KATIKA kuhakikisha usawa wa kijinsia kwenye mchezo wa gofu, klabu ya TPC Moshi imeanza rasmi mchakato wa kuongeza idadi ya wachezaji wa kike.
Mzuka wa gofu, kupitia gazeti la Mwanaspoti limefanya mahojiano na nahodha wa TPC, Jafari Ali ambaye anataja mipango ya klabu hiyo.
Anasema mkakati wa klabu hiyo ni kuhakikisha wanawapata wanachama wa kike 40 wa Klabu ya TPC watakaokuwa wanapatiwa mafunzo katika klabu hiyo.
“Wanawake hawapo nyuma, naamini wanaweza kufanya makubwa kama wataendelezwa na hilo ni jambo kubwa kwenye mchezo huu hatuna,” alisema Jafar.
Ingawa wameanza kuwashawishi wanawake hao lakini tatizo kubwa kwao ni ukosefu wa vifaa vya kufundishia.
Anasema hadi sasa tayari wameuomba uongozi wa Chama cha gofu nchini (TGU), ili waweze kuwasaidia changamoto hiyo.
“Kwa sasa tuna vifaa vya kutosha kufundishia na hata fimbo tulizokuwa nazo ni za kupokezana tunaamini kama TGU ikitusaidia kidogo itarahisisha kazi,” anasema Ali.
Ukiachana na wanawake pia mipango yao ni kuwa na kituo cha Akademi kitachokuwa kinatoa mafunzo ya mchezo wa gofu kwa vijana wadogo.
Jambo lingine wanalotarajia kulifanya kwa mwaka huu ni kuwekeza nguvu shuleni, ili kupata watoto angalau wanaoonyesha wanaweza kucheza.
“Katika eneo la TPC kuna shule tano za msingi na shule mbili za Sekondari, hivyo kwa upande wetu inakuwa ni rahisi kuwafikia,” anasema Ali.
Anasema hadi sasa wana watoto 70 wanaopatiwa mafunzo klabuni hapo lakini asilimia 50 ya wachezaji wanaotoka timu ya taifa ya vijana wanatoka TPC.
Mchezaji kutoka klabu hiyo, George Sembi anasema ingawa wamekuwa wakipambana kuwapata wachezaji wa kike lakini wanao saba.
“Bado ni wageni wanahitaji kuelekezwa kila wakati, ili umakini kuongezeka na ukomavu kimbinu, ndio tunaowategemea wakiendelea kukua kwenye uzoefu, watakuwa msaada kwenye timu ya taifa ya wanawake, anasema Sembi na kuongeza
“Kwa watoto nimekuwa nikipokea simu nyingi za wazazi wa wanafunzi waliohamasika, wakiomba watoto wao wapate nafasi ya kujifunza kucheza gofu.”
Clara Mushi ambaye ni mmoja wa wachezaji waliojiunga hivi karibuni anasema ametokea kuupenda na anashangaa kwa nini alichelewa kujifunza mchezo huo.
“Kwa kweli nilivyokuwa naona wakicheza nilijua ni mchezo wa matajiri, kumbe mtu yeyote anaweza akacheza, umenipa hamasa ya kuendelea kupambania najua siku moja na mimi nitafika mbali,” anasema Clara.