Mauaji ya Kikatili Kanisani- 3

Njombe. Jana katika mfululizo wa simulizi ya mauaji haya ya kikatili tuliwaletea sehemu ya maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya Katekista Daniel Mwalango maarufu kwa jina la Dani, aliyoyaandika akielezea hatua kwa hatua namna alivyotekeleza mauaji.

Katika maelezo yake alisema Februari 7,2022, walikubaliana na Nickson Myamba kukutana ndani ya duka na wakiwa ndani ya duka, alisubiri hadi marehemu awe ‘bize’ kukagua hesabu ndipo atekeleze mauaji, sasa endelea na simulizi hiyo.

Alisema wakati huo alichua kipande cha chuma cha bomba ambacho alikuwa amekihifadhi dukani na kumpiga nacho Nickson kichwani kwa nyuma mara mbili na akaelezea namna alivyoweka karatasi za nailoni sakafuni damu isitapakae.

“Nakumbuka wakati naendelea kufanya mahesabu, Nickson Myamba alikuwa ananibana sana kwa maswali na kwa kuwa nilikuwa tayari nimejenga chuki dhidi yake kwa sababu yeye ndiye alikuwa kinara wa mimi kunitoa pale dukani kuuza duka nikapata hasira.”

“Wakati yeye anaendelea kupiga hesabu mimi nilichukua bomba la chuma ambalo nililichukua katika vyuma chakavu eneo la kanisa siku za nyuma na kulihifadhi dukani na nikampiga nalo kwa kumshtukiza eneo la kichwa kisogoni nilimpiga mara mbili.”

“Akaanguka chini na wakati nampiga alikuwa amesimama. Baada ya kuona amekufa mimi nilichukua panga na kuanza kumkata kuanzia kiunoni na nikamtenganisha sehemu mbili ambapo panga hilo ni mali yangu nilihifadhi dukani siku moja kabla ya mauaji.”

“Kabla sijamkatakata nilitandika mfuko wa kinga njaa (sulphate au Sandarusi) ili damu zisitapakae zaidi chini. Baada ya hapo nilimlaza juu ya mfuko na kuanza kumkatakata vipande viwili viwili ambapo nilianza kumkata kuanzia kiunoni mpaka miguuni.”

“Kipande hicho nilikiweka kwenye karatasi ya kinga njaa na kupaki kwenye boksi la vitabu”, alisimulia Dani na kuelezea namna alivyosafisha sakafu baada ya kumkatakata na baada ya kumaliza alisafisha sakafu, alisafisha pia vifaa vyote alivyovitumia.

Dani alieleza kuwa; “Mimi nilirudi tena dukani na kuanza kudeki damu iliyokuwa imetapakaa kwa kutumia dekio la sweta rangi nyekundu na matambala mengine na ile damu iliyokuwa imetapakaa nilizoa kwa kutumia madekio hayo.

“Baada ya kuzoa niliweka (damu) kwenye ndoo ya plastiki yenye ujazo wa lita ishirini ya rangi aina ya Gold Star na kwenda kuimwaga karibu na uzio na baada ya hapo nilisafisha ndoo na baadhi ya madekio niliyasafisha kwa kutumia maji,”anasimulia Dani.

“Baadhi ya matambala niliyaweka kwenye mfuko wa sukari na kuitupa nyuma ya vyoo, bomba la chuma nililotumia kumpigia marehemu nililificha kwenye bomba la PVC linalopokea maji kutoka kwenye gata hatua chache kutoka pale dukani,” alisema.

“Panga niliondoka nalo hadi shule ya msingi Makambako pana umbali kidogo toka eneo la tukio na kulitupa kwenye shimo la choo cha walimu upande wa wanaume.”

“Simu ya marehemu na funguo za duka na ofisi nyingine niliondoka nazo. Lengo la kugawanya mwili wa marehemu ni kurahisisha namna ya kuubeba na kuupitisha pale getini kwa walinzi na wasingegundua,” anasimulia Katekista katika maelezo yake.

“Lakini nilishindwa kuondoka na mwili huo kwani Katekista mtendaji wa Parokia ya Makambako aitwaye Moses Lubangula alikuwa ananipigia simu sana akiniulizia endapo bado nipo dukani na simu ya marehemu ilikuwa inapigwa sana”

“Mtendaji aliniambia kuwa walinzi wanalalamika kuwa mpaka muda ule saa 4:00 usiku bado nipo dukani nafanya nini, hali hiyo mimi nilipata hofu zaidi. Hivyo wazo la kwenda kuutupa ule mwili mbali na pale kanisani nilishindwa nikaamua kuuacha ndani ya duka”

Huu ndio utetezi wa Katekista

Baada ya mahakama kumaliza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka, ilimuona Katekista huyo ana kesi ya kujibu hivyo kumtaka ajitetee na aliamua kujitetea mwenyewe na kuelezea alikuwapo siku ya tukio na alikuwa akifanya nini siku hiyo.

Alieleza kuwa Februari 7,2022, siku ambayo Nickson Myamba aliyekuwa Katibu wa Kanisa alitoweka alikuwa nyumbani kwake mtaa wa Ndondole hadi saa 10:00 alasiri na baadaye alienda kanisani kusaidia watoto kujaza fomu za mitihani hadi saa 12:00 jioni.

Akaeleza kuwa kuanzia saa 12:00 hadi saa 1:00 jioni, alikutana na kikundi cha walei wamisionari wa Consolata (Wamisco) na baadae akawa na kikao na Baba Paroko hadi muda wa saa 2:00 usiku na kurudi ofisini kwake alilokaa hadi 3:00 usiku akafunga duka.

Baada hapo alirudi nyumbani kwake na kueleza kuwa siku ya mwisho kumuona Nickson Myamba ni siku moja ya Jumapili kabla ya Februari 7, 2022 wakati wa ibada kanisani.

Alijitetea kuwa siku ya tukio hakukutana kabisa na marehemu na kukanusha kuwa Februari 7,2022 aliitwa saa 5:00 usiku na badala yake akaeleza kuwa Justine Sanga alimpigia simu saa 8:00 mchana ya Februari Februari 8,2022, siku moja baada ya mauaji.

Katika simu hiyo, aliulizwa mahali alipokuwa kwa siku hiyo hiyo ya mauaji na kueleza kuwa aliondoka kanisani saa 3:00 usiku na kwenda nyumbani, hapo Sanga akakata simu lakini akapigiwa tena akitakiwa kuhudhuria kikao kanisani, alikataa kwa sababu ni usiku.

Sababu za kusafiri kwenda Dar es Salaam

Ni ushahidi wake kuwa asubuhi ya siku iliyofuata yaani Februari 8,2022 alisafiri kwenda Dar es Salaam kumtembelea binamu yake ambaye siku za nyuma alikuwa amefiwa na mama yake na yeye (Dani) hakwenda kushiriki maziko yake.

Alieleza kuwa Februari 11, 2022  saa 6:00 usiku, akiwa anarudi Makambako alikamatwa eneo la Doma Morogoro na baada ya kukamatwa alipelekwa kituo cha Polisi Morogoro ambako aliambiwa anawekwa mahabusu kusubiri Polisi wanaotoka Njombe.

Kuhusiana na funguo za duka, alisema kulikuwa na funguo mbili, mmoja alikuwa nao yeye na mwingine alikuwa nao Padri Pachal Makoga na akakanusha ushahidi kuwa aliwaongoza maofisa wa polisi na kuwaonyesha alipokuwa ameficha silaha za mauaji.

Hata hivyo, alikiri kwenda kanisani baada ya kukamatwa na Polisi na kueleza kuwa “Tulielekea kanisani pale dukani kwa sababu walikuwa wamezungushia utepe. Tuliingia na baada ya hapo tulitoka,” alinukuliwa Dani akieleza katika utetezi wake huo.

Alichokisema kuhusu maelezo yake

Kuhusiana na silaha anayodaiwa aliitumia kumuua Nickson Myamba, alikanusha kufahamu lolote kuhusiana na bomba la chuma na panga lililopatikana eneo la tukio.

Alipoulizwa kwanini suruali yake ya rangi ya kijivu ikiwa na matone ya damu ilipatikana nyumbani kwake na jibu lake lilikuwa “Nyumbani sikwenda” na alipotakiwa kufafanua kuhusu jibu lake hilo, Dani alijibu tu kwa kifupi “Sijajua”.

Kuhusiana na maelezo ya onyo ya kukiri kosa hilo,Dani alijitetea kuwa baada ya kukamatwa na kufikishwa Makambako Polisi, alipigwa sana na kuwekwa mahabusu.

Baadaye alitolewa mahabusu, na kupigwa sana na kutakiwa kueleza nani anahusika na mauaji ambapo alikanusha na baada ya kutotoa ushirikiano, Februari 12,2022 saa 8:00 mchana alipigwa tena na kutakiwa kusaini fomu ambayo hakujua kilichoandikwa.

Alipoulizwa kwanini hakutoa hoja ya kupigwa wakati maelezo hayo yakitolewa kama kielelezo alisema hakufanya hivyo kwa kuwa hakuwa na fomu ya polisi namba 3 (PF3) na akaeleza kuwa mashitaka dhidi yake yametengenezwa na kesi hiyo ni ya kubambikwa.

Alieleza kuwa kwa kuzingatia umbali kati ya duka la vitabu na geti kuu, isingekuwa rahisi kwa jambo lolote kutokea dukani  bila walinzi waliopo getini kusikia chochote.

Alijenga hoja kuwa walinzi walikuwapo getini muda wote mpaka muda wa saa 3:00 usiku alipoondoka kwenda nyumbani,  hivyo ni vigumu mauaji kufanyika ndani ya duka bila walinzi kung’amua na kwamba hakuna ushahidi kuwa alionekana akiwa na marehemu.

Usikose sehemu ya tatu kesho tukiwaletea namna jaji alivyochambua ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri na ule wa mshitakiwa na kumtia hatiani kwa kosa la mauaji kisha kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Related Posts