SERIKALI imeanza kuichunguza Taasisi ya Athuman Kapuya, dhidi ya tuhuma za usambazaji ushoga inazoikabili shirika hilo lisilo la kiserikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa ya uchunguzi huo imetolewa Leo tarehe 4 Juni 2024 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, ikiwa ni siku Moja tangu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, kuifungia Taasisi hiyo baada ya kudaiwa kusambaza vitabu na bidhaa nyingine zinazotumiwa na watu wanaofanya mapenzi ya Jinsia Moja hususan ushoga.
Kupitia taarifa yake, Dk. Gwajima amesema uchunguzi huo unafanyika ili kubaini ukweli wa madai hayo na ikithibitika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa Taasisi husika kwa kosa la kukiuka Sheria, mila na desturi za Tanzania.
“Kutokana na upungufu huo, ofisi ya msajili kupitia bodi ya uratibu wa mashirika hayo imesimamisha utendaji kazi wa shirika hilo kote nchini ili kupisha uchunguzi na hatua zaidi. Baada ya uchunguzi kukamilika wahusika watachukiliwa hatua zote stahiki kwa mujibu wa Sheria,” imesema taarifa ya Dk. Gwajima.