Chongolo aagiza mzee aliyeporwa ardhi arejeshewe

Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ameuaguza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe kumrejeshea ekari 18 Wendisoni Sasala ambazo ziliongezwa kutoka ekari 50 alizotoa bure kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Itindi na kufikia ekari 68 bila ridhaa yake.

Mzee Sasala ametoa malalamiko hayo jana jioni Juni 4, 2024 mbele ya mkuu huyo wa mkoa alipofika kijijini hapo kusikiliza kero za wananchi.

Amesema eneo hilo alilitoa mwaka 1982 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo baada ya kijiji kukosa eneo la kuijenga.

Sasala amesema anasikitika kuona eneo lake lililobaki la ekari 18, nalo limechukuliwa na Serikali bila ridhaa yake wakati ardhi hiyo alikuwa anaitumia kwa kilimo.

“Mwaka 1982 kijiji kilitaka kujenga shule, lakini eneo halikuwepo, nikaamua kujitolea ekari 50 bila fidia na shule imejengwa, lakini cha kushangaza hata ekari 18 nilizojibakizia  zimechukuliwa tena, naomba mkuu wa mkoa nisaidie nirejeshewe eneo hilo kwa manufaa yangu,” amesema Sasala.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasahuri ya Songwe, Cecilia Kavishe amekiri mzee huyo kutoa ekari 50 miaka ya 1982 na kuwa kupitia ofisi ya ardhi ya halmashauri hiyo watahakikisha mzee huyo anarejeshewa eneo lake.

Pia amekiri ekari hizo 18 kuchukuliwa na shule ya Itindi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songwe, Ibrahimu Sambila amesema busara haijatumika kupoka ardhi ya mtu ambaye amesaidia kupatikana kwa eneo la shule bila malipo.

“Inasikitisha kuona mzee huyu ananyang’anywa ekari 18, naomba nikuahidi mkuu wa mkoa kwamba nitasimamia mchakato mzima mpaka mzee apewe ekari zake 18 kwa ajili ya kujiendeleza kwenye kilimo,” amesema Sambila.

Akitoa maelekezo kwa uongozi wa halmashauri hiyo, Chongolo amemhakikishia Sasila kuwa atatendewa haki.

“Kama nilivyosema mwenyekiti wa halmashauri utasimamia zoezi hili na ripoti utampelekea mkuu wa wilaya ambaye ataleta kwangu na mzee atafurahia kwa sababu serikali ya awamu ya sita na viongozi wa Mkoa wa Songwe wapo kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi,” amesema Chongolo.

Related Posts