Mauzinde akatwa masikio na kutelekezwa msituni

Unguja. Hussein Abdala (30) maarufu Mauzinde mkazi wa Rahaleo Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar amekatwa masikio yote mawili na kutelekezwa msituni.

Tukio hilo limetokea  jana Jumapili Juni 2, 2024 saa 3 usiku eneo la Kibele Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo Juni 3, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Daniel Shila amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema atalitolea maelezo zaidi baadaye.

Shila amesema yupo kwenye msafara wa viongozi hivyo hawezi kuzungumza zaidi kuhusu tukio hilo.

“Kweli tukio hilo lipo, ila nitalitolea zaidi ufafanuzi baadaye kwa sasa nipo kwenye msafara wa viongozi,” amesema Kamanda Shila.

Baada ya kukatwa masikio, Mauzinde alifungwa bandeji kichwani na kutelekezwa kwenye msitu wa hifadhi wa Kibele.

Hata hivyo, sababu za kukatwa masikio, bado hazijajulikana.

Majeruhi amepelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwera, Pongwe na kupatiwa Rufaa kwenda hospitali ya Mnazi Mmoja kwa matibabu zaidi.

Related Posts