Majaliwa aagiza mrejesho wa michango ya maafa kwa jamii

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa  na wilaya kutekeleza wajibu wao wa kutoa mrejesho kwa jamii juu ya michango, kazi zilizofanyika na kiasi cha fedha kilichotumika katika maafa pindi yanapojitokeza.

Majaliwa amesema hayo leo Alhamisi Aprili 18, 2024 wakati akijibu swali la papo kwa hapo kwa Mbunge wa viti maalumu Agnes Hokororo.

Agnes amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na majanga kama vile moto na yale ya asili hasa katika majengo ya umma.

Hata hivyo, amesema kumekuwa na mrejesho usioridhisha wa matumizi ya michango hiyo, hivyo kusababisha kutokamilika kwa miundombinu iliyokusudiwa kurejeshwa.

“Je,  Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha michango hiyo inasimamiwa ili kutokukatisha tamaa wadau ambao ni pamoja na Serikali ambao wamekuwa na nia njema ya kuhakikisha hali inarejea katika hali ya asili ili shughuli za umma ziendelee?” amehoji mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema majanga ya moto na maafa ambayo wadau au Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kuwasaidia waathirika yanawekwa katika kundi moja linaloshughulikiwa na kamati za maafa.

“Serikali imeweka utaratibu wa kamati za maafa kwa ajili ya kushughulikia majanga hayo kwenye ngazi ya kata, vijiji, wilaya na mkoa na ile kamati ya Taifa ya maafa ambayo iko chini ya waziri mkuu,” amesema.

Amesema katika ngazi za chini viongozi wakuu ndio wenyeviti wa kamati za maafa na kuwa yanapojitokeza majanga yanaanza kuratibiwa na viongozi wa mahali lilipotokea tukio hilo.

Amesema kama kunakuwa na michango ya kuwezesha miundombinu kurudi katika hali yake ya kawaida, shughuli hizo huratibiwa na ngazi husika.

Amesema baada ya michango hiyo, mwenyekiti wa kamati ya maafa kama ni kwenye ngazi ya mkoa au wilaya anapaswa kuwajulisha wadau wake, matumizi lakini pia kazi iliyofanywa kurejesha miundombinu hiyo.

Majaliwa amesema ofisi ya Waziri Mkuu inayoratibu maafa kitaifa na jukumu lake ni kuona kama mwenendo wa utoaji huduma unaendelea.

Amesema wakuu wa maeneo husika wanatakiwa kutoa mrejesho kwa jamii iliyochangia ili kuwajengea imani na hivyo wakati mwingine ikitokea jambo kama hilo waweze kujitokeza kutoa mchango.

Hali ilivyokuwa kwenye mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang’ mkoani Manyara baada ya kutokea mafuriko mwaka jana.

Majaliwa ametoa mfano wa soko lililoungua la Hamashauri ya Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro kuwa ni jukumu la kutoa mrejesho wa michango ya wadau ni la mkuu wa wilaya hiyo ili kuwatia imani wananchi.

Ametoa mfano mwingine ni shule ya sekondari iliyoungua moto katika Mkoa wa Lindi ambayo alisimama jukwaani kuhamasisha michango kwa wananchi.

Amesema lakini michango yote iliyopatikana haikwenda ofisi ya waziri mkuu bali ilibakia ofisi ya mkoa ambayo ndio mratibu.

“Kwa hiyo Mkuu wa Mkoa wa Lindi anawajibika kwa wananchi wa Manispaa ya Lindi kwanza kuwaonyesha kazi iliyokusudiwa lakini kiwango cha fedha kilichotumika na tathimini itafanywa na wadau. Lengo ni kuwatia imani wachangiaji waendelee kuchangia,” amesema.

Majaliwa amesema hata katika maeneo yaliyopata maafa ya mafuriko ikiwamo Mkoa wa Pwani ni michango mingi imepelekwa na wadau mbalimbali lakini inaratibiwa na kamati ya maafa ya mkoa.

“Nitoe wito kwa wakuu wa mikoa wote nchini, wakuu wa wilaya ambao ndio wakuu wa kamati za maafa za wilaya kwenye maeneo hayo kutekeleza wajibu wao wa kutoa mrejesho wa michango iliyochangwa na jamii ili iweze kuhamasika kutoa michango zaidi,” amesema.

Majaliwa ametoa maagizo pia Wilaya ya Hanang mkoani Manyara kutoa mrejesho kwa jamii ili wadau waliochangia kwenye maafa ya maporomoko ya udongo ya Mlima Hanang wapate imani kuwa michango iliyotolewa imeenda kutumika kama ilivyokusudiwa.

Related Posts