumesikia wasiwasi wao, masikitiko yao na kutoridhika kwao.”
Aidha Mbalula ameweka wazi kuwa ANC itafanya majadiliano ndani na makundi mengine katika siku chache zijazo.
Hata hivyo matokeo ya mwisho yatatangazwa rasmi leo Jumapili jioni, huku Ramaphosa akitarajiwa kutoa hotuba wakati wa hafla rasmi karibu na Johannesburg.
Kutokana na kutangazwa rasmi kwa matokeo vyama vya siasa vitakuwa na wiki mbili kufanya makubaliano kabla ya bunge jipya kuketi kumchagua rais, ambaye kuna uwezekano bado ataweza kuibuka kutoka ANC kama chama kikubwa zaidi.
Hadi sasa takwimu kutoka Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) inaonyesha Chama cha pili ni Democratic Alliance (DA) kikiwa kimepata kura milioni 3.4 sawa na asilimia 21.78, huku uMkhonto we Sizwe (MK) kinachoongozwa na Rais wa zamani Jacob Zuma kimeshika nafasi ya tatu kikiwa na kura milioni 2.3 sawa na asilimia 14.58, ikiwa ni jambo la kushangaza kwa chama kilichoanzishwa miezi michache iliyopita.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF), kinachoongozwa na kiongozi wa zamani wa vijana wa ANC, Julius Malema, kimekuwa cha nne kikipata kura milioni 1.5 sawa na asilimia 9.51.
Kupoteza kura kwa ANC kunaashiria mabadiliko ya kihistoria kwa Afrika Kusini kwani chama hicho kimekuwa kikipata wingi wa kura tangu 1994, wakati Nelson Mandela alipoliongoza taifa hilo kutoka kwa utawala wa Wazungu wachache na kuingia katika demokrasia.