BAADA ya kudumu kwa msimu mmoja hatimaye kiungo mshambuliaji wa Yanga Princess, Kaeda Wilson anarudi nchini Marekani lakini akiwa na kumbukumbu ya kufunga mabao kwenye mechi za dabi.
Kiungo huyo ataondoka nchini mwezi huu kuendelea na masomo kwenye Chuo cha UTAH kilichopo nchini kwao baada ya kucheza Yanga msimu mmoja.
Mchezaji huyo hadi raundi ya 15 amefunga mabao manne, Yanga ikisalia nafasi ya nne na pointi 27 kwenye msimamo wa Ligi ya Wanawake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaeda alisema anaondoka nchini lakini atakumbuka upendo alioonyeshwa na Watanzania kubwa zaidi kwake ni kucheza michezo mikubwa ya dabi na kufunga mabao ingawa timu yake haikushinda.
“Hakika nitakumbuka ugumu wa mazoezi au tulipopoteza mechi, lakini nitakumbuka upendo walionionyesha wachezaji wenzangu na benchi la ufundi,” alisema Kaeda na kuongeza:
“Kubwa zaidi ni vile mashabiki wakiniita mzungu kila wanionapo, licha ya kupoteza mechi ya dabi lakini kwangu ilikuwa furaha kuifunga Simba mabao mawili.”