Makampuni wazawa wapewa kipaumbele utekelezaji mradi wa LTIP

Asilimia themanini (80%) ya kazi zote za urasimishaji mijini kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) zitatekelezwa na Makampuni binafsi yaliyosajiliwa kufanya kazi za upangaji (mipango miji) na upimaji wa ardhi na asilimia (20%) ya kazi hizo zinatekelezwa na Serikali kupitia watumishi walioko katika Halmashauri husika.


Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Meneja Urasimishaji Mjini katika Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Bw. Paul Kitosi wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, tarehe 5 Juni 2024 Mkoani Kilimanjaro.

Alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mradi umepanga kutoa hati 32,000 katika Kata 9 ambapo kazi hii itafanywa na makampuni binafsi na tayari kazi hii imetangazwa kupitia mfumo wa manunuzi ambapo wataalamu washauri (consultants) wanaojishuhulisha na masuala ya mipango miji na upimaji wanatakiwa kuomba kabla ya tarehe 7 Juni 2024.

Ni matarajio kuwa makampuni binafsi yataanza kazi hii mapema mwa mwezi Julai 2024 na kumaliza kwa kipindi kisichozidi miezi nane.

‘‘Kwa kuwa kazi hii itafanywa kwa haraka tunatoa wito kwa wamiliki kuhakikisha kuwa wanakuwepo katika zoezi la kupanga na kupima ili kutoa taarifa sahihi kwa wataalamu lakini pia kama kuna migogoro ya mipaka ya ardhi na umiliki ianze kushughulikiwa mapema kabla ya wataalamu kufika ili kuwawezesha wanufaika kupata huduma’’ alisema Kitosi.


Nae Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi Bw. Shaban Mchomvu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya amesema kuwa wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi huu na kuahidi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wake hasa kwa kuzingatia haki za makundi maalumu.

‘‘Kila kiongozi ajitahidi kusimamia eneo lake na kutoa ushirikiano kwa timu ya mradi ili lengo la kuwafikia na kuwahudumia watanzania litimie kwa kupatiwa hati miliki itakayopelekea kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi, kuongeza usalama wa milki za ardhi pamoja na kukuza uchumi’’ alisema Mchomvu.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi unatambua na kuthamini michango ya sekta binafsi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Mashirika ya Kijamii katika utekelezaji wake.

 

Related Posts