CCM yawapongeza Mbowe, Lissu kuongoza maandamano

Hai. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amempongeza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu wake-Bara, Tundu Lissu kwa kufanya maandamano kwani yanakisaidia katika medani za siasa za kimataifa, kuonyesha Tanzania kuwa na demokrasia ya kweli.

Dk Nchimbi amesema hayo leo jioni Jamanne, Juni 4, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Bomang’ombe, Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.

Amesema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Rais Samia Suluhu Hassan ameendeleza demokrasia ndani na nje ya chama, ikiwemo kuruhusu maandamano ya Chadema ambayo yanachochea uhuru wa wananchi.

“Lakini Watanzania uhuru wao wa kuchagua na kuchaguliwa uendelee kuwa mkubwa na uhuru wa kutekeleza saisa uendelee kuwa mkubwa na uhuru unakuwa kwa vitendo na ndio maana kuna wakati tunawalaumu hata wapinzani kwa maandamano, pengine yasiyo na tija, lakini wanatusaidia sana kufanya kazi ya kuiambia dunia kwamba Tanzania kuna demokrasia ya kutosha,” amesema.

Katika kusisitiza hilo, Dk Nchimbi aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amesema: “Kwa hiyo wakati mwingine wanafanya kazi yetu.”

 “Nikiwaona mheshimiwa Mbowe na Tundu Lissu wakitokwa jasho kwenye maandamano moyoni mwanangu nasema mnatusaidia kazi baba, na ingekuwa wanahitaji malipo ya kufanya kazi, walahi ningewalipa.”

Akisisitiza, Dk Nchimbi amehoji: “Hivi ukiamka ukakuta mtu amefagia uwanja wa nyumba yako utakasirika? Tundu Lissu na Mbowe wametusaidia kufagia uwanja, wanatufulia nguo zetu, Mungu atupe nini, tunawashukuru sana kwa kufanya kazi ya CCM ya kutangaza kwamba demokrasia kwenye nchini hii ipo.

Mafuwe: Miaka 25 hatukuona kitu

Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mambo mengi, hivyo  wana uhakika katika chaguzi zijazo watafanya vizuri.

Amesema kwenye jimbo hilo kwa miaka mingi likiwa chini ya upinzani halikupata maendeleo.

 “Tulikuwa na watu hapa miaka 25 hatukuona walichokifanya, leo maendeleo ambayo tumayafanya ni historia ndani ya Wilaya ya Hai, tupelekee salamu kedekede kwa Mama Samia kwa mambo ambayo ameyafanya.

Katika kipindi hicho, wabunge walioongoza jimbo hilo ni Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema (2000-2005 na (2010 hadi 2020) na Godwin Kimbita wa CCM (2005-2010). Serikali wakati wote huo ilikuwa ya CCM.

“Nilisimama hapa nikawaambia wananchi wa Hai, suala la maji yatakwenda kupatikana, nilipiga kelele kwelikweli bungeni, miongoni mwa wabunge wanaouzungumza zaidi bungeni ni mimi Saashisha Mafuwe,” amesema Mafuwe.

Amesema kwa sasa tatizo la maji Bomang’ombe limekwisha.

“Tulipewa Sh3.39 bilioni katika mradi wa maji na kuna mradi mkubwa kule Mkalama unaendelea, tunahakikisha maji yanapatikana ya kutosha.

Kuhusu sekta ya afya, amesema Hospitali ya Wilaya ilisahaulika lakini kwa sasa kuna chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kimejengwa kipya, leo tuna jengo la mama na mtoto limejengwa na magari mawili ya wagonjwa.”

Mbunge huyo amesema sekta ya elimu imepiga hatua lakini akabaianisha shule nyingi zilijengwa tangu mwaka 1952, hivyo ni chakavu.

Kuhusu hilo, Dk Nchimbi ameitaka Wizara ya Elimu na Tamisemi kufanya utafiti wa shule zote chakavu ili kuzifanyia maboresho ili ziwe katika mazingira mazuri.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Serikali imeleta Sh829 bilioni ndani ya miaka mitatu za utawala wa Rais Samia zimepelekwa mkoani humo kwa ajili ya miradi mabalimbali ya maendeleo.

“Wananchi wa Hai hawataki maneno wanataka maendeleo,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema “mwaka huu tutakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani kutakuwa na uchaguzi Mkuu, kwa haya mambo mazuri ambayo Rais Samia amefanya tunaomba muendelee kutuamini, itakapofika uchaguzi tuwachague viongozi wa vijiji wenye bendera ya CCM.”

“Tunataka tushinde uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kishindo, ili tuwapelekee salamu kwamba mwakani tutachukua udiwani, ubunge, na Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan. Tuendelee kuhamasishana mafanikio haya tulipopata ni kwa sababu ya mipango mizuri ya Chama cha Mapinduzi,” amesema.

Related Posts