Wataalamu elimu kujifunza teknolojia mpya

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha mpango wa kuwa na mkondo wa elimu ya amali kwa shule za sekondari na vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi unatekelezeka, Tanzania imeweka mkakati wa kuimarisha uhusiano na mataifa yaliyoendelea kwenye teknolojia.

Hatua hiyo itawezesha watalaamu wa ndani kujifunza teknolojia mpya zinazotumika kwenye elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na kuweza kupenya kwenye soko.

Hayo yameelezwa leo Juni 3, 2024 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Profesa James Mdoe wakati akifungua semina iliyovikutanisha vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi vya Tanzania na China ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa mataifa hayo.

Amebainisha kuwa msingi mkubwa katika mapitio ya sera ya elimu yaliyofanyika mwaka jana ni ujuzi, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mikakati ya kutengeneza rasilimali watu watakaowezesha utekelezaji wa mkondo wa amali.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ujuzi watakaopata wahitimu wa vyuo vya ufundi na shule za elimu ya amali unakuwa wa hali ya juu ukijiegemeza katika teknolojia ya kisasa

“Tunajenga vyuo vya Veta katika wilaya 64 kazi ya ujenzi inaendelea na kama ambavyo bajeti ya wizara inavyoeleza kuna shule 100 za mkondo wa amali zitaanza kujengwa kuanzia Julai mwaka huu.

“Huku kote kutahitaji walimu na wakufunzi, changamoto tuliyonayo bado hatunao wa kutosha hivyo ushirikiano wa namna hii na nchi zilizoendelea katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ni kitu tunachopaswa kukiwekea mkazo ili tupate ujuzi wa kisasa ambao tutauleta kwenye vyuo na shule zetu,” amesema Profesa Mdoe.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dk Adolf Rutayuga amesema semina hiyo imehusisha vyuo 40 vya China na 40 vya Tanzania ambavyo vyote kwa pamoja vinaangalia maeneo ya ushirikiano.

Ametaja maeneo ambayo vyuo hivyo yatashirikiana ni ufanyaji tafiti, vifaa na mbinu vya kufundishia, teknolojia.

 “Kwa sababu wenzetu wamepiga hatua kwenye mambo ya teknolojia, tunatarajia ushirikiano huu utakuwa na manufaa zaidi kwetu.Tunataka kuwajengea vijana ujuzi ambao unaendana na hali ya sasa sio tu ujuzi ili mradi ujuzi,” amesema Dk Rutayuga.

Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza hilo Beradetta Ndunguru amesema semina hiyo ni muhimu katika kutengeneza mfumo utakaowezesha vijana wanaosoma kwenye vyuo vya ufundi kupata ujuzi wanaoweza kuutumia kujiajiri.

Amesema, “Tuna tatizo kubwa la ajira, sasa ajira haziwezi kupatikana bila kuwa na stadi za kazi, ujuzi na elimu ya ufundi, wenzetu wako mbali kwenye eneo la ujuzi hivyo tuna mengi ya kujifunza kutoka kwao na ifike wakati tujiwekee lengo la kila Mtanzania kuwa na ujuzi ambao anaweza kuutumia kujiajiri au kuajirika,” amesema.

Related Posts