KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI MAKOME WILAYANI MTWARA,AWAPONGEZA WATENDAJI WA RUWASA KWA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA ZA MIRADI YA MAJI


WANANCHI wa kijiji cha Makome na Makome B wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara,wamepata matumaini ya kuondokana na adha ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),kuanza ujenzi wa mradi wa maji ya bomba.

Wananchi wa vijiji hivyo,kwa muda mrefu wanalazimika kuamka usiku wa manane kila siku kwenda kijiji jirani cha Nachenjele umbali wa zaidi ya kilometa 5 kwa ajili ya kuchota maji na wengine wanalazimika kutumia maji ya visima vya asili na mabonde ambayo sio safi na salama.

Matumaini hayo yamekuja baada ya Wizara ya maji kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) chini ya mpango wa lipa kwa matokeo(PforR),kutoa Sh.milioni 605,662,947 ili kujenga mradi mkubwa wa maji utakaomaliza changamoto hiyo iliyokuwepo tangu Uhuru.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Menej wa Ruwasa wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike amesema,mradi huo umeanza kujengwa Mwezi Novemba 2023 na utakamilika mwezi Novemba mwaka huu

Mashindike amesema,mradi huo umefikia asilimia 70 na unatarajia kuhudumia zaidi ya wananchi 1,584 ambapo wananchi 858 wanatoka kijiji cha Makome na 726 wanatoka kijiji cha Makome B.
Amesema,mpaka sasa mkandarasi anayejenga mradi huo Kampuni ya M/S Kellogg Construction Ltd ameshalipwa kiasi cha Sh.168,524,526.96 kama malipo ya awali na lengo la kujenga mradi huo ni kusogeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Halmashauri ya wilaya Mtwara.


Kwa mujibu wa Mashindike ni kwamba,mradi wa maji Makome umehusisha ujenzi wa matenki mawili yenye ujazo wa lita 50,000 kila moja na mnara wa mita 9 ambap tenki moja limejengewa kijiji cha Makome na lingine katika kijiji cha Makome B.

Ameeleza kuwa,mradi umehusisha ujenzi wa vituo 7 vya kuchotea maji,nyumba ya Mhudum,nyumba ya mitambo ya maji,kupeleka umeme kwenye chanzo cha maji,kujenga ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO) ununuzi na ulazaji bomba za maji umbali wa kilometa 4.1.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava,amefurahishwa na watendaji wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini( Ruwasa) wilaya ya Mtwara kwa kutekeleza mradi huo kwa viwango na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi kabla ya haujakamilika.

Alisema,lengo la Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,ni kutaka kuona wananchi wanapata huduma ya maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao ili kuwapa nafasi ya kujikita katika shughuli za maendeleo.
Mnzava,amewapongeza watendaji wa Ruwasa kwa matumizi sahihi ya fedha zinazoletwa ili kutekelezaji miradi ya maji na kwa kufuata sheria za manunuzi ya umma

Pia,amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuwa walinzi wa kwanza na kuhakikisha wanatunza mradi huo na miundombinu yake ili uweze kudumu kwa muda mrefu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji cha Makome, wameishukuru serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira(Ruwasa) kwa kuwajengea mradi wa maji ya bomba unaokwenda kumaliza adha ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Hamza Mohamed amesema,tangu Uhuru mwaka 1961 hawajawahi kupata maji ya bomba,hivyo kujengwa kwa mradi huo ni kama ukombozi wa maisha yao yaliyojaa tabu na mateso makubwa.


Sofia Athuman amesema,mradi huo utakapokamilika utawasaidia kumaliza kero ya kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji badala ya kufanya shughuli zao za maendeleo.

Hata hivyo,ameiomba serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Mtwara,kuwa karibu na Mkandarasi ili aweze kukamilisha kazi ya ujenzi wa mradi huo mapema na waanze kupata huduma ya maji kwenye makazi yao.



Related Posts