Serikali kutunga sera kuzilea kampuni changa

Seoul. Serikali imeanza mchakato wa kutunga sera kwa ajili ya kampuni changa (startups), ili kujenga mazingira mazuri ya ukuaji wa bunifu za watu na kuzilea hadi kuwa kampuni kubwa.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Juni 3, 2024 Seoul, Korea Kusini na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alipotembelea Kituo Atamizi cha Kimataifa cha kukuza Wabunifu Korea (GCCEI) kujionea shughuli za kituo hicho.

Nape ambaye ni mmoja wa mawaziri walioambata na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake nchini Korea Kusini, ametembelea kituo hicho akiwa pamoja na wabunifu wa Tanzania kwa lengo la kuwapa motisha kwa kile wanachokifanya Wakorea.

Akizungumzia ziara hiyo, Nape amesema Serikali itajenga Kituo Atamizi cha Ubunifu mkoani Dodoma na tayari wamepata Dola 600,000 kutoka Serikali ya Korea kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na Julai 2024 wataanza ujenzi.

Nape amesema changamoto kubwa iliyopo sasa ni kukosekana kwa sera, sheria na kanuni zinazosimamia na kulea bunifu za kampuni changa licha ya kwamba kuna hatua kubwa imepigwa kwenye eneo hilo.

“Sasa tuko kwenye mchakato wa kutunga sera ya startups (kampuni changa) ambayo itatengeneza njia ya kupata sheria na kanuni zinazosimamia eneo hili,” amesema Waziri Nape.

Amesisitiza Serikali imejipanga kuwekeza kwenye rasilimali watu hasa vijana kwa kuwa tafiti zinaonyesha kwamba Afrika ndiyo bara litakalokuwa na vijana wengi duniani ukilinganishwa na mabara mengine, hivyo ni muhimu kuwekeza kwa vijana ili wanufaike na fursa hiyo kama nguvu kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kampuni Changa, Zahoro Muhaji amesema wamejifunza mengi kutoka Korea Kusini ikiwamo namna Serikali inavyowasaidia katika kuendelea bunifu zao.

Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo, Muhaji amesema ni kukosekana kwa sera, sheria na kanuni zinazosimamia wajasiriamali wachanga.

“Mitaji pia ni changamoto nyingine inayozikabili kampuni changa za wabunifu. Kupitia ziara hii, tumejifunza namna Korea wanavyokabiliana na changamoto hizi na kupiga hatua,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chama cha Kampuni Changa za Zanzibar, Iqra Ramadhan Soraga amesema wamefurahi kujifunza kutoka Korea kwa kuwa wamepiga hatua kubwa katika kulea bunifu za watu wao. Amesisitiza kwamba wanakwenda kutumia maarifa waliyoyapata kuinua bunifu za Wazanzibari.

Related Posts