Tathmini ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalofanya uchunguzi kwa kutumia Satelati (UNOSAT) imeonyesha zaidi ya majengo 137,000 yameathirika huko Gaza. Makadirio hayo yanatokana na picha za satelaiti zilizopigwa Mei 3. Na ilikingalinishwa na picha zilizopigwa mwaka mmoja kabla ya shambulizi la Hamas la Oktoba 7 nchini Israel. Takwimu hizo zinalingana na karibu asilimia 55 ya jumla ya miundombinu katika Ukanda wa Gaza. Shirika la UNOSAT limesema picha zimeonyesha kuwa majimbo ya Deir Al-Balah katikati mwa Palestina na Gaza huko kaskazini ndiyo yalioathirika zaidi.
Shirika hilo limesisitiza kuwa matokeo hayo bado ni sehemu ya uchambuzi wa awali, ambao ulikuwa bado haujathibitishwa katika eneo la tukio.
Hata hivyo bado Israel inaendelea na mashambulizi yake huko Gaza. Kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza, takriban watu 40 wameuawa katika muda wa saa 24 zilizopita. Usiku wa kumakia Jumatatu (03.06.2024), Israel pia ilishambulia kiwanda karibu na Aleppo nchini Syria na kuua wapiganaji wasiopungua kumi na wawili wanaoiunga mkono Iran kutoka Syria na mataifa ya kigeni.
Misri yawataka wanajeshi wa Israel kuondoka kwenye mpaka wa Rafah
Waziri wa mambo ya nje wa Misri Sameh Shoukry amesema zoezi la usambazaji misaada Gaza halitoendelea tena hadi hapo Israel itaondoka kwenye kivuko cha mpakani cha Rafah na kurejesha udhibiti wake chini ya utawala wa viongozi wa Palestina.
“Kuna msimamo na sera ya wazi ya Wamisri ya kukataa uwepo wa Israeli katika kivuko cha Rafah. Kivuko cha Rafah ndicho kiunganishi pekee cha uhusiano kati ya Wapalestina na ulimwengu wa nje. Vivuko vilivyosalia vya Israel vimefungwa kwa Wapalestina na harakati za Wapalestina kwa ajili ya mahitaji ya elimu au matibabu yamepitia Misri kutoka zamani.”, alisema Shoukry.
Kabla ya kuongeza : “Ni vigumu kwa kivuko cha Rafah kuendelea kufanya kazi bila utawala wa Wapalestina kwa upande wa Palestina na ni jambo la kawaida kwamba hii itakuwa sehemu ya suluhisho lolote la hali ya sasa.”
Shinikizo dhidi ya Netanyahu
Jumatatu vyombo vya habari vya Israel vilimnukuu waziri mkuu Benjamin Netanyahu akisema awamu ya kwanza ya mpango wa amani unaoungwa mkono na Marekani wa kuachiwa huru mateka unaweza kutekelezwa bila usitishwaji kamili wa mapigano.
Netanyahu aliongeza kwamba kipaumbele cha juu cha Israeli huko Gaza ni kulisambaratisha kundi la Hamas. Serikali ya Israel imehisi kuwa mpango wa amani wa Marekani haujakamilika.
Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya mawaziri wake ambao wanatishia kujiuzulu endapo mpango wa usitishwaji mapigano utatekelezwa.