Uchaguzi Afrika Kusini waiweka ANC njiapanda

Johannesburg. Uchaguzi wa Afrika Kusini ukiwa umekamilika baada ya kuchagua wabunge 400, kwa mara ya kwanza katika miaka 30 ya utawala wa kidemokrasia, hakijapatikana chama kinachoweza kuunda Serikali pake yake.

Mtihani mgumu upo kwa Chama tawala cha African National Congress (ANC) kilichopata asilimia asilimia 40.18, baada ya kunyakua viti 159 katika Bunge la Taifa, kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi (IEC).

Kwa uamuzi huo, Rais Cyril Ramaphosa wa African National Congress (ANC), anakosa udhibiti kamili wa hatima yake.

Chama kinachofuata ni Democratic Alliance (DA)  kilichipata asilimia 21.81, kikifuatiwa na uMkhoto we Sizwe (MK) (asilimia 14.58), Economic Freedom Fighters (EFF) (asilimia 9.52), huku vyama vingine vidogo vikikusanya jumla ya asilimia 13.91.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Afrika Kusini 2024 yalitangazwa Jumapili na Bunge jipya linapaswa kukutana si zaidi ya siku 14 baada ya hatua hii, katika tarehe itakayowekwa na jaji mkuu.

“Kikao chake cha kwanza baada ya uchaguzi, Bunge la Taifa lazima lichague mwanamke au mwanamume kutoka miongoni mwa wabunge wake kuwa Rais,” kulingana na Katiba.

Rais mteule ataacha kuwa mbunge katika Bunge lililoko Cape Town na lazima aapishwe ofisini ndani ya siku tano, baada ya hapo atateua Baraza la Mawaziri kumsaidia kuendesha Serikali Kuu huko Pretoria.

Katika chaguzi zilizopita, ANC ilikuwa ina urahisi wa kuchagua Rais na kumthibitisha, kwa sababu ilikuwa ikipata wabunge zaidi ya 200 (zaidi ya asilimia 50), lakini safari hii, mambo yamekuwa magumu.

Mwaka huu, Rais Ramaphosa au kiongozi mpya wa ANC atalazimika kutegemea wafuasi kutoka vyama vingine ili kuvuka kizingiti, ikimaanisha kuwa na muungano au makubaliano kuruhusu uundaji wa serikali ya wachache.

ANC ilifanya mkutano wa viongozi wake wa kitaifa Jumamosi iliyopita, ambapo walijadili uwezekano wa muungano na uwezekano wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Vyama kadhaa vya upinzani, hasa Democratic Alliance (DA) ya mrengo wa kulia na Inkatha Freedom Party (IFP) ya uzalendo wa Kizulu, vimeashiria kuwa tayari kujadili makubaliano ya kisiasa na ANC.

Kwa pamoja, viti 159 vya ANC na viti 87 vya DA tayari vinaongeza wingi kufikia unaotakiwa. Kuongeza viti 17 vya IFP kutaleta ahueni kubwa zaidi ikiwa baadhi ya wabunge wa chama tawala watakataa wazo la kufanya makubaliano na wapinzani wa melngo wa kulia.

Endapo ANC na DA zitaungana, hilo litakuwa linarejea historia ya mwaka 1994, ambapo Rais wa kwanza mweusi Nelson Mandela, aliongoza Serikali ya umoja wa kitaifa kutoka 1994 hadi 1997 akiwa Rais, huku FW De Klerk akiwa waziri mkuu wa mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi na naibu rais.

Viongozi wa Inkatha Freedom Party (IFP), walikuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri, Chief Mangosuthu Buthelezi akiwa waziri wa mambo ya ndani.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuna njia nyingine za kupata wingi viti vya Bunge, ambapo ANC inaweza kutafuta makubaliano na vyama vidogo.

Kwa mfano Patriotic Alliance ya mrengo wa kulia ina wabunge tisa na itazungumza na yeyote mwenye mamlaka, ikiwa atakubaliana kufukuza wahamiaji wasio na vibali. Vyama vingine 16 vina kati ya kiti kimoja na sita, na vinaweza kuunda muungano usio na usawa.

Kiitikadi, ANC ya kihistoria yenye mwelekeo wa kushoto inakaribiana zaidi na vyama viwili vinavyoongozwa na wanachama wa zamani wa safu zake za juu.

Kiongozi wa zamani wa vijana wa ANC, Julius Malema na EFF yake ina wabunge 39, kama ikikubali kushirikiana na ANC, itamwacha Ramaphosa akiwa na viti vitatu tu pungufu ya wingi unaotakiwa.

Lakini sera za mrengo wa kushoto za chama hicho – hasa ahadi ya kutaifisha biashara nyingi binafsi na ardhi – na historia ya Malema ya matamko ya vitisho anayotoa hadharani, vinatishia wapigakura wengi wa wastani na wazungu.

Chama cha tatu kwa ukubwa, MK cha Jacob Zuma, rais wa zamani wa ANC kimepata viti 58, lakini kimekataa matokeo ya uchaguzi na kutishia kususia Bunge.

MK pia imesema kwamba haitaiunga mkono Serikali inayoongozwa na ANC, ikiwa Ramaphosa atasalia madarakani.

Zaidi ya hayo, kiongozi mweupe wa DA John Steenhuisen anasema yuko tayari tu kwa mazungumzo na ANC ili kuzuia kile anachokiita “Muungano wa Siku ya Mwisho” wa ANC-MK-EFF ambao anasema ungeharibu katiba na uchumi.

Mazungumzo yatafanyikaje?

Maofisa kadhaa kutoka makundi pinzani wameliambia shirika la habari la AFP wakati wa kutangazwa kwa matokeo Jumapili usiku kwamba mazungumzo yasiyo rasmi kati ya viongozi wa vyama yameanza tayari.

DA na IFP zinasema zimechagua timu za uongozi kufanya mazungumzo rasmi.

Baraza Kuu la Utendaji la ANC linatarajiwa kukutana Jumanne kuamua kama litamshikilia Ramaphosa kama mgombea wake na kuweka mwelekeo wa mazungumzo.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa chama kinaweza kuelekea kwenye mpango wa “imani na ugawaji” ambapo DA na IFP zinakubali kumpigia kura Ramaphosa kama Rais na kuahidi kumuunga mkono katika kura za bajeti na kura za imani.

Lakini kunaweza kuwa na makubaliano juu ya muungano rasmi na wagombea wa zamani wa upinzani katika nafasi za utendaji na wizara.

Akizungumzia hali hiyo, mwanahabari mkongwe na mchambuzi wa siasa, Maggid Mjengwa anasema ANC imeingia kwenye mtihani mgumu.

“ANC iko njiapanda kwa sababu, ikiamua kwenda mrengo wa kushoto kwa MK na EFF itajikuta inapoteza imani kwa wawekezaji na ikiamua kwenda mrengo wa kulia kwa DA, huko nako inapoteza imani ya chama.

“Hapo ni sawa na kusema kuwa ANC imeangushwa na ANC, kwa sababu EFF imetoka hukohuko na MK imetoka hukohuko,” anasema.

Anasema mtanziko huo unatoa somo kwa kwa vyama vya siasa kudhibiti migogoro ya ndani.

“Ukifukuza watu wanaondoka na kura. Kama Malema na Zuma wasingefukuzwa ANC isingefika hapo ilipo,” anasema.

Mbali na vyama hivyo, Mjengwa anasema mambo makubwa matatu yaliyoiangusha ANC ni uhalifu, ukosefu wa ajira na ufisadi.

Akizungumza na Al Jazeera, mtaalamu wa sera za umma wa nchini Afrika Kusini, Kagiso “TK” Pooe, anasema Serikali ya umoja wa kitaifa inaweza kufanya kazi tu ikiwa itajengwa kwa malengo wazi ambayo vyama vyote vinaweza kukubaliana nayo.

“Miongoni mwayo muhimu itakuwa ni kurejesha wa uchumi wa Afrika Kusini na kukuza ajira. Pili, kudhibiti tatizo la ufisadi wa kitaasisi na kutokuwepo kwa ufanisi. Bila nia ya kujitolea kwa malengo kama hayo, muungano utaendelea kuwa katika hatari ya kushindwa na kuvunjika,” anasema.

Related Posts