Chozi la DC akidai kupewa tuhuma uvunjifu maadili

Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amelia mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, akidai amebambikiwa tuhuma za uvunjifu wa maadili baada ya kuwabana watumishi kwa ubadhirifu.

 Buswelu alifika mbele ya baraza hilo leo Juni 4, 2024, akituhumiwa kutoa lugha ya matusi au chafu, kuwaweka ndani watumishi wa halmashauri na fundi ujenzi kinyume cha sheria.

Akijitetea mbele Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji mstaafu Rose Teemba, Buswelu, aliyekuwa akikatisha ushahidi ili kufuta machozi, amesema hakutoa agizo la mtu yeyote kukamatwa wakati wa majumuisho ya mbio za Mwenge wa Uhuru na wala hakutukana wakati walipokuwa wakikagua miradi.

“Wakati nakuja hapa sikujua anayenishataki, lakini baada ya kufika ndipo nikajua mmoja wa watu wanaonishtaki ni Halima (hakutaja jina la pili) ambaye ni mke wa mmoja wa viongozi, ambaye ndiye aliyepewa zabuni ya kununua matofali,” amesema.

Amedai kiongozi huyo alihusika katika ununuzi wa matofali ya ujenzi wa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwenye hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Buswelu amesema walipeleka matofali yasiyo na ubora unaotakiwa katika ujenzi huo.

Amedai kiongozi huyo pia alihusika katika kupeleka vyakula katika Shule ya Msingi Mwakangombe na kwamba, baadhi ya vyakula havikupelekwa na vingine vilipelekwa kwa bei ya juu.

Mkuu huyo wa wilaya amedai gunia la mahindi ambalo linauzwa Sh50,000 wao waliliuza shuleni kwa Sh130,000, jambo ambalo liliwachefua pia wanakamati wa shule hiyo.

Buswelu amedai alichokifanya ni kukaa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tanganyika na kumwagiza afanye upya mapitio ya zabuni ya chakula.

“Ni mazingira tu yametengenezwa katika jambo hili. Nayasema haya kwa kuwa najua kuwa mtafuatilia kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan na nchi hii. Tangu nikae katika ofisi ile sijawahi kumweka mtu ndani,” amesema.

Ameshauri baraza kwenda kwenye vitabu vya polisi kuangalia kama aliwahi kumweka mtu yeyote ndani tangu alipofika kwenye wilaya hiyo.

Buswelu amekatisha maelezo akafuta machozi kwa kutumia ‘tishu’ kisha akaendelea kusema hata kauli kwamba alitoa lugha ya matusi alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa katika majumuisho wa mbio za Mwenge ni uongo.

“Kile ni kikao kikubwa sana, sijawahi kumwakilisha kama mmoja wa mashahidi alivyosema. Kile ni kikao kikubwa sana mimi siwezi kumwakilisha,” amedai.

Wakili wa Serikali, Hassan Mayunga alipomhoji iwapo maelezo anayodaiwa kuyatoa wakati walipoenda kumhoji ni ya kwake, Buswelu amesema karatasi ya mwisho tu yenye saini ndiyo maelezo aliyoyatoa alipohojiwa.

Amesema kwa kuangalia karatasi moja tu aliyotia saini ndiyo yenye maelezo yake na nyingine hazifahamu kwa kuwa karatasi zote zilizoandikwa wakati wa mahojiano aliziweka saini.

Awali, shahidi wa kwanza katika shauri hilo, Leonard Kansimba, ambaye ni Ofisa Uchunguzi Nyanda za Juu Kusini, amesema walipokea malalamiko kutoka kwa watumishi wanne na mwananchi mmoja.

Amesema waliandaa mpango wa uchunguzi ulioidhinishwa na Kamshina wa Maadili.

Amedai katika mahojiano hayo, Ofisa Elimu wa Kata ya Kasegese, Wilaya ya Tanganyika, Lucas Machali, alidai kutukanwa matusi machafu kwenye mkutano wa hamasa ya kilimo cha pamba baada ya kuchelewesha vyombo vya muziki.

“Kwa nini umechelewesha mkutano ondoa *** yako hapa, pumbavu,” amesema na kuongeza kuwa pia alimtishia kumpiga kofi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kakoso, Raymond Bernard ambaye ni shahidi wa pili katika shauri hilo,  amedai alitolewa maneno machafu na mkuu huyo wa wilaya wakati wa ukaguzi wa awali wa miradi inayokaguliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru.

“Mkuu wa shule huna akili, unachokiweza ni kubeba *** umejaa *** kila sehemu lakini bado hujakomaa, kwa hiyo hufai kuwa mkuu wa shule,” amesema akitoa ushahidi dhidi ya kiongozi huyo.

Amesema kwa upande wa Halima Kitumba, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii yeye alitolewa lugha mbaya kwa kusema:

“Wewe mwanamke una kiherehere sana huna adabu, kwa nini ulinipigia simu zako za usiku kumbe ni upumbavu mtupu.”

Amedai aliyekuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanganyika, Geofrey Mwashitete pia alitoa maelezo kuwa Mkuu wa Wilaya alimtolea maneno machafu mkuu wa shule ya sekondari Kakoso, Raymond akisema:

“Nitakunyoa ndevu na *** kwa chupa” na kumtishia kuwa atamtoa koromeo.

Alidai Ofisa Elimu ya Awali na Msingi wa halmashauri hiyo, Gedion Bunto pia alitukanwa kuwa hana akili.

Shahidi wa tatu, ambaye ni fundi ujenzi, Primo Kampamba, amedai alipelekwa kituo cha polisi kwa maelekezo ya mkuu wa wilaya kuwa atolewe Jumatatu bila kuelezwa sababu za msingi, ingawa alikaa nyuma ya kaunta ya polisi hadi saa tano usiku. Amedai katika mradi huo, kazi yake ilikuwa kujenga tu na kwamba, suala la ununuzi wa vifaa lilifanywa na kamati ya ujenzi.

Akihitimisha shauri hilo, Jaji mstaafu Teemba amesema baraza litafanya tathimini na uchambuzi, watakaobaini watawajulisha.

Aidha, katika taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Maadili Tanzania, Jaji mstaafu Sivangilwa Mwangesi, Juni 7 mwaka huu, Baraza litasikiliza shauri la uvunjifu wa maadili linalomkabili Diwani wa Kata ya Cheyo, iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Related Posts