Siri ya Taliss ubingwa wa kuogelea hii hapa

Nahodha wa Taliss Swim Club, Delbert Ipilinga amefichua siri ya kuibuka washindi wa jumla kwenye michuano ya 16 ya Klabu Bingwa Tanzania (TNCC) kuwa ni bidii na uthubutu.

Klabu hiyo ilikusanya pointi 385 katika michuano ya siku mbili iliyofanyika katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Nashukuru tumetwaa ushindi wetu wa sita wa TNCC na hili limechangiwa na bidii na ari yetu sisi kama wachezaji pamoja na benchi la ufundi,” alisema na kuongeza;

“Tuna makocha wazuri ambao wanatunoa vyema ili tuwe waogeleaji washindani na wakati huo huo, tunafanikiwa kutumia maelekezo yote tunachojifunza kutoka kwake,” alisema Ipilinga.

Alisema ushindi walioupata watautumia kama hamasa ili kushinda michuano mingi iwezekanavyo.

Muogeleaji Sofia Latiff alisema kufanya kazi kama timu pia kuliwasaidia sana kung’ara kwenye mashindano ya TNCC mwaka huu.

Sambamba na hilo, kocha wa Bandari Swim Club yenye maskani yake nchini Kenya, Fakhry Mansoor alisema wakiwa timu ya wageni, wamefurahia mashindano hayo huku akitoa sifa kwa Tanzania kwa kupiga hatua katika kuogelea.

“Zamani tulikuwa tunang’ara kwa waogeleaji wa Tanzania katika mashindano mbalimbali lakini mambo yamebadilika kwa sasa, wanafanya vizuri zaidi yetu Tanzania inazidi kupanda,” alisema.

Wakati huohuo, Dar Swim Club imeambulia nafasi ya pili kwa pointi 330 huku Mwanza Swim Club ikishika nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 96 na nafasi ya nne ni Bandari Swim Club (Kenya) iliyojinyakulia pointi 88.

Klabu ya Reptide Swim Club ilishika nafasi ya tano kwa pointi 54, Bluefins Swim Club nafasi ya sita kwa pointi 34, Lake Victoria Sports Club nafasi ya saba kwa pointi 25 na FK Blue Marlins ilikuwa ya nane baada ya kuzoa pointi 13.

Lifetime Swim Club na Champion Riase Swim Club zote zilishinda pointi 6 ili kuchukua nafasi za tisa na kumi ambapo Mis Piranhas aliketi chini ya ngazi na pointi moja.

Related Posts