Geita. Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha maeneo yote ya utawala yanayotoa huduma karibu na wananchi yanaimarishwa kwa viwango.
Majaliwa amesema hayo leo Jumapili Juni 2, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale linalojengwa kwa zaidi ya Sh4 bilioni.
Amesema halmashauri ni mpya nchini iliyoanza kufanya kazi zake kwenye majengo ya kupangisha lakini sasa, wamefanikiwa kuhamia kwenye jengo lao na kuwataka watumishi kufanya kazi kwa bidii ili wawaletee maendeleo wananchi.
Majaliwa amesema Serikali imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo sekta ya elimu, afya, miundombinu na huduma za umeme lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wote hasa wa vijijini wanapata huduma stahiki.
Katika hatua nyingine, amewataka watumishi wa umma nchini wakuu wa idara kuwa na mpango kazi unaohusisha kuwatembelea wananchi vijijini na kuwasikiliza badala ya kusubiri wawafuate ofisini.
“Sote lazima tuwe na mpango kazi unaohusisha kuwatembelea wananchi vijijini ambao hawana uwezo wa kusafiri na kuja ofisini, tengeni siku mbili au tatu za kuwatembelea wananchi naamini mtafanya hivyo, wakurugenzi simamieni watu wenu kuhakikisha hili linatekelezwa,” amesema Majaliwa.
Pia, amesema Serikali inatambua wilaya mpya zilizopo pembezoni zenye changamoto nyingi, lakini zifanye kazi kwa bidii na kuwatumikia wananchi ili waendelee kuiamini Serikali iliyopo madarakani.
“Mko hapa kwenye wilaya ya pembezoni najua maeneo haya mapya yana changamoto nyingi endeleeni kuchapa kazi na kuwatumikia wananchi,” amesema Majaliwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Husna Toni akizungumzia ujenzi wa jengo hilo amesema ulianza mwaka 2021 na mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 87.
Amesema ujenzi wake umegharimu Sh3.9 bilioni, “ili ukamilike kabisa kwa asilimia 100 Sh1.9 bilioni nyingine zinahitajika.”
Pia, akiwa wilayani humo, Majaliwa amezindua jengo la uwezeshaji wananchi kiuchumi lililojengwa kwa Sh247.1 milioni litakalosaidia wajasiriamali kupata elimu ya kuongeza thamani ya mazao wanayozalisha.
Jengo hilo pia, litasaidia kupata elimu ya masoko ya bidhaa,uzalishaji kwa kutumia teknolojia itakayoongeza tija katika uzalishaji, kusajili biashara na kupata elimu ya kati na ya juu ndani.
Mkuu wa wilaya hiyo, Grace Kingalame amesema tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani Sh28 bilioni zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya, elimu na utawala.