Huduma za Posta zitumie teknolojia ya kisasa

Arusha. Serikali imewataka wataalamu kuitumia teknolojia ya Habari na Mawasiliana (Tehama) kuboresha huduma za Posta barani Afrika, baada ya kukua kwa teknolojia na matumizi ya mitandao kutajwa kama changamoto kwenye utendaji wake.

Ushauri huo umetolewa jana Juni 3, 2024 na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Mzee Suleiman Mndewa wakati akifungua vikao vya wataalamu wa Posta jijini Arusha, kwenye mkutano wa 42 wa Baraza la utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) uliohudhuriwa na nchi 46 za Afrika.

Mndewa amezitaka nchi za Afrika kutumia teknolojia katika utoaji wa huduma za Posta ili kupunguza gharama na pia kuongeza ufanisi wa kazi katika sekta hiyo na si kuichukia.

Amesema teknolojia kwa sasa ndio inayoongoza dunia, hasa katika kipindi hiki nchi za Afrika zinapoelekea kwenye uchumi wa kidigiti, hivyo haiwezi kuepukika katika utoaji wa huduma.

Dk Mndewa amesema matumizi ya teknolojia ndio ulimwengu wa sasa unataka katika kupunguza gharama na kuleta ufanisi wa huduma kwa kuwa dunia inaelekea kwenye uchumi wa kidigiti.

“Changamoto kubwa katika huduma za posta ni teknolojia, lakini sasa huwezi kuikwepa kutokana na dunia kuelekea huko. Bila uchumi wa kidigiti hivi sasa hutoweza kushiriki kwenye maendeleo ya kimataifa,” amesema.

“Ndio maana lazima wataalamu wa Posta wa nchi za Afrika wafanye pia uwekezaji kwenye miundombinu ya mawasiliano,” ameongeza.

Amesema kadri miundombinu itakavyokuwa imewekwa, hasa rasilimali watu, wenye kujengewa uwezo mara kwa mara na teknolojia wakitumika zaidi, ufanisi utapatikana.

Awali, Katibu Mkuu wa Papu, Dk Sifundo Moyo amesema kuwa lengo la mkutano huo kujadili fursa, changamoto na suluhisho ili kuboresha huduma za posta katika kuleta ufanisi na kupunguza gharama.

“Jambo moja kubwa hapa ni kuona jinsi gani teknolojia pia inaweza kusaidia katika huduma za posta ikiwemo matumizi ya akili mnemba, ambayo tunaamini ni rahisi na itafikia watu wengi kwa wakati mmoja popote walipo, lakini pia itapunguza gharama,” amesema Dk Moyo.

Amesema Mpango wa Posta ni kuhakikisha changamoto zote zinazoikabili sekta hiyo zinapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na nchi zingine zilizopiga hatua kwenye utoaji wa huduma za Posta.

Naye Postamasta Mkuu, Maharage Chande amesema kutokana na mchango wa Posta katika ukuaji wa kiuchumi, ndio sababu iliyowakutanisha wataalamu hao kujadili utatuzi wa changamoto katika huduma zake na kuona fursa zilizopo, ili kuchangamkia na kunufaika zaidi.

“Mchango wa huduma za posta kiuchumi ni pamoja na kusaidia kurahisisha biashara katika nchi zetu za Afrika kwenda mabara mengine,” alisema.

Hivyo, aliwataka wataalam wasikubali teknolojia ichukue nafasi ya Posta, bali wajipange kuitumia kama fursa ya kukuza huduma zao zaidi.

Related Posts