Dar es Salaam. Wakala wa Taifa wa Barabara Tanzania (Tanroads) imesema upanuzi unaoendelea wa sehemu ya barabara ya Morogoro kutoka Ubungo hadi Kimara-Mwisho jijini Dar es Salaam hautahusisha ubomoaji wa mali za watu.
Ujenzi wa sehemu hiyo ni sehemu ya upanuzi wa barabara yote inayounganisha Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam kwa kuibadilisha kuwa barabara yenye njia nane (ikijumuisha mbili kwa ajili ya Mabasi yaendayo Haraka – BRT).
Ujenzi halisi wa sehemu ya barabara ulianza miaka michache iliyopita ambapo majengo na miundo kadhaa, ikiwa ni pamoja na vituo vya afya, makanisa na misikiti, vilibomolewa kati ya Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam na Kibaha mkoani Pwani.
Lakini sasa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta, aliiambia The Citizen jana kwamba hakuna ubomoaji utakaofanyika wakati upanuzi unaingia awamu nyingine.
The Citizen limeshuhudia shughuli kama usafishaji eneo kando ya barabara kuu, ikijumuisha kukata miti na kuchimba baadhi ya maeneo kutoka Kimara-Mwisho hadi Ubungo.
“Hakutakuwa na ubomoaji wowote kwani shughuli hiyo tayari ilifanyika hapo awali,” amesema Besta.
Mradi unatekelezwa chini ya Mpango wa Uboreshaji wa Usafiri Dar es Salaam (DUTP).
Serikali, kupitia Tanroads, ilisaini mkataba wa upanuzi wa barabara hiyo na Sichuan Road and Bridge Group Corporation Ltd Novemba, 2023.
Kazi inatarajiwa kukamilika Mei 2025.
“Maendeleo ya kazi za zilizofanyika hadi sasa ni asilimia mbili na mradi unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa kwa gharama ya Sh83.8 bilioni,” alisema Besta.
Amesema malipo ya awali yalilipwa kikamilifu tangu Desemba mwaka jana yakifikia Sh12.2 bilioni.
Miongoni mwa shughuli zinazoendelea ni pamoja na kumalizia usafi kwa asilimia 100 kwenye eneo la mradi.
“Pia kuna kusafisha na kuondoa magugu, maandalizi ya kitanda cha barabara, ujenzi kwenye sehemu za kujaza, ujenzi wa kuta za kuzuia, na kutambua vikwazo,” amesema.
Amesema kila upande wa barabara una nafasi ya kutosha kwa ajili ya kufanikisha kazi ya upanuzi kwa haraka na ufanisi.
Kutokana na ongezeko la idadi ya magari yanayotumia barabara hiyo, Tanroads inaamini kulikuwa na haja ya haraka ya kuipanua.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na The Citizen jana wamesema, ni jambo la kutia moyo kuwa shughuli hiyo itafanyika bila ubomoaji.
“Nilisikia kuhusu upanuzi wa barabara hii muda mrefu uliopita, na ilifadhiliwa na Benki ya Dunia. Mwaka huu, waliamua kuendelea, na tuliambiwa kwamba hakutakuwa na kubomolewa kwa nyumba zetu. Hili ni jambo jema kweli,” amesema Atanasi Mkenda, mkazi wa Kimara-Mwisho.
Mtumiaji wa mara kwa mara wa barabara hiyo, Sarah Ombeni, amesema foleni za asubuhi na jioni zimekuwa changamoto kubwa, na kusababisha madereva kutumia muda mrefu barabarani kutokana na ufinyu wa barabara.
Amebainisha kuwa jinsi Dar es Salaam inavyokua, idadi ya watu pia inaongezeka; barabara hiyo ni lango kuu la Tanzania, hivyo kusababisha wingi mkubwa wa magari, malori, na pikipiki za magurudumu matatu.
“Katika miaka mitatu iliyopita, bajaj chache tu zilikuwa zikiendeshwa barabarani, lakini idadi yao imeongezeka, hivyo kuchangia msongamano. Naishukuru Serikali kwa uamuzi wake kwa sababu utarahisisha usafiri kutoka Kimara-Mwisho hadi Kibaha,” amesema.
Dereva wa bajaj, Nasri Abdalah, amesema barabara hiyo ina shughuli nyingi kila wakati.
‘’Kuboresha barabara ni muhimu, lakini jambo muhimu zaidi ni kwamba nyumba za watu hazitavunjwa,’’amesema.