Dar es Salaam. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua akaunti ya mfugaji mahususi kwa ajili ya wadau wa sekta ya ufugaji nchini.
Huduma hiyo ya kwanza kutambulishwa na benki hiyo nchini imeanzishwa maalumu kwa kundi hilo, pamoja na kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta hiyo kupitia huduma za fedha zilizorahisishwa.
Akizungumza Leo Jumapili Juni 2, 2024 katika hafla ya utambulisho wa huduma hiyo uliofanyika katika Soko la mifugo Pugu mnadani, Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini hapa, Edward Mpogolo amesema pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa kubuni huduma hiyo muhimu, amesema ujio wake ni ukombozi kwa wadau wa sekta ya mifugo nchini.
Amesema kilio kikubwa kwa wadau wa sekta ya mifugo ilikuwa ukosefu wa huduma za kibenki zinazoendana na mahitaji yao.
“Kwa mfano katika mnada huu wa Pugu unahusisha mzunguko wa fedha wa wastani wa Sh1 bilioni kila siku, wafanyabiashara wengi wanajikuta wanatembea na fedha taslimu kitu ambacho ni hatari kwao.”
“Sasa huduma za kifedha ikiwemo miamala zitapatikana kwenye maeneo ya minada hii karibu yao kabisa,’’ amesema mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo Mpogolo ameiomba NBC kupitia huduma hiyo kuhakikisha inawasaidia zaidi wafugaji kwa kuwekeza zaidi kwenye suala zima la utoaji wa elimu ya fedha, ufugaji wa kisasa na masoko ili wanufaike zaidi.
Awali akizungumzia huduma hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na wakubwa wa NBC, Elibariki Masuke amesema inahusisha wafugaji mmojammoja na vikundi huku ikitoa faida mbalimbali ikiwemo mikopo kwa ajili ya sekta ya ufugaji.
“Kwa upande wa wafugaji wa vikundi au vyama pia hawatakiwi kuwa na hofu sababu watakuwa na uhuru wa kuweka na kutoa fedha zao wakati wowote na pia watapata kitabu cha hundi kwa gharama nafuu, wanachotakiwa ni kufungua akaunti bure kabisa kwenye matawi yote kote nchini,” amesema.
Akifafanua zaidi kuhusu huduma hiyo Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo kutoka benki hiyo, Raymond Urassa amesema inahusisha wafugaji wa mifugo ya aina zote wakiwemo ng’ombe na kuku na hatua hiyo ni mwendelezo wa jitihada za benki hiyo kuyafikia makundi yote ya uzalishaji nchini.
“Hivi karibuni tumetoka kuzindua huduma ya Bima kwa wakulima na sasa ni wakati wa kuwageukia wafugaji nao waweze kunufaika na huduma hizi za NBC,’’ amesema Urassa.
Akizungumzia huduma hiyo, Mkuu wa Mnada wa Pugu, Noel Byamungu amesema imekuja wakati muafaka na itakuwa suluhisho kwa wafugaji, wafanyabiashara wa mifugo na wadau wengine sokoni hapo.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mifugo kwenye mnada huo, Iddy Maziku amesema wanaamini kupitia huduma hiyo sasa hawatalazimika tena kutembea na fedha taslimu ili kufanya malipo ya manunuzi ya mifugo na huduma nyingine.