MWISHONI mwa msimu huu, inaelezwa Yanga Princess itaachana na kocha mkuu, Charles Haalubono baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu ya wanawake (WPL) na jicho la wananchi lipo kwa Edna Lema ‘Mourinho’ kuwa mbadala wake.
Huu unaweza kuwa msimu mbaya zaidi kwa Yanga baada ya kufungwa na timu tatu tofauti nyumbani na ugenini ikichapwa na Ceasiaa Queens 3-1, Simba Queens 6-2 na JKT Queens 5-1 na hadi sasa ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na pointi 27.
Sababu ya Edna kurejeshwa Yanga inaelezwa ni baada ya Mzambia Haalubono kufanya vibaya zaidi msimu huu jambo lililowafanya waanze kumtafuta mrithi wake mapema kwa ajili ya mazungumzo.
Mwanaspoti linafahamu Edna ambaye ni kocha msaidizi wa Biashara United inayoshiriki Championship yupo Dar es Salaam tangu mwezi uliopita akionekana kwenye baadhi ya mechi za Yanga.
Inaelezwa kuwa viongozi wa timu hiyo wamekaa kujadili namna ya kumrejesha kocha huyo ambaye mkataba wake na Biashara upo ukingoni ingawa inaelezwa ofa aliyopewa na wananchi hao wa kike hajairudisha mezani.
Mmoja wa viongozi wa Yanga Princess (jina tunalo) alisema wamefikia uamuzi wa kutaka kumrejesha kocha huyo kutokana na kulifahamu soka la wanawake na kubwa zaidi ni kocha mzawa.
“Msimu huu umekuwa mgumu zaidi kwetu na viongozi wamefanya tathmini wakagundua kuna shida kwa kocha ambaye bado hajazoea mazingira ya Tanzania hivyo jina ambalo liko mezani hadi sasa ni Edna ingawa bado kuna taratibu hazijakamilika,” alisema kiongozi huyo.
Akizungumza na gazeti hili, Mratibu wa Yanga Princess, Kibwana matokeo alisema: “Mimi mwenyewe nasikia tetesi hizo lakini sina taarifa juu ya usajili wa kocha huyo.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Edna alisema kuwa ni kweli mkataba wake unatamatika mwezi huu lakini kuhusu kurudi Yanga ni tetesi tu.
“Ngoja kwanza msimu uishe tutajua tunafanyaje lakini hizo ni tetesi bado sijatafutwa na Yanga wakinifuata mtajua tu, mambo hayajifichi.”
Msimu wa 2021, Lema alifanikisha timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.