Mpina atakiwa kuwasilisha ushahidi wa Bashe kusema uongo bungeni

Dodoma. Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amempa siku 10 Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kuwasilisha uthibitisho kwamba Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe amelidanganya Bunge.

Dk Tulia ametoa maelekezo hayo wakati akiahirisha Bunge leo Jumanne ya Juni 4, 2024 baada ya mbunge huyo kudai, “Waziri Bashe amesema uongo na amevunja sheria.”

Wakati wa mabishano ya hoja kati ya Bashe na Mpina kuhusu uingizaji wa sukari ya nje, Dk Ackson amemuliza Mpina kwa kutumia kanuni ya 70 kwamba ana hakika waziri anasema uongo. Mpina amejibu “anasema uongo na kuvunja sheria.”

Kufuatia hali hiyo amesema kwa mujibu wa kanuni ya Bunge ya 70 anayesema mbunge au waziri amesema uongo ndiye anatakiwa kuleta uthibitisho.

“Naomba ieleweke siyo kwamba namuweka Mpina kwenye kona,” amesema Spika. Mpina anatakiwa kuwasilisha ushahidi wake Juni 14, 2024.

Hoja iliyosababisha Mpina kutakiwa kuwasilisha uthibitisho inahusu kiwango cha uagizaji wa sukari ya ziada nje ya nchi katika kipindi ambacho viwanda vinakuwa vimesimamisha uzalishaji.

Mpina amedai kwa mujibu wa sheria uagizaji wa sukari nje ya nchi kwa ajili ya kuziba pengo unatakiwa uwe takriban tani 150, 000 na  zabuni itangazwe.

Hata hivyo, Mpina amedai Wizara ya Kilimo haikutangaza zabuni na imetoa vibali kwa wasioruhusiwa na sheria kupata kibali cha kuagiza sukari nje, ikiwamo kuangiza tani nyingi zaidi ya tani laki nne.

Akijibu hoja hizo Waziri Bashe amesema hakuna zabuni kwa uagizaji wa sukari ya kuziba pengo kutokana na viwanda vya ndani kusimamisha uzalishaji kwa miezi mitatu ya msimu wa mvua.

Pia, Bashe amesema walitoa vibali kwa viwanda vya ndani kuagiza sukari, lakini hakuna kiwanda kilichoingia hata kilo moja ya sukari na kusababia kilo moja ya sukari kuuzwa hadi Sh10, 000.

Bashe amesema viwanda hivyo vilionekana kula njama ya kupanga bei baadaye, kwa kuingiza sukari na kuifungia kwenye maghala yao.

“Tumekwenda na Polisi kufungua maghala yao walikoficha sukari. Siwezi kuwa waziri ‘boya’ kuangalia wananchi wanavyoumizwa,” amesema.

Pia, Bashe amesema viwanda hivyo kwa ajili ya kula njama ya kupanga bei, vimeweka msambazaji mmoja wa sukari kwa mikoa zaidi ya kumi.

“Tunakwenda kuweka utaratibu wa kuondoa njama za kupanga bei kwa kila mkoa kuwa na msambazaji mmoja wa sukari,” amesema.

Pia, Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba naye amemjibu Mpina kuhusu hoja yake kwamba Tanzania imewekwa kwenye uangalizi kwa madai kwamba miamala trilioni 280 ya fedha chafu imepita nchini.

Mwigulu amesema ni kweli hali hiyo ilitokea mwaka 2021 na Serikali imechukua hatu kudhibiti hali hiyo na kwamba wakati wowote nchi itaondolewa kwenye hatua ya uangalizi.

Kuhusu hoja zingine za wabunge, Mwigulu amesema zile za ushauri watanzifanyia kazi na mengine yatajionesha kwenye bajeti ya Serikali.

Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Fedha ya Sh18.17 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Related Posts