ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, amekata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyomng’oa madarakani na kumpa ushindi Joseph Mbilinyi (Sugu). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Mchungaji Msigwa ametangaza kusudio hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni siku chache tangu uchaguzi huo wa kusaka viongozi wa Chadema Kanda ya Nyasa, kufanyika.
Mchungaji Msigwa amesema tayari rufaa hiyo ameiwasilisha kwa Kamati Kuu ya Chadema, jana tarehe 2 Juni 2024.
“Ni kweli nimekata rufaa Kamati Kuu jana sasa sijui lini watajibu. Msingi wa rufaa napinga matokeo ya uchaguzi nataka uchaguzi uitishwe upya kwani wa mwanzo ulikuwa sio wa haki kulikuwa na fujo pamoja na wapiga kura watatu kuzuiwa kupiga kura,” amesema Msigwa akizungumza na MwanaHALISI Online.
Katika malalamiko yake, Mchungaji Msigwa anadai uchaguzi huo haukuwa wa haki akidai wasimamizi wake walikuwa na upendeleo.
Pia, Mchungaji Msigwa amedai kuna wajumbe halali waliopaswa kupiga kura siku ya uchaguzi lakini hawakuruhusiwa.
“Tunalalamikia Serikali ya CCM kwamba wasimamizi wa uchaguzi huwa hawatendi haki, Chadema iliyotakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwamba chaguzi zetu wanaosimamia wanatenda haki. Sasa kama Mimi mjumbe wa kamati kuu natoa malalamiko hayasikiliziwi tena ndani ya Chadema chenye kutenda haki nani atasikilizwa?” amesema Mchungaji Msigwa.
Mwanasiasa huyo ameendelea kulalamika “watu watatu hawakuruhusiwa kupiga kura, lakini kama haitoshi wale walioleta fujo wakati wa mchakato unavyotaka kuanza wa kupiga kura mbeke ya msimamizi wa uchaguzi Benson Kigaila, wakawa wanatukana Kigaila hakuchukia hatua yoyote kama ambavyo hakuchukua hatua kule Njombe kwa wale walifanya fujo.”
Mchungaji Msigwa amedai kuwa, kabla ya uchaguzi huo kufanyika aliona zengwe na kutoka malalamiko yake hadi ndani ya Kamati Kuu ya Chadema, lakini hayakufanyiwa kazi
MwanaHALISI imemtafuta aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Benson Kigaila, kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa malalamiko hayo bila mafanikio.
Sugu alifanikiwa kumng’oa madarakani Mchungaji Msigwa baada ya kupata ushindi mwembamba.
Baada ya matokeo ya uchaguzi huo Mchungaji Msigwa aliahidi kuheshimu matokeo hayo.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo, Sugu alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 54 wakati Msigwa akipata kura 52.