AKIBA COMMERCIAL BANK PLC YAAZIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI KWA KUZINDUA VIUNGA VILIVYOBORESHWA VYA INDEPENDENCE SQUARE, DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaji Jabir Shakimweri, akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi viunga vilivyoboreshwa vya Independence Square, akiwa pamoja na Meneja wa Tawi la Dodoma la Benki ya Akiba, Bi. Upendo Makula (wa pili kushto). Wengine katika picha ni wageni waliohudhuria hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaji Jabir Shakimweri, akikagua viunga vya Independence Square.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaji Jabir Shakimweri, akisalimiana na wafanyakazi wa Benki ya Akiba.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaji Jabir Shakimweri, akihutubia wakati wa uzinduzi wa viunga vya Independence Square vilivyoboreshwa na Benki ya Akiba.
Katika tukio muhimu lililofanyika sambamba na Siku ya Mazingira Duniani (World Environmental Day), tawi la Dodoma la Benki ya Akiba  lilikabidhi rasmi awamu ya pili ya uboreshaji wa viwanja vya Independence Square. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shakimweri, wawakilishi mbalimbali wa vyombo vya habari, na wafanyakazi wa Benki ya Akiba Commercial.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa tawi la Dodoma la Benki ya Akiba, Bi. Upendo Makula, alisisitiza jitihada za Benki hiyo katika  kujitolea  kuhifadhi  na kutunza mazingira, samba samba  na kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani ya mwaka huu, isemayo “Our Land, Our Future” – “Ardhi Yetu, Mustakabali Wetu,” ambayo  imebebwa na mada  kuu ya “Land restoration, desertification and drought resilience”  ambayo  inalenga urejeshaji (utunzaji) wa ardhi, kupambana na uzalishaji wa majangwa, na ukame. Alikumbusha na kusisitiza juu ya wajibu wa pamoja wa kulinda na kuhifadhi mazingira ili kuhakikisha dunia inabaki kuwa mahali salama pa kuishi kwa  sasa na vizazi  vijavyo.
Katika picha ya pamoja ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaji Jabir Shakimweri (katikati), na wafanyakazi wa Benki ya Akiba baada ya hafla ya kuazimisha siku ya mazingira duniani ndani ya viunga vya Independence Square.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaji Jabir Shakimweri, akipanda mti kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani katika viunga vya Independence Square.
Bi. Makula alieleza kuwa Benki ya Akiba inashiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira kwa namna mbali mbali kuanzia kupitia huduma zake na ushiriki wa katika shughuli mbali mbali za kijamii.  Aliainisha kuwa Benki hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya karatasi kwa kuboresha huduma zake za kidijitali, zikiwemo Akiba Mobile, Akiba Wakala, kadi za VISA, taarifa za kielektroniki (E-statement), na huduma za benki Mtandao (Internet Banking). Huduma hizi si tu kwamba zinapunguza matumizi ya karatasi, bali pia huleta urahisi na uhakika, hivyo kukidhi mahitaji ya soko kwa ufanisi. Aidha, benki hiyo inatoa huduma mbalimbali kama mikopo, akaunti, na bima, zinazowafikia wateja tofauti kuanzia mtu binafsi hadi makampuni makubwa na taasisi za serikali.
Vilevile, Bi. Makula alibainisha kuwa Akiba Commercial Bank inashiriki kikamilifu katika shughuli za jamii za kuhifadhi mazingira kama sehemu ya Sera yake ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Mfano halisi ni jitihada zake za muda mrefu za kutunza na kuboresha viwanja vya Independence Square huko Dodoma, jukumu ambalo limekuwa likitekelezwa kwa zaidi ya miaka kumi. Juhudi hizi zinaonyesha nia thabiti ya benki hiyo ya kutunza  na kuhifadhi mazingira   kwa ajili ya urithi bora wa vizazi vijavyo.
Tukio hilo pia lilihusisha kukata utepe na kupanda mti wa kumbukumbu katika viwanja vilivyoboreshwa na Mgeni Rasmi Mh. Mkuu wa Wilaya Alhaji Jabir Shakimweri ya Dodoma. Aidha, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya aliipongeza Benki ya Akiba kwa juhudi na jitohada zake katika kuboresha na kuhifadhi mazingira. Pia ametoa rai kwa taasisi nyingine kuiga mfano wa Akiba.
Bi. Makula, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Silvest Arumasi, pamoja na uongozi na wafanyakazi wote wa tawi la Dodoma, alisisitiza nia ya benki hiyo ya kuendelea kusaidia uboreshaji wa mazingira na miradi mingine ya kijamii, hasa katika sekta za afya na elimu.

Related Posts