Wagombea uongozi Chadema Kaskazini kufanyiwa usaili

Babati. Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini waliochukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa majimbo, watafanyiwa usaili kabla ya kupitishwa kuwania nafasi hizo.

 Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Juni 4, 2024 na ofisa habari na mawasiliano wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Mozee Joseph imesema usaili kwa Tanga mjini utafanyika Juni 7, 2024 na uchaguzi utafanyika Juni 9, 2024.

Amesema jimbo la Moshi mjini usaili utafanyika Juni 8 na uchaguzi utakuwa Juni 10 huku jimbo la Hai usaili utafanyika Juni 10 na uchaguzi ni Juni 12, 2024.

“Jimbo la Arusha mjini usaili utafanyika Juni 11 na uchaguzi Juni 14, na Babati mjini mkoani Manyara Juni 13 na uchaguzi utakuwa Juni 15, mwaka huu,” amesema Joseph.

Amesema wanachama waliochukua fomu za kugombea watatakiwa kurudisha ndani ya muda ulioelekezwa katika matangazo ya uchaguzi na huku akihimiza fomu hizo zijazwe kwa usahihi. 

Ameeleza kuwa wasimamizi wa uchaguzi wataratibu maandalizi ya siku za usaili na uchaguzi, wakishirikiana na viongozi wa chama hicho.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Manyara, Derick Magoma amesema ngazi za msingi na kata wameshafanya uchaguzi wao, wanajiandaa ngazi ya majimbo.

“Jimbo la Babati mjini watafanya uchaguzi wao Juni 15 kisha watafuata jimbo la Babati vijijini, kisha  jimbo la Hanang na kumalizia majimbo mengine ya Simanjiro, Kiteto, Mbulu mjini na Mbulu vijijini,” amesema Magoma.

Amesema hivi sasa wapo kwenye mchakato wa wanachama wao kutumia kadi mpya za kielektroniki na kuachana na kadi za karatasi kama takwa la kikatiba linavyotaka.

“Baada ya uchaguzi wa ngazi za msingi na kata kufanyika tupo katika mwendelezo wa kufanya uchaguzi wa majimbo kisha tutafika katika ngazi ya mkoa na kanda,” amesema Magoma.

Related Posts