KUNYANYUA upanga juu ni ishara tosha kuwa tayari kwa mapambano. Ndio! yupo tayari Kelvin John kwa hilo ikiwa ni siku chache tu tangu atambulishwe kuwa mchezaji mpya wa Aalborg BK ya Denmark baada ya kumaliza mkataba wa kuichezea KRC Genk ya Ubelgiji.
Licha ya mambo kutomwendea vile ilivyokuwa ikitarajiwa na wengi ndani ya miaka mitatu akiwa na Genk alikopita pia nahodha na Taifa Stars, Mbwana Samatta na kufanya makubwa, hii ni nafasi nyingine kwa kinda huyo.
Kelvin mwenye kasi na maarifa, aliishia kucheza mchezo mmoja tu wa ushindani akiwa na kikosi cha kwanza cha Genk, alitumika mara nyingi katika timu za vijana kutokana na ufinyu wa nafasi kwa wababe hao hadi mkataba wake ulipofikia ukomo.
Katika mahojiano ambayo amefanya Denmark, Kelvin ameonyesha shauku ya kujitafuta na kufanya makubwa akiwa na chama lake jipya atakalolitumikia kwa miaka mitatu hadi Julai 2028.
“Nimekuwa na shauku ya kuwa sehemu ya kikosi cha AaB (Aalborg BK), na nina furaha nimetua mahali pake, ili niweze kuvaa jezi nyekundu na nyeupe ya AaB baada ya mapumziko ya majira ya joto na kuingia kwenye uwanja mzuri,” anasema nyota huyo na kuongeza;
“Mara ya kwanza kabisa AaB ilipoonyesha nia, nilidhamiria kuja hapa, na kupitia mazungumzo yangu na klabu nimepata hisia nzuri, nimefuatilia na kuona mtindo ambao klabu inacheza unanifaa, kikamilifu.”
Anaendelea katika mahojiano hayo kwa kusema; “Natumaini kwa kasi yangu, bidii yangu katika uchezaji tena na mawazo yangu ya kupenda kuwa mshindi naweza kusaidia timu wiki baada ya wiki na wakati huo huo kustawi kama mchezaji katika ligi (Super League).”
Kelvin ambaye amepewa jezi namba 27, ni usajili wa kwanza katika klabu hiyo ndani ya majira haya ya kiangazi, amebeba matumaini makubwa kutokana na uzoefu wake pamoja na kipaji alichonacho.
Ikumbukwe kuwa mbali na kushindwa kupenya katika kikosi cha kwanza, Kelvin alikuwa akicheza mara kwa mara katika kikosi cha vijana kilichokuwa kikishiriki madaraja ya chini Ubelgiji kwa ajili ya kujiweka sawa kiushindani.
Pia nyota huyo alicheza michuano ya Ulaya, ligi ya mabingwa kwa vijana wakati ambao KRC Genk ilipata ticketi hiyo baada ya kumaliza msimu wa 2020/21 ikiwa nafasi ya pili katika ligi ‘Jupiler Pro League’.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa michezo wa AaB, Ole Jan Kappmeier anasema wanaamini kupitia kipaji cha Kelvin ndio maana waliamua kuipambania saini yake.
“Kelvin John ni mchezaji mzuri ambaye tunaamini anaweza kukua vyema kisoka na kupata mafanikio akiwa na AaB. Ana kasi, maarifa uwezo wa kumiliki mpira, tunamwona kama nyongeza ya kusisimua kwenye kikosi chetu,” anasema Ole Jan Kappmeier.
Mashabiki mbalimbali wa timu hiyo, wamempokea vizuri Kelvin kwa kuonyesha matumaini makubwa juu yake katika mitandao ya kijamii wapo wanaomfananisha na Nicklas Helenius ambaye anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea.
Hansen alisema,”karibu sana Kelvin, tunasubiri kwa hamu kukuona ukiwa na jezi za timu yetu wewe ni Helenius mpya kabisa, ukiwa na damu changa.”
Helenius ndiye mfungaji bora wa muda wote kwa chama hilo jipya kwa Kelvin, mwamba huyo anashikilia rekodi hiyo akifunga mabao 62 katika michezo 205. Bado yupo kikosini akiwa na miaka 33 lakini kwa sasa amepungua makali.
Zipo ripoti kuwa huenda huu ukawa ndio msimu wa mwisho kwa lijendi huyo ambaye msimu uliopita alicheza michezo minne tu pengine ndio sababu ya mashabiki hao kumwona Kelvin ndiye Helenius ajae.
AaB ilianzishwa Mei 13, 1885 na wahandisi wa Kiingereza waliokuwa wakijenga mfumo wa reli wa Jutland, na miaka ya kwanza ilijikita kwenye mchezo wa kriketi.
Hapo awali iliitwa Aalborg Cricketklub (Klabu ya Kriketi ya Aalborg) lakini jina la klabu hiyo lilibadilishwa na kuwa Aalborg Boldklub (Aalborg ballclub) mwaka 1899 ndipo soka likaanza kuchezwa.
Tangu wakati huo ndio ukawa mchezo mkuu katika klabu hiyo. Mwaka 1995 AaB iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Denmark kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilipotunukiwa nafasi kwa sababu Dynamo Kyiv kutupwa nje ya michuano hiyo baada ya kujaribu kupanga matokeo.
Klabu hiyo kwa sasa inashiriki ligi daraja la kwanza nchini humo maarufu kama NordicBet Liga kuanzia 2023 hadi 2024 baada ya kushuka daraja kutoka Denmark Superliga msimu wa 2022-23.
Ligi Kuu ‘Danish Superliga’
Mabingwa (4): 1994-95, 1998-99, 2007-08, 2013-14
Nafasi ya tatu (3): 1935-36, 1969, 2006-07
Daraja la kwanza ‘Danish 1st Division’
Daraja la pili ‘Danish 2nd Division’
Kombe la FA ‘Danish Cup’
Mabingwa (3): 1965-66, 1969-70, 2013-14
Washindi wa pili (10): 1966-67, 1986-87, 1990-91, 1992-93, 1998-99, 1999-2000, 2003-04, 2008-09, 2019-20, 2022-23
Ngao ya jamii ‘Danish Supercup’
Nafasi ya pili (3): 1995, 1999, 2004