NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM),Mkoa wa Mwanza kimeibomoa ngome ya CHADEMA wilayani Ilemela baada ya wanachama 18 akiwemo katibu wa tawi la Nyambiti,kusamilisha kadi zao na kujiunga na CCN.
Wafuasi hao wapya wa CCM wamejiunga leo baada ya Halmashauri Kuu ya CCM kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake hao 17, aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Tawi la Nyambiti wilayani Ilemela,Joseph Kimune amesema wamejiunga na CCM baada ya kuridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Amesema kuwa amerejea CCM kupambana na wapinga maendeleo na yupo tayari kupambana kuhakikisha inaendelea kushika dola iendelee kuwaletea wananchi maendeleo ya dhati.
“Binafsi nikoshwa sana na utendaji wa Rais Dk.Samia,umesababisha nirudi CCM badala ya kuendelea kubaki kutukana watu wanaoleta maendeleo,”amesema Kimune.
Kiongozi huyo wa zamani wa CHADEMA,alisema tawi lote la Nyambiti limejiunga na CCM baada ya kuchoshwa na matusi ya viongozi wao dhidi ya waleta maendeleo.
“Watu wanazungumza ukabila wakati Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere alishatukaza kuzungumzia ukabila isipokuwa kwa utani huku akionya ukabila ni dhambi mbaya ya ubaguzi akiifananisha na mtu aliyekwisha kula nyama ya mtu,akiisha kuila ataendelea kuila.
Awali Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza,Omar Mtuwa amesema wafuasi hao wapya wa CCM wameridhishwa namna serza nzuri za CCM zinavyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa mwanamke hodari na jemedari,Mama Dk. Samia kupitia utekelezaji wa ilani kwa mafanikio makubwa mkoani humu.
“Niwapongeze wenzetu hawa kutoka vyama rafiki ambao kwa hiari yao wenyewe leo wameamua kujiunga na CCM baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa sera na ilani yake,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ kabla ya kufunga mkutano wa Halmashauri Kuu, aliwapongeza kwa uamuzi wao wa busara na kuwataka washirikiane kukijenga Chama.
“Niwapongeze kwa uamuzi wenu wa busara uliowasukuma kujiunga na CCM,Chama chenye sera nzuri na wala hamjakosea,tuendelee kuchapa kazi na kumuunga mkono Rais Dk.Samia nchi ipate maendeleo,”amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ akipokea kadi ya CHADEMA kutoka kwa mmoja wa waliokuwa wananchama wa chama hicho ,leo baada ya kujiunga na CCM.Kulia ni Katibu wa Mkoa Omar Mtuwa.
Aliyekuwa Katibu wa CHADEMA, tawi la Nyambiti,wilayani Ilemela,Joseph Kimune akizungumza baada ya kuachana na chama hicho na kujiunga na CCM, nyuma ni wanachama wengine waliokuwa CHADEMA.Picha na Baltazar Mashaka