Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ndogo ya Bukoba iliyoketi Karagwe, imemhukumu kifungo cha miaka 10 jela, Edson Aron baada ya kumkuta na hatia ya kumuua bila kukusudia Philemon Thadeo, kwa kumkata na panga kichwani na mkononi.
Edson alimuua Thadeo baada ya kutokea kutokuelewana katika mazungumzo yao na kusababisha mapigano kati yao.
Imeelezwa kuwa, Thadeo alikuwa akimdai mshitakiwa fedha alizompa kwa ajili ya kununulia mtama.
Tukio hilo lilitokea Julai 7, 2022 katika Kijiji cha Chamchuzi, Kata ya Bweranyange, wilayani Karagwe mkoani Kagera.
Katika kesi hiyo ya mauaji namba 89/2023, mtuhumiwa huyo alikiri kosa katika maelezo yake ya onyo aliyoyatoa polisi.
Ukurasa wa tatu wa maelezo hayo imenukuliwa mshitakiwa akisema, “nilipofika akasema kwamba tuanze kuhesabiana pesa anazonidai akaniambia nimpatie magunia yake matatu ya mtama ili tuache kudaiana.”
“Nami nikamwambia kwa sababu namdai 140,000, hivyo nimlipe gunia moja yeye akakataa kisha akanishika na kunikwida na kunipiga ngwala nikaanguka pia akanipiga ngumi. Nikashindwa kuvumilia na kuchukua panga langu kisha kumkata nalo kichwani…”
Akisoma hukumu hiyo Mei 31, 2024, Jaji Immaculate Banzi, alisema Edson alishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alisema Mahakama imebaini mshitakiwa aliua bila kukusudia.
Hivyo, kwa kuzingatia ushahidi hakuna ubishi kuwa marehemu amekufa kifo kisicho cha kawaida na ilibainika alikuwa na jeraha kichwani.
“Ni jambo lisilopingika kwamba, maisha ya marehemu yalipotea jambo ambalo kwa mujibu wa Katiba yetu, mtuhumiwa alikuwa na wajibu wa kulinda, hakukuwa na sababu ya msingi kwa mtuhumiwa kutumia silaha hiyo hatari katika mapambano yao huku marehemu akitumia teke na ngumi.”
“Mbali na hilo, hakuchukua hatua yoyote ya kumsaidia baada ya kumsababishia majeraha hayo ambayo ingeonyesha kujutia. Hata hivyo, kwa kuwa yeye ndiye mkosaji wa kwanza na tayari alikuwa ameshakaa rumande miaka miwili, ninamhukumu kifungo cha miaka 10,” amesema Jaji Immaculate.
Katika kesi hiyo upande wa jamhuri ulikuwa na mashahidi wanane na vielelezo vinne huku mshitakiwa huyo akijitetea chini ya kiapo, ilidaiwa siku ya tukio saa mbili asubuhi, Thadeo alipigiwa simu na mshitakiwa akimtaka aende aliko kumsaidia ng’ombe wake mgonjwa.
Ilidaiwa kuwa marehemu alimpeleka mkewe kwa pikipiki nyumbani kisha akapitia Kituo cha Chamchuzi ambako aliwajulisha rafiki zake akiwamo shahidi wa pili kuwa anakwenda kukutana na mshitakiwa.
Kwa mujibu wa kielelezo cha pili na tatu ambayo ni maelezo ya onyo ya Edson, watu hao walipokutana waliadili kuhusu pesa ambazo Thadeo alimpa mshitakiwa kumnunulia mtama na kukazuka kutokuelewana na mapigano kati yao.
Shahidi wa kwanza na pili walidai siku ya tukio marehemu alienda kukutana na mshitakiwa na baada ya marehemu kupita katika Kituo cha Chamchuzi akielekea kukutana na mshtakiwa, dakika 15 baadaye, alionekana akiwa amebebwa kwenye pikipiki akiwa na majeraha kichwani.
Shahidi wa tatu alidai alipokuwa katika kituo cha bodaboda, alimuona Thadeo akiwa na majeraha na kumpeleka hospitali na alipoulizwa, Thadeo alimtaja mshitakiwa kuwa ndiye aliyemshambulia.
Aidha, Mahakama ilijiridhisha ni kweli hakuna shahidi wa jamhuri aliyeshuhudia tukio hilo ila uliegemea mshitakiwa alivyokiri polisi.
Jaji alieleza katika maelezo yote mawili, mshtakiwa alikiri kumkata marehemu kichwani na mkononi kwa kutumia panga huku akinukuu mashauri mbalimbali yaliyotolewa maamuzi yakieleza.
“Ungamo au maelezo yatachukuliwa kuwa yametolewa kwa hiari hadi pingamizi dhidi yake litakapotolewa na upande wa utetezi, ama kwamba halikufanywa kwa hiari au halikufanywa kabisa.”
Jaji aliendelea kunukuu katika kesi ya Paulo Maduka na wengine dhidi ya Jamhuri (2009), ikielezwa kuwa, “…ushahidi bora katika kesi ya jinai ni kukiri kwa hiari kutoka kwa mtuhumiwa mwenyewe.”
“Ingawa mtuhumiwa alijitenga na madai ya uhalifu, kwa mtazamo wangu nilionao, utetezi wake haujaleta shaka yoyote dhidi ya ushahidi wa mashitaka kuhusiana na uhusika wake,ukiangalia kwa makini utetezi wake, japo hakukata kuwepo kijijini Chamchuzi ,alikana kuwepo eneo la tukio,”alieleza Jaji
“Ikiwa hakuwepo eneo la uhalifu, ilitarajiwa kuibuliwa wakati wa kutoa ushahidi wa shahidi wa kwanza na pili, ambao waliieleza Mahakama jinsi walivyoagana na marehemu aliyeenda kuonana na mshtakiwa na muda mfupi baadaye, alirejea na majeraha na kumtaja mshitakiwa ndye amemshambulia.”
Jaji alieleza mshtakiwa kupitia kwa wakili wake hakuwachunguza katika kipengele hicho na ni kanuni iliyowekwa kwamba, kushindwa kumhoji shahidi kwenye jambo husika kwa kawaida humaanisha kukubalika kwa ukweli wa ushahidi.
“Mtuhumiwa alidai hakusikia tukio la kushambuliwa na kuuawa kwa marehemu (Thadeo). Inaweza kukumbukwa kwamba, hakukuwa na kupingwa ushahidi kutoka kwa shahidi wa kwanza na pili kuhusu mtuhumiwa kuwa jirani na marehemu,”alieleza.
“Ikiwa madai ya mtuhumiwa yalikuwa ya kweli,vipi anasema hakusikia tukio hilo hadi kesho yake wakiwa na majirani? Mbali na hilo, katika maungamo yake yote mawili, alieleza kwa kina jinsi alivyokutana na marehemu na kubishana kuhusu fedha alizopewa kumnunulia mtama.
“Pia, alieleza jinsi kutoelewana kulivyozuka katika mazungumzo yao na kusababisha mapigano kati yao, hali iliyosababisha mtuhumiwa kumshambulia marehemu(Thadeo). Ingawa katika utetezi wake alijaribu kukataa maelezo yake ya ziada ya mahakama,”aliongeza Jaji.
Amesema kwa kuzingatia hayo ni kwa maoni yake kwamba, ushahidi wa upande wa utetezi ulikuwa wa kufikirika na hauleti shaka yoyote juu ya kesi ya upande wa mashtaka na ni mtazamo thabiti wa Mahakama hiyo kuwa mshitakiwa ndiye aliyemsababishia majeraha marehemu ambayo ndiyo chanzo cha kifo cha marehemu.
Suala lingine Mahakama hiyo ililolizingatia ni endapo mtuhumiwa alimuua Thadeo kimakusudi na kuwa ni kweli kwamba ubaya uliofikiriwa hapo awali, unaweza kuanzishwa kwa sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na aina ya silaha iliyotumika katika shambulio hilo.
Nyingine ni kiasi cha nguvu kutumika katika shambulio hilo, sehemu au sehemu za mwili pigo zilielekezwa, idadi ya mapigo, aina ya majeraha , matamshi ya washambuliaji, ikiwa wapo, walifanya kabla, wakati au baada ya mauaji na tabia ya mshambuliaji kabla na baada ya mauaji.
Akitoa ushahidi wake mahakamani hapo, mshitakiwa huyo alidai kuwa siku ya tukio, aliamka na kwenda katika duka lake analouza sukari, mchele, petroli na bidhaa nyinginezo, na alikaa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 8:30 mchana na kurudi nyumbani kwake.
Alidai siku iliyofuata alikwenda Nyakaiga kununua bidhaa za dukani kwake na wakati akisubiri usafiri wa umma kutoka Omurushaka hadi Chamchuzi, aliamua kwenda Chabalisa kumtembelea dada yake, Leokardia Aron.
Alidai kuwa alipofika Kijiji cha Chabalisa, alikutana na dada yake mwingine na baada ya hapo, akiwa eneo la Akadipii, alikamatwa akihusishwa na kifo hicho na kudai kupelekwa Kituo cha Polisi Chabalisa na baadaye kituo cha Nyakaiga.
Alidai akiwa kituoni hapo alipigwa na shahidi wa sita, G.7525 D/Koplo Emmanuel, akiwa na wenzake na kumlazimisha kusaini maelezo hati iliyoandikwa bila kujua kilichokuwa kimeandikwa na baadaye kurudishwa Kituo cha Polisi Nyakaiga.
Alieleza kuwa baada ya hapo, alihamishiwa kituo cha polisi cha Kayanga ambako alikaa hadi Julai 15, 2022 alipofikishwa mahakamani Julai 19, 2022 na alikana kuhusika na mauaji hayo na kudai ushahidi wa upande wa mashitaka ulikuwa wa uongo.