Polisi watatu kizimbani wakidaiwa kupokea rushwa ya Sh55 milioni

Songwe. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Songwe imewafikisha mahakamani waliokuwa askari polisi watatu wakishtakiwa kwa kuomba na kupokea rushwa.

 Askari hao waliokuwa wanahudumu katika Kituo cha Polisi Tunduma, wilayani Momba, wanashtakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh55 milioni.

Washtakiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Momba, iliyopo eneo la Chapwa mjini Tunduma leo Juni 4, 2024.

Kabla ya kufikishwa mahakamani na Takukuru, walifukuzwa kazi ndani ya Jeshi la Polisi baada ya kushtaakiwa kijeshi kwa tuhuma hizo.

Washtakiwa ni Enock Marando (43) na Samson Kalebe (38), waliokuwa na vyeo vya Koplo na Zawadi Malakasuka (39) aliyekuwa Konstebo wa Polisi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba, Timoth Lyon, mwendesha mashtaka wa Takukuru, Simona Mapunda amedai washtakiwa walitenda makosa hayo, Machi 7, 2024 katika mpaka wa Tunduma.

Mapunda amedai siku ya tukio washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Jeshi la Polisi waliomba rushwa Sh55 milioni kinyume cha kifungu cha 15 (1) na (2) cha makosa ya rushwa.

Imedaiwa waliomba kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mfanyabiashara Halima Abdallah ili wamsaidie baada ya kumkamata akiwa na shehena ya vipodozi vilivyopigwa marufuku.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka katika kesi ya rushwa namba 15094 ya mwaka 2024 wamekana kutenda makosa hayo.

Hakimu Lyon ameahirisha shauri hilo hadi Juni 18, mwaka huu, kesi itakapoitwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wamekosa dhamana na kurejeshwa mahabusu baada ya wadhamini wao kushindwa kukikidhi masharti yaliyowekwa na mahakama.

Masharti yaliyotolewa na mahakama yalimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya Sh22.5 milioni kila mmoja.

Sharti lingine limewataka kuwasilisha dhamana ya maandishi ya Sh19 milioni kila mmoja.

Related Posts