Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi kwa Rais mteule wa Mexico Claudia Sheinbaum baada ya kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, uliofanyika Jumapili ya Juni 2, 2024.
Rais Samia ametoa pongezi hizo kupitia ukurasa wake wa X leo Juni 4, 2024 akimtakia kila la kheri katika uongozi wake.
“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Claudia Sheinbaum, Rais Mteule wa Mexico, kwa ushindi wako wa kihistoria katika uchaguzi mkuu wa 2024 nchini Mexico. Mheshimiwa Rais Mteule, nakutakia kila la kheri,” ameandika Rais Samia.
Mexico inaingia katika historia kwa mara ya kwanza kupata Rais mwanamke kama ilivyo kwa Tanzania. Sheinbaum, meya wa zamani wa Mexico amepata kura kati ya asilimia 58.3 na 60.7, kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Uchaguzi ya Mexico, (INE).
Katika kinyang’anyiro hicho, kulikuwa na wagombea wawili wanawake waliokuwa wakichuana vikali ambao ni Sheinbaum aliyechaguliwa sambamba na mpinzani wake Xóchitl Gálvez.
Gálvez ambaye anaongoza muungano wa vyama vingi vya kihafidhina, amepata kati ya asilimia 26.6 hadi 28.8, ingawa matokeo rasmi yatatangazwa Juni 8, 2024.
Inaelezwa asilimia alizopata Sheinbaum ni 30 mbele ya mpinzani wake Gálvez na asilimia 50 mbele ya mgombea mwingine Jorge Alvarez. Galvez amekubali kushindwa baada ya matokeo haya ya awali.
Ifikapo Oktoba, Sheinbaum mwenye umri wa miaka 61 atachukua nafasi ya Rais Andres Manuel Lopez Obrador.
“Nataka kuwashukuru mamilioni ya wanawake na wanaume wa Mexico walioamua kutupigia kura katika siku hii ya kihistoria. Sitawaangusha,” Sheinbaum ameuambia umati uliokuwa ukishangilia.
Vilevile amemshukuru mpinzani wake mkuu Galvez kwa kukubali kushindwa.
Mbali ya kushinda urais lakini chama cha Morena kimeshinda pia umeya wa Mexico City, mojawapo ya nyadhifa muhimu zaidi nchini humo.
Katika uchaguzi huo takriban watu milioni 100 walijiandikisha kupiga kura kwenye nchi hiyo yenye watu zaidi ya milioni 120.
Katika kampeni zake Sheinbaum ameahidi kuendeleza mkakati wa Rais anayemaliza muda wake wa kukabiliana na uhalifu ulioota mizizi nchini humo.
Pamoja na kuchagua Rais mpya, wananchi wa Mexico waliwapigia kura wajumbe wa Congress, magavana kadhaa wa majimbo na maelfu ya maofisa wa Serikali za mitaa, jumla ya nyadhifa zaidi ya 20,000.