MAKONDA KAMA NAKUELEWA HALAFU SIKUELEWI HIVI …ILA NAKUPA TANO

Na Said Mwishehe

MAKONDA, Najua kwa sasa wewe ndio bosi wa Mkoa wa Arusha,Mkoa wenye raha za Utalii,Mkoa wenye Madini na Mifugo.

Najua Makonda ndio Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkoa wenye watu wakarimu, watu wapole, wacheshi, watu ambao ukizingua nao wanakuzingua. Si unajua tena Arusha ina Wameru, Waarusha na makabila mengine, hata sisi wa Morogoro Arusha tuko pia.

Ndio tupo kule Ngaramtoni ukifika Kibao cha Dodoma uliza kwa mzee Mpogoro utatukuta tena tumejaa tele. Tunashida gani na Arusha ya wote.

Lakini pia kabla sijasahau najua Makonda uko katika Mkoa wenye wananchi wapambanaji, wananchi wanaojua kuisaka na kuitega hela. Utawaambia nini watalii wote wanaanzia Arusha halafu ndio wanakwenda kwingine.

Sijasahau Arusha ndio yenye kizazi OG, kizazi ambacho maisha yake kinayajua wenyewe. Ni kizazi ambacho wanachozungumza na kutenda wanajua wenyewe .

Arusha ya Makonda ndio inayoishi wale jamaa wanajiita Wadudu yaaani Haina kwere, saizi ya viatu vyao inaanzia 50 kwenda mbele, unakuta Mdudu amevaa tairi ya gari, halafu anatembea kwa madaha, kichwani amekata nywele staili ya Papa Upanga…Chuga noma sana jombaaa.

Ni Wadudu haswaa,ukitaka kujua Wadudu wanafananaje muulize Makonda atakueleza vizuri. Nakumbuka baada ya kutua Arusha Makonda alikutana na Wadudu pamoja na Kizazi OG, hakuna mbaya yaani maflekeflekeche tu .

Unamjua Kenyonyo kale kajamaa kafupii hivi,machachari sana.Ni Kenyonyo wa kizazi OG.Ufupi wa Kenyonyo ni kama ule wa Zakayo wa kwenye Biblia kwa waliobahatika kumuona kama mimi.

Hivyo nikiri mimi binafsi najua Makonda ndio Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Watanzania wanajua hivyo. Unabisha nini sasa? Kwani taarifa ya Zuhura Yunus wa Ikulu hukuiona alipoitoa baada ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kumteua Makonda kuwa RC wa Arusha? Acha kuzingua.

Sawa tufanye hukuona alipoteuliwa,Je mikutano yake anayoifanya katika Wilaya za Mkoa wa Arusha hujaiona? Kama hujaona hiyo sio shida yetu, ni shida yako,lionee kwanza…..

Achana na hayo niliyoanza nayo hapo juu,Sasa ngoja nizungumze japo kidogo kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda. Makonda ninayemzungumzia ni huyu aliyezaliwa Februari 15, 1981 katika kijiji cha Koromije, wilayani Misungwi, mkoa wa Mwanza.

Namzungumzia Makonda aliyepata umaarufu wakati wa kura ya maoni ya marekebisho ya Katiba ambapo alikuwa miongoni mwa wanachama wachache wa kikao maalumu cha Bunge la Katiba, waliotumwa kuandaa rasimu ya Katiba mpya.

Baadaye alipata umaarufu zaidi katika siasa za Tanzania, kwanza akiwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni halafu Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam chini ya Rais Hayati. Dk.John Magufuli.

Namzungumzia Makonda ambaye alipokuwa Dar es Salaam alianzisha vita dhidi ya vitendo vya dawa za kulevya,Ushoga na Ukahaba. Namzungumzia Makonda aliyekuwa na mipango mbalimbali ya kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kinara katika mambo mbalimbali.

Hakika wanaume wa Dar tunamkumbuka Makonda na kampeni ya kuzungumza na wanawake ambao walizaa na wanaume kushindwa kutoa matunzo ya watoto. Alizua gumzo sana,wanaume wakaona sasa hii balaa .

Namzungumzia Makonda ambaye Januari 2020 Marekani ilitangaza kwamba Makonda na wanafamilia yake watapigwa marufuku kuingia Marekani kwa tuhuma ya kukandamiza haki za binadamu.

Namzungumzia Makonda ambaye Oktoba 22, 2023 Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilimteua kuwa Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi na Aprili 2024 aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Hata hivyo jamani tukiri na tuwe wakweli si unaona anayofanya sasa Makonda huko Arusha? Tuzungumze polepole wasije kutusikia. Ujue Makonda kote ambako amepita hakuna asiyejua, hakuna asiyemsikia, hakuna asiyemuona. Makonda bwana …ana balaa sana.

Makonda ni aina ya watu wa LIWALO NA LIWE, Makonda ni aina ya watu MWAGA MBOGA, NAMWAGA UGALI, Makonda ni aina ya Watu wa SEMA SU…..Najua unanielewa naamanisha nini. Makonda ni wale watu mtaani tunawaita Wababe wa Kitaa, akipigwa sawa, akikupiga kaa mbali.

Akiwa Katibu wa Itikadi pale CCM amefanya mengi kupitia ziara zake alizofanya katika mikoa mbalimbali. Amepita na kuzungumza na wananchi, akatatua shida zao na akasikiliza changamoto zao. Ingekuwa kwenye mikutano ya Dini tungesema watu walipata uponyaji. Makonda bwana kuna muda na muelewa halafu kuna muda simuelewi kabisa.

Yaani Makonda unapomuangalia mchana anavyoshughulikia changamoto za wananchi tu, anavyowapiga Spana, anavyowabananisha kisawasawa, basi unabakia unajiuliza huyu jamaa mbona kama anachukua Sheria Mkononi? Mbona kama Mbabe? Mbona kama KAULI zake hazina staha, Mbona kama anavuka mipaka?

Ukimuangalia Makonda anavyoshughulikia matatizo ya wananchi wa Arusha unajiuliza huu ujasiri anautoa wapi. Kuna wakati nashindwa kumuelewa, Kuna muda naona Kama vile kwenye nafasi ya Mkuu wa Mkoa siku zake zinahesabika. Ukimuangalia anavyoshughulika na wakuu wa idara unaona kama vile haeleweki haeleweki hivi. Hiyo ni mchana, yaani mchana ukimuangalia Makonda unamuona kama vile NIGUSE NIKUFUMUE.

Lakini huyo huyo Makonda kaa zako usiku ukiwa umetulia muangalie vizuri kupitia mitandao ya kijamii unabaini kumbe jamaa ni bonge la Kiongozi, unabaini jamaa Mungu amempa uwezo mkubwa wa kushughulika na changamoto za watu.

Ukimfuatilia Makonda kwa umakini unabaini ana huruma dhidi ya anaowaongoza,unabaini ana unyenyekevu mkubwa. Ukikaa kwa kutulia unamuona Makonda alivyo na nia njema na wananchi wa Arusha. Ndio kwa Makonda Nyeupe ni nyeupe na Nyeusi ni nyeusi. Ana misimamo sana huyu jamaa.

Unapoangalia aina ya uongozi wa Makonda ni ule uongozi KOSEA nikunyooshe….angekuwa mchezaji Makonda kuna wakati namuona kama Chama Mwamba wa Lusaka vile pale uwanjani lakini matokeo yake ni ya ushindi.

Achana na Chama wa Simba turejee kwa Makonda huyu asiyekubali kushindwa. Ukimkosoa ndio kama unamwambia Ongeza Huyu jamaa kiboko sana.

Pamoja na yote na hapa nieleweke Sitaki kusema Makonda anakosea au anapatia lakini ukweli Makonda ni kati ya Wakuu wa Mikoa wa Wachache ambao wanauelewa wa Rais Dk .Samia anataka nini kutoka kwao. Rais amekuja na kanuni ya R nne na Makonda anazitendea haki haswaaa.

Rais alitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa kwenda kuzungumza na wananchi na kutatua changamoto zao, kazi hiyo Makonda anaifanya kwa zaidi ya asilimia 100. Makonda hana muda wa kupoteza, muda mwingi kwa wananchi akitatua shida zao.

Najua upinzani mkubwa ambao anaupata Makonda unatokana na aina ya uongozi wake, jamaa anatamka maneno mazima mazima, hapo ndipo shida inapoanzia .

Binafsi huwa namuona kama anakosea lakini ukimtafakari unaona yuko sawa. Unadhani kwa wazembe unapaswa kutumia lugha gani zaidi ya anayotumia Makonda .

Nadhani tumpe maua yake japo tunamkosoa. Natamani tuwe na akina Makonda wengi na kwa ngazi mbalimbali, changamoto itakuwa katika kumsikiliza matamko yao…Nchi itakuwa ya Moto sanaaaaaa. Acha tuendelee na tulio nao kwenye Mkate wanasema Nkate.

Makonda piga kazi, endelea kuwapiga Spana lakini basi ndio upunguze tena ukali wa maneno .Watakuelewa tu, watakusikiliza .Au kama vipi basi ruka nao tu hadi kieleweke.

Halafu kuna jamaa namuona hapo anamwambia mwenzie eti najipendekeza kwa Makonda. Acha mambo yako, acha ushamba weweee, Makonda na mimi ni mbingu na ardhi, Sina pa kuonana naye Wala kuzungumza naye. Sina urafiki wala ukaribu. Namuona kwenye mitandao tu kama wewe. Kwanza Ncheke miyee, Niko zangu Majohe napiga fundo tu la Pepsi baridiiiiii.

0713833822.

Related Posts