Kijiji chapata maji safi na salama kwa mara ya kwanza tangu Uhuru

Adha ya upatikanaji wa maji safi na salama, iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Kijiji cha Mherule, kata ya Mwanya Tarafa ya Mang’ula wilayani Kilombero mkoani Morogoro, imebaki historia baada ya serikali kutekeleza mradi wa maji safi na salama ya kunywa kijijini hapo. Anaripoti Victor Makinda, Morogoro…(endelea).

Wakizungumza na MwanaHALISI Online wananchi wa kijiji hicho wamesema ujio wa mradi huo licha ya kuwatua ndoo kichwani akina mama, pia utawaepushia magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakiwapata kutokana na kutumia maji yasiyo safi na salama.

Meneja wa RUWASA wilaya ya Kilombero, Mhandisi Frorence Mlelwa.

Shamsia Seleman, mwananchi wa kijiji hicho akizungumza kwa niaba ya wenzake anasema kuwa awali hapakuwa na  maji safi na salama kijijini hapo ambapo walikuwa wanakunywa maji kutoka kwenye mabwawa  na vidimbwi yaliyokuwa yakiwasababishia magonjwa ya mlipuko ya tumbo ya mara kwa mara.

“Tunamshuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kututua ndoo kichwani sisi wananchi wa Mherule kwani tulikuwa tunapata shida kubwa ya maji na magonjwa ya tumbo ya mara kwa mara,” amesema.

Amesema kuwa uwepo wa mradi huo kijijini hapo utawapa muda wa kutosha kufanya shughuli za maendeleo kwa kuwa awali walikuwa wakitumia muda mrefu kutafuta maji.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mherule, Mustapha Chapchap anasema kuwa kijiji hicho chenye wakazi 2400 hakijawahi kupata huduma ya maji safi na salama ya bomba tangu Tanganyika ipate uhuru mwaka 1961, hivyo anaishukru serikali ya awamu ya sita kusikia kilio chao na kuwapelekea mradi wa maji safi na salama.

Aidha, Meneja wa RUWASA wilaya ya Kilombero, Mhandisi Frorence Mlelwa, amesema jumla ya Sh 542.9 milioni zimetumika kutekeleza mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 85 ambapo unatarajiwa kukabidhiwa rasmi Octaba mwaka huu ukiwa tayari umeanza kunufaisha wananchi.

“Ruwasa Kilombero, tumetekeleza ujenzi wa mradi wa maji safi na salama kijiji cha Mherule, ambao umehusisha  uchimbaji wa kisima kirefu, uwekaji wa pampu ya umeme,ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo kuihifadhi lita 100, 000  sambamba na vituo vya kuchotea maji (DP) 8 vinavyotoa maji safi na salama ambayo mwananchi haitaji kuyachemsha kabla ya kunywa,” amesema Mhandisi Mlelwa.

Ameongeza kuwa vituo vyote vya kuchotea maji vimewekewa mfumo wa malipo ya kabla kwa kutumia mfumo wa   kadi janja (smart card).

Related Posts