NBC yanogesha Derby Kariakoo, Aziz Ki aibuka mchezaji bora Machi

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambayo ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premiere League juzi Jumamosi ilinogesha shangwe za mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga kwa kuwapeleka uwanja wa Benjamin Mkapa wateja wake ili kushuhudia mtanange huo ulioisha kwa timu ya Yanga SC kuibuka na ushindi wa 2-1. Benki hiyo pia ilikabidhi zawadi kwa mchezaji wa Yanga Azizi Ki ambae aliibuka mchezaji bora wa ligi hiyo mwezi Machi. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Elvis Ndunguru (kulia) akiwaongoza wageni waalikwa ambao ni wateja wa benki hiyo pamoja na maofisa wa benki kupata chakula cha mchana kwenye Hoteli ya Hyatt the Kilimanjaro jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea uwanja wa Benjamin Mkapa kutazama mechi kati ya Simba na Yanga kwa ufadhili wa benki hiyo.

Jijini Dar es Salaam sehemu maalum zilizoandaliwa na benki hiyo kwa ajili ya kutazama mchezo huo ni ‘Restaurants’ za Samaki Samaki zilizopo maeneo ya Mlimani City na Masaki, pia restaurant ya Uvuvi Kempu pamoja na restaurant ya Hoppipola iliyopo Masaki.

Wakizungumza kwenye hafla fupi ya chakula cha mchana na wateja wa benki hiyo kwenye Hoteli ya Hyatt the Kilimanjaro kabla ya kuwapeleka mashabiki hao uwanjani, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Benki ya NBC, Elibariki Masuke na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Elvis Ndunguru walisema hatua hiyo ni mwendelezo wa utaratibu wa benki hiyo kutumia mechi hizo maarufu kama ‘Derby ya Kariakoo’ kuandaa matukio kama hayo ili kutoa fursa kwao kufurahia ladha ya ligi hiyo inayoendelea kujiongezea umaarufu barani Afrika kufuatia udhamini mnono uliofanywa na benki hiyo.

Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Benki ya NBC, Elibariki Masuke (wa pili kushoto) akitazama baadhi ya zawadi zikiwemo jezi zinazotolewa na benki hiyo kwa wateja wake wakati wa hafla ya chakula cha mchana kwenye Hoteli ya Hyatt the Kilimanjaro jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekea uwanja wa Benjamin Mkapa kutazama mechi kati ya Simba na Yanga kwa ufadhili wa benki hiyo.

“Umekuwa ni utaratibu wetu sasa kufurahia na wateja wetu kwenye kila mechi ya ligi kuu ya NBC kuanzia Dar es Salaam hadi mikoani kwa kutoa zawadi mbalimbali zikiwemo tiketi za bure kwa baadhi wateja kwa kuzingatia vigezo tofauti.

“Kwa kutambua uzito wa mechi hii huwa tunaitumia kama siku maalum kufurahia pamoja na wateja wetu kwa kuwaandalia chakula cha mchana, kutoa fursa kwa wao kufahamiana, kubadilishana mawazo yakiwemo ya kibiashara pamoja na kuwakumbusha kuhusu huduma zetu mbalimbali kisha pamoja tunaelekea uwanjani tukiwa kwenye msafara maalum kushuhudia pamoja mechi hiyo,’’ alibainisha Ndunguru.

Zaidi Ndunguru aliongeza kuwa benki hiyo imejipanga zaidi kuendelea kuihudumia ligi hiyo kupitia huduma zake mbalimbali mahususi kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo pamoja na ligi Daraja la Kwanza (NBC Championship) na Ligi ya Vijana (NBC Youth League) ambazo zote zinadhaminiwa na benki hiyo.

“Kwenye hili tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kutoa mikopo ya usafiri kwa timu zinazoshiriki ligi kuu kwa masharti nafuu, tunaendelea kutoa huduma za bima za afya kwa wachezaji na mabechi ya ufundi na mikopo mbalimbali kwa kuzingatia vigezo na masharti,’’ aliongeza.

Mbali na matukio hayo pia wateja hao walipata fursa ya kupata huduma mbalimbali za kifedha kutoka benki ya NBC kupitia maofisa wa benki hiyo waliokuwa wakitoa huduma mbalimbali ikiwemo kufungua akaunti pamoja na kufanya mihamala ya kifedha wakiwa maeneo hayo pamoja na viunga vya Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Related Posts