Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Profesa Abel Makubi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.
Kabla ya uteuzi huo Profesa Makubi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Hayo yamebainishwa leo Juni 4, 2024 kwa taarifa iliyotolewa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus.
Prof Makubi anachukua nafasi ya Dk Alphonce Chandika ambaye amemaliza muda wake.
Juni 8, 2023 Rais Samia alimteua Profesa Makubi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MOI akichukua nafasi ya Dk Respicious Boniface ambaye alimaliza muda wake.
Kabla ya uteuzi wa MOI, Profesa Makubi amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo.
Pia, amewahi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali katika kipindi cha miaka michache ya Serikali ya Awamu ya tano, akitokea Hospitali ya Bugando ambako alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo.