Dar es Salaam. Mshtakiwa Fadhil Athuman na wenzake wawili, wameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwabadilishia shtaka la mauaji linalowakabili liwe shtaka la mauaji bila kukusudia.
Ombi hilo limetolewa leo Jumatatu, Juni 3, 2024 kupitia wakili wao, Hassan Kiangio wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo yaani ‘Committal Proceedings’.
Kiangio ametoa ombi hilo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya anayesikiliza shauri hilo.
Kiangio amedai kuwa, baada ya kupitia vijalada vya kesi hiyo, ameona kuna chembechembe za kosa la mauaji ya bila kukusudia hivyo kama itawapendeza upande wa mashata wapitie jalada na kuona namna ya kuwabadilishia washtakiwa shtaka hilo.
Akijibu ombi hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga aliomba Mahakama iwape wiki moja ili aende kifanya majadiliano na uongozi wa juu ili waweze kuona kama watabadilisha hati hiyo au la.
“Mheshimiwa hakimu, nimeyasikia maombi ya upande wa utetezi, hivyo tunaomba Mahakama itupe siku saba ili tuweze kufanya mashauriano na uongozi wangu ili tuweze kuona kama washtakiwa hawa watabadilishiwa mashtaka au laa,” alidia wakili Mwanga.
Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Juni 10, 2024 na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalowakabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Mbali na Athuman, washtakiwa wengine ni Fadhili Mikidadi na Karim Hassan.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, Machi 13, 2023 eneo la Tip top, Manzese, Wilaya ya Kinondoni.
Siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kumuua, Mwinyi Kingwa.